Mama

Nani kama Mama .

Afya ya Mimba

Mwanamke anayetaka kubeba mimba anashauriwa aache kunywa pombe na kuvuta sigara.

Mama na Mtoto

Mazingira mazuri ya Afya ni Moja ya njia ya kuepuka matatizo ya mama wakati wa kujifungua.

Tuwalinde watoto

watoto 200 kati ya 100,000 wanapoteza maisha wakati wa kuzaliwa na baada ya kuzaliwa, idadi hii ya vifo ni kubwa sana hapa nchini Tanzania.

Karibu kwenye blog hii kwa Habari za Afya ya Mama na Mtoto.

Kufikia mwaka 2010, takwimu zilikuwa zinaonesha kwamba kila wanawake 454 katika vizazi hai 100,000 walikuwa wanapoteza maisha wakati wa ujauzito au kujifungua kwa matatizo mbalimbali ya uzazi.

watoto 200 kati ya 100,000 wanapoteza maisha wakati wa kuzaliwa na baada ya kuzaliwa, idadi hii ya vifo ni kubwa sana hapa nchini Tanzania..

Wednesday, January 30, 2013

WAKULIMA WA KOROSHO LINDI NA MTWARA WAPONEA BAKARI KICHWA

Wakulima wa Korosho katika Mikoa ya Lindi na Mtwara wako katika hali mbaya ya kipato, baada ya korosho walizokopesha katika stakabadhi ghalani kuanzia mwezi Octobar mwaka jana hawajalipwa mpaka sasa.

"Bakari kichwa na majani ya mhogo au kisavu ndio mboga tunayokula kila siku kwa kutokana na ukata wa kukosa pesa niliyokopesha korosho toka mwaka jana, fungu la Bakari kichwa linauzwa Tshs. 1000 na Bakari kichwa mmoja anauzwa Tshs. 100, hali ni mbaya hata watoto wameshindwa kwenda shule toka imefunguliwa kwa sababu sina kilo 60 ya mahindi, kilo 40 ya maharage na kilo 40 ya mchele pamoja na ada ya shule Tshs. 20000 kwa mwanafunzi wa sekondari," alisema Lidia Chinguile Mkazi wa Masasi Mtwara.

Waziri wa Kilimo na Chakula Mhandisi Christopher Chiza aliwaahidi wakulima wa korosho tarehe 3 mwezi wa 12 mwaka 2012 alipofika katika Wilaya ya Nachingwea Mkoa wa Lindi akiwa katika ziara na Rais Jakaya Kikwete, alisema wakulima wote wa korosho watalipwa pesa zao walizokopesha korosho ghalani baada ya wiki mbili.

Monday, January 28, 2013

UKOJOAJI WA BARABARANI ULIVYOKITHIRI TANZANIA

Baadhi ya abiri wa kwenda Mikoa ya Kusini Lindi na Mtwara, wakijisaidia katika kichaka ambacho kipo karibu na barabarani katika Kijiji cha Ikwiriri Wilaya ya Rufiji Mkoa wa Pwani. Aina hii ya kujisaidia sio tuu kuchafua mazingira pia ni hatari kwa afya inachangia magonjwa ya kuambukiza.

Hivi karibuni Waziri wa Uchukuzi Dr. Mwakyembe alisema kuwa, basi litakalo kamatwa linashusha abiria kwenda kujisaidia kichakani watachukuliwa hatua kali. Je? atatumia njia ipi ili kuwakamata abiria na dereva wa basi? Barabara mbalimbali za kwenda Mikoani hapa Nchi hakuna vyoo vya kujisaidia abiria inawalazimu kujisaidia vichakani na kuchafua mazingira, tena madereva wanajua sehemu maalumu za kujisaidia kwenye vicha mbalimbali mpaka imepelekea sehemu hizo kuwa na biashara kwa sababu abiri hujisaidia kwa dakika tano hadi kumi.

Sunday, January 27, 2013

KUTANA NA ABIRIA WANAONING'INIZA ROHO ZAO BAHARI

Baadhi ya Abiria nilikutana nao kwenye Mtumbwi katikati ya Tanga na Wete nikielekea visiwani Wete Pemba, upakiaji wa abiria kwa kutumia Mtumbwi, Ngalawa, Mashua na Jahazi sio salama kwa wasafiri mbalimbali wanaotumia Bahari, Ziwa na Mto kusafiri.
"Sio kama tunapenda kuning'iniza roho yangu kwa kupanda katika Mtumbwi na mizigo lakini kwa sababu sina pesa Tshs. 16,000 nauli ya kupanda Meli, humu nalipa Tshs. 8000 kutokana na ugumu wa maisha ndio inanilazimu kuhatarisha maisha yangu kiasi hiki ili kubakiza hiyo Tshs. 8000 nikale nyumbani na watoto," alisema Juma Khamis Shoka mkazi wa Wete.
Afisa wa Sumatra Mkoa wa Tanga Bwana Kamata alisema kuwa, ni makosa makubwa kwa mmiliki wa chombo cha aina ya Mtumbwi, Mashua, Jahazi na Ngalawa kusafirisha abiria. Kazi kubwa ya vyombo hivyo ni kusafirisha mizigo mbalimbali na sio abiria, Sumatra wakimkamata nahodha wa chombo anafikishwa Mahakamani na mmiliki wa chombo anafutiwa leseni ya kumiliki chombo hicho.
Kwa sasa Nchini Tanzania huo ndio usafiri wa pekee katika maeneo mengi yenye Bahari, Ziwa na Mto  na ndio vinavyoongoza kwa kuzama na kuuwa abiria.

Monday, January 21, 2013

MAABARA BADO NI TATIZO SUGU KATIKA SHULE ZA SEKONDARI ZA KATA MTWARA

Hicho ndio chumba cha darasa kinachotumika kama maabara katika shule ya sekondari Dr. Alex iliyoko katika Wilaya ya Newala katika Mkoa wa Mtwara, Wilaya hiyo ina shule za sekondari za kata 28 lakini kati ya hizo ni shule nne tuu ambazo zina majengo mbalimbali ya maabara nazo ni Nambunga, Newala day, Nangwanda na Mnyambe.

"Nasoma masomo ya sayansi lakini hakuna maabara ya uhakika ya kujifunza mambo mbalimbali ya kisayansi, kama unavyoona hivyo ndio vifaa vya kujifunzia unaweza kuingia katika darasa hili kwa ajili  kujifunza ukakuta majiko hayana mafuta ya taa ambayo utawesha na kuchemshia baadhi ya madawa, basi tunasoma tuu kwenye vitabu ukifika mtihani wa vitendo unaferi kwa sababu hujui chochote cha kufanya unapata sifuri," alisema John Nandule mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari Dr. Alex

Mkurugenzi wa Wilaya ya Newala Abdallah Chikota alisema kuwa, tatizo la ukosefu wa maabara lipo katika Wilaya yake lakini kwa sasa wameanza ujenzi wa majengo ya maabara katika baadhi ya shule za sekondari, lakini itachukua muda mrefu kumaliza na kuweka vifaa vya kisasa, maana majengo hayo yanatakiwa katika shule 24. Wanafunzi wa masomo ya sayansi wasome kwa shida shida masomo hayo kwa sasa lakini baada ya muda tatizo hilo litakwisha.

SHULE ZA SEKONDARI ZA KATA ZAKUMBWA NA UHABA WA MABWENI MTWARA













Mwajuma Ramadhi ni mwanafunzi wa kidato cha tatu  katika Shule ya Sekondari ya Mkoma iliyoko katika Wilaya ya Newala Mkoa wa Mtwara, anayeishi katika nyumba ya kupanga iliyoko karibu ya shule ambayo anasoma kwa mwezi analipa kodi Tshs 2500. 
Pia Athumani Hamza Mwanafunzi wa Kidato cha pili anayesoma katika shule ya sekondari ya Mnyambe iliyoko katika Wilaya ya Newala, naye anaishi katika nyumba ya kupanga kwa mwezi analipa kodi Tshs. 2000, Shuleni Mnyambe kuna bweni la kulala wanafunzi, lakini mzazi wake hana pesa ya kulipia bweni kwa mwaka Tshs.100,000.

"Nasoma kwa shida sana usiku kwa kutokana na nyumba ninayokaa haina umeme wa solar inanibidi kusoma kwa kutumia kibatali, macho yanauma sana kwa sababu mwanga wa kibatari ni mdogo siwezi kuona vema maandishi, na muda mwengine natumia tochi kama nyumbani hawajanipa pesa ya matumizi ikiwa kununua mafuta ya taa, sio tuu pesa ya kununua mafuta ya taa kwa ajili ya kusomea usiku hata pesa ya matuzi nacheleweshewa kutumiwa nyumbani inanilazimu kufanya kibarua cha kuchota maji kwa kutumia baiskeli na kulima mashamba kama kibarua ili nipate pesa ya kununua chakula, wakati wa kufanya kibarua wenzangu wanaendelea na masomo darasani," alisema Mwajuma.
Pesa ya matumizi kwa mwanafunzi wa Newala ambaye anaishi nje ya shule anatakiwa kupewa Tshs. 50,000 pamoja na unga, sukari, majani ya chai, maharage, dagaa, sabuni na mafuta ya taa kwa miezi miwili.

Kwa sasa Wilaya ya Newala ina shule za Sekondari za Kata zipatazo 28 kati ya hizo shule nne tu ndio zinamabweni ya kulala wanafunzi wakike na wakiume nazo ni Nangwanda, Mtangalanga,Kihuta na Mnyambe.

Saturday, January 19, 2013

UKOSEFU WA MAKTABA KATIKA SHULE ZA SEKONDARI ZA KATA BADO NI TATIZO SUGU MTWARA



Hiki ni moja ya  chumba kinachotumika kama Maktaba ya shule ya Sekondari ya Nangwanda iliyoko katika Wilaya ya Newala Mkoa wa Mtwara, Wilaya hiyo inashule za Sekondari za Kata 28 na jengo moja la  Maktaba  katika shule ya  Sekondari ya  Newala day.
"Tunapata shida sana ya kusoma kwa sababu ya kukosa vitabu vya uhakika hapa shuleni, ukitaka vitabu lazima uwende kusoma au kuazima katika shule ya sekondari ya Newala day ambako ni zaidi ya kilometa 7 kutoka hapa ninaposoma mimi tena unatembea kwa mguu, muda mwengine ukifika unamkuta mwalimu anayetunza fungua ya maktaba hayupo amekwenda bank kufuata mshahara basi inakulazimu kurudi shuleni bila ya mafanikio ya kupata kitabu,"alisema Juma Mussa Mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya Sekondari Mtangalanga.
Zaidi ya Shule 27 katika Wilaya ya Newala hazina Maktaba za uhakika ambazo zina vitabu vya masomo mbalimbali wanayofundishwa wanafunzi katika shule hizo, vyumba hivyo vya kusomea kama maktaba  kwa sasa viko katika hali mbaya na havilidhishi kwa mwanafunzi kusoma na kuelewa kile alichokikusudia kusoma.
Mkurugenzi wa Wilaya hiyo Abdallah Chikota alisema kuwa, tatizo la ukosefu wa maktaba katika Wilaya yake ni kubwa sana shule ambazo hazina jengo la maktaba ni 27 kwa sasa, kutokana na  hali hiyo inawalazimu kutumia chumba cha darasa kama maktaba ili waweze kusoma lakini hata hivyo vyumba vya madarasa wanavyotumia kama maktaba viko katika hali mbaya.

 Hali halisi ya ufaulu kwa wanafunzi wa shule hizo bado upo chini kutokana na kutokuwa na sehemu rasmi ya kusomea wakati wa usiku, kwa sasa tumeanza ujenzi wa Maabara katika shule za sekondari mbalimbali tukimaliza ujenzi ndio tutaanza ujenzi wa maktaba katika shule hizo.