"Leo nimeanza kuhudhuria kliniki katika Hospitali ya Sinza kwa mara ya kwanza. Nimefika hapa nimetoa historia ya muhimu kuhusu ujauzito wangu, nikapelekwa kwenye vipimo na nimepimwa kujua kama nina maambukizi ya UKIMWI. Hata hivyo kuna baadhi ya vipimo sikupimwa. Vipimo hivyo ni pamoja na kipimo cha wingi wa damu (HB test), maambukizi ya kaswende na gonorea (VDRL test) na mfumo wa mkojo. Nimeambiwa kuwa vipimo hivyo havipo hospitalini, hivyo natakiwa nikatafute huduma hii kwenye hospitali zingine hususani za binafsi," alisema Mwanahawa Mohamed (25) mkazi wa Sinza Madukani.
Gharama za vipimo katika hospitali za binafsi kama kipimo cha wingi wa damu (HB test) shilingi 3,000, kipimo cha maambukizi ya kaswende na gonorea (VDRL test) shilingi 5,000 pamoja na kipimo cha kutambua kama mkojo mchafu shilingi 3,000.
Tatizo la ukosefu wa vipimo muhimu kwa akina mama wajawazito katika Hospitali ya Sinza ni la muda mrefu sana zaidi ya miezi sita toka mwezi Oktoba mwaka 2012. Toka kipindi hicho kumekuwa na upungufu wa vipimo vya kuangalia magonjwa ya kaswende, maambukizi katika mfumo wa mkojo, kisonono na kujua wingi wa damu.
Mratibu wa Afya ya Mama na Mtoto katika hospitali hiyo Milka Maganga alisema kuwa, tatizo la ukosefu wa vipimo vya wingi wa damu, maambukizi ya kaswende, kisonono na maaumbukizi katika mfumo wa mkojo kwa wajawazito katika hospitali ya Sinza ni la muda mrefu.
Maganga alisema kuwa vipimo hivyo ni muhimu sana kwa akina mama wajawazito wakati wa mahudhurio ya kliniki kwa mara ya kwanza na katika marudio.Aidha alisema kuwa wajawazito wanashauriwa kutumia na kupewa dawa za kuongeza damu na kupewa ushauri juu ya matumizi ya chakula bora, bado anatakiwa kuchukualiwa kipimo cha wingi wa damu kila anapohudhulia kliniki, ili kujua kama damu aliyonayo inatosha au anahitaji tiba ya kuufanya mwili wake utengeneza damu zaidi.
Pia alifafanua kuwa, tutahitaji kujua kama mkojo hauna shida kila mara afikapo kliniki. Huduma zote hizi zinachangia kwa mjamzito kujifungua salama na kuwa na mtoto mwenye afya nzuri.
Maganga alisema kuwa, kuna kipindi wanazaliwa watoto wakiwa na maambukizi ya magonjwa ya zinaa, kwa sababu mjamzito alishindwa kupata huduma hizi muhimu kipindi alichokuwa anahudhulia kliniki, kwa sababu vituo vya afya vya binafsi ambako tunamshauri kwenda kupima kuna huduma za kulipia. Na wajawazito wengi wanashindwa kwenda katika vituo hivyo, kwa sababu ya gharama za vipimo hivyo kuwa ni kubwa ukilinganisha na hapa katika hospitali ya sinza tunatoa bure.
Kwa mujibu wa Maganga alisema kuwa, mwaka jana jumla ya wajawazito 24 walioshindwa kwenda katika vituo vya afya vya binafsi kupima maambukizi ya kasendwe na kisonono, walijufungua watoto walikuwa na maambukizi ya magonjwa hayo na watoto wote walikuwa wamefariki kwa kuugua magonjwa hayo wakiwa tumboni.
Katika Hospitali ya Sinza kwa siku hupokea wajawazito wapya wanaoanza kuhudhuria kliniki wapatao 20.
Kwa upande mwingine wajawazito wa marudio ya kliniki kwa siku hufikia kiwango cha 90 hadi 100. Lakini kwa upande wa zanati ya Tandale wanaohudhuri kwa mwezi Febuari ni 347. Idadi hii ni kubwa ukilinganisha na upatikanaji wa vipimo mbalimbali vinavyohitajika wakati wa ujauzito.
Maganga alisema kuwa, pamoja na wingi huu wa wateja, katika mwanzo wa mwezi tunapewa kikopo kimoja cha vipimo vya wingi wa damu na ndani ya kikopo hicho kunakuwa na vipimo 100 tu. Kikopo hiki kinatakiwa kitumike kwa mwezi mmoja! Hali hii ndivyo ilivyo kwa vipimo vya kaswende,kisonono, damu na mkojo.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa hospitali hiyo Dk. Benedict Luoga alisema kuwa, sio vipimo tu kwa wajawazito wakihudhulia kiliniki, pia kuna uhaba wa upatikanaji wa damu salama kwa wajawazito mbalimbali wanaohitaji huduma hiyo kwa hapa hospitali ya sinza ni tatizo kubwa sana. Mwaka jana zaidi ya wajawazito 120 walifika katika hospitali hii wakiwa na tatizo la upungufu wa damu, na kwa mwezi zaidi ya wajawazito 10 wanahitaji damu.
Mahitaji ya damu salama kwa siku katika chumba cha kujifungulia wajawazito mbalimbali katika hospitali hiyo ni chupa kumi za damu, lakini kuna kipindi wanakosa hizo chupa kumi na kulazimika kuomba katika hospitali ya mkoa mwananyamala.
Aidha alisema kuwa kama kutakuwa na wajawazito ambao wengi wana damu ya kutosha, basi chupa kumi zinatumika kwa muda wa siku tatu, kisha wanakwenda tena benki ya damu katika hospitali ya Taifa muhimbili wakiwa na damu ya kutoa ili waweze kupata damu nyengine.
"Wajawazito wengi wanafika katika chumba cha kujifungulia wakiwa na damu ya units saba, ambayo haitoshi kumsaidia kujifungua salama tunalazimika kumuongezea damu kuanzia units mbili hadi tatu ili aweze kujifungua salama," alisema Luoga.
Mwaka jana tarehe 14 mwezi wa Disemba ilikuwa ni historia kwa kituo hiki. Mheshimiwa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alifungua jengo la Kituo cha Afya Sinza, na kukipa hadhi kuwa Hospitali ya Wilaya ya Kinondoni.
Mabadiliko hayo yalileta matumaini makubwa ya kuboresha huduma za hospitali ikizingatiwa kuwa mabadiliko haya yana maana ya kuongezewa bajeti. Tofauti na mategemeo yaliyokuweko, mabadiliko hayo hayakuenda sambamba na ongezeko la bajeti toka Serikali Kuu pamoja na kupandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Wilaya ya Kinondoni.
"Toka Rais Kikwete afungue jengo la wazazi idadi ya wajawazito imeongezeka mara dufu kutoka 20 kwa siku wanaohitaji huduma ya kujifungua mpaka kufia 50 hadi kufikia 70, hawa wanajifungua kwa njia ya kawaida,"alisema Luoga
Lakini kwa wale wanaofanyiwa upasuaji kwa siku wanafanyiwa watano hadi 10 kulingana na idadi ya vitanda viko 11 tu, hivyo inalazimika kusubiri muda wa siku tatu ili kidonda cha upasuaji kipone kisha ndio anaruhusiwa na kuweza kuwafanyia upasuaji wajawazito wengine. Kwa mwezi wanapokea wajawazito wanaohitaji huduma ya upasuaji kuanzi 87 hadi 100. Pia ongezeko la wahitaji huduma haliendi sambamba na watumishi, dawa na vifaa tiba kwa sasa.
"Kuna wauguzi na manesi 18 tu katika jengo la wazazi,waliokuwa na stashahada 9 na wenye cheti 9, wanatoa huduma kwa zamu asubuhi wanaingia wauguzi na manesi watano, mchana wanaingiza watatu na usiku wanakuwa watatu hawatoshi ukilinganisha na wajawazito wanaofika kwa siku," alisema Luoga.
Tatizo la uhaba wa dawa na vifaa tiba lipo pia katika zahanati ya Tandale, ambako kuna idadi kubwa ya wajazito wanaofika kuhitaji huduma ya vipimo kwa siku wanapokea wajawazito 50 na kwa mwezi wanapokea wanawazito 300 hadi 320.
"Khafsa Shabani (32) mkazi wa Manzese ni uzazi wake wa nne anasema kwa masikitiko, nimefika toka saa 3:00 asubuhi siku ya kwanza kuanza kliniki ndio namaliza muda huu wa saa 6:30 mchana.
Nimepimwa urefu wangu, uzito na urefu wa mtoto alietumboni na hatimae nimepimwa maambukizi ya virusi vya ukimwi, lakini vipimo vya wingi wa damu, kaswende, kisonono na mkojo sijapimwa nimeambiwa vipimo hivyo vimeisha na ninatakiwa kwenda kupima katika hospitali za binafsi." alisema Khafsa.
Kwa upande wake Mratibu wa afya ya mama na mtoto wilaya ya Kinondoni Mary Massay alisema kuwa, tatizo la wajawazito kukosa vipimo muhimu wanahudhuria kliniki mbalimbali, ni tatizo kubwa katika vituo vingi vya afya kunakuwa na idadi kubwa wa wajawazito ukilinganisha na vipimo hivyo.
Massay alisema kuwa sio tu vipimo kukosekana, bali hata kadi za kliniki kwa wajawazito na watoto wadogo nalo ni tatizo sugu kwa sasa, mpaka kunakipindi ofisi ya mganga mkuu inachapisha kadi 10,000 kila mwaka ili kuweza kuziba pengo la upungufu wa kadi za kliniki kwa wajawazito na watoto wadogo.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Dk. Gunini Kamba alisema kuwa, kuna tatizo la upatikani wa vipimo hivyo vya (VDRL test)
na (HB test) katika hospitali ya sinza kwa sababu ya wateja kuwa wengi tofauti na dawa na vifaa tiba.
Dk. Kamba alisema kuwa, kwa sasa wanatumia njia ya kupima (HB test) kwa kutumia Hamemoque machine ambayo inagharama kubwa sana kununua ni shilingi 900,000 na vipimo vyake katika kopo moja vinakuwa 50 hadi 100. kwa kununua duka la kawaida kwa kikopo ni shilingi 89,000.
Kwa kutumia utaratibu wa manunuzi kwa kikopo kimoja cha (HB test) kinauzwa kati ya shilingi135,000 hadi 15,0000 kwa kikopo, lakini kupitia bohari ya madawa wananunua kwa kikopo kimoja ni shilingi 75,500.
Dk. Kamba alisema kuwa, ufumbuzi wa tatizo hilo unafanyiwa kazi itakapopatikana mashine aina ya (Tallquist Method) kutoka nchini German ambayo inauzwa kwa gharama nafuu sana na kikopo kimoja kilichokuwa na vipimo vya (HB test) kinauzwa kuanzi shilingi 45,000 hadi shilingi 50,000. Ila kwa sasa vipimo hivi havipatikani bohari ya madawa (MSD)
Aidha kwa upande wa vipimo vya (VDRL) wapo katika mchakato wa kufanya manunuzi, ukikamilika basi watakuwa na vipimo hivyo vya kutosha na wajawazito watakuwa na fulsa ya kupima kila anapopangiwa kuhudhulia kliniki.
Aidha alisema kuwa idadi ya wajawazito imeongezeka kuanzia mwaka jana, kutoka 4,23 wajawazito waliopima mwaka 2011, hadi kufikia 6,908 mwa ka 2012 kuanzia mwezi January hadi Novembar, waliojifungua kwa kufanyiwa upasuaji walikuwa 7,22.
Kwa mwaka huu matarajio yao kuwazalisha akina wajawazito 100,000 katika hospitali ya Sinza pekee, wajawazito hao ambao wanatarajiwa kuhudhuria kliniki mara tatu kwa kila mjamzito, kwa hivyo basi tunatakiwa kuwa na boxi 600 za vipimo vya damu, sawa na shilingi milini 53,4000 kwa mwaka.
Dk. Kamba alisema kuwa, kwa sasa wilaya ya Kinondoni kwa upande wa zahanati, vituo vya afya na hospitali, wanapewa bajeti ya Serikali Kuu katika wilaya ya Kinondoni ni shilingi 766,438,000 na wafadhili wamechangia shilingi 2,480,746,600.
Aidha Dk. Kamba alifafanua kuwa, Fedha hii hugawanywa katika zahanati, vituo vya afya, hospitali na ofisi ya mganga mkuu wa wilaya kwa kuzingatia asilimia iliyowekwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Dk. Kamba alifafanua kuhusu mgawanyo wa fedha hizo alisema, Ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya hupata asilimia 15 hadi 20, hospitali ya wilaya asilimia 25 hadi 30, vituo vya afya asilimia 15 hadi 20, zahanati asilimia 20 hadi 25 na jamii ni asilimia 2 hadi 5.
Kiasi hicho cha pesa hakikidhi mahitaji halisi ya wagonjwa wanaostahili kupatiwa huduma kwa siku na mwezi katika vituo vya afya mbalimbali katika wilaya ya Kinondoni.
Akionyesha kuwa kunahitaji mtazamo mpya, Dk. Kamba aliiomba Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kubadilisha utoaji wa pesa za bajeti katika wilaya mbalimbali na wanatakiwa kupanga bajeti kulingana na idadi ya watu wanaohitaji kupatiwa huduma za afya.
Kwa kutumia kigezo hicho suala la upungufu wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya mbalimbali hapa nchini, vitakuwa havipati changamoto ya kukosa dawa za muhimu hasa kwa watoto wa chini ya miaka mitano na wajawazito.
Kwa mfano takwimu zinaonyesha kuwa mwaka jana Zaidi ya wajawazito 40,000 walikadiliwa kujifungua katika wilaya ya Kinondoni kwa mwaka jana, lakini kati ya hao wajawazito 31,000 walijifungua katika vituo vya afya mbalimbali katika wilaya hiyo.
Kwa upande wa wilaya ya Ilala na Temeke nako hali itakuwa inafanana na ya wilaya ya Kinondoni, wajawazito ni wengi lakini kutakuwa na upungufu wa madawa na vifaa tiba.
Tatizo hili limelikuta katika wilaya ya Nachingwea mkoa wa Lindi, idadi ni kubwa ya wajawazito lakini wanakosa huduma bora ya kujifungua salama kwa sababu ya ufinyu wa bajeti.
Pia katika wilaya ya Songea mkoa wa Ruvuma hali sio nzuri katika upatikanaji wa huduma za kliniki, katika zahanati Ifinga kwenye kijiji cha Ifinga wajawazito wanachingia huduma mbalimbali za kliniki, kupima ujauzito unalipia shilingi 2,000, kupima wingi wa damu unalipa shilingi 15,00, kama damu yako pungufu kupewa dawa za kuongeza damu unalipa shilingi 1,000.
Sera ya Afya ya mwaka 2007 inasema wajawazito wanatakiwa kutibiwa bure, lakini utimizaji wa sera hii una changamoto nyingi zikiwamo ukosefu wa vitendea kazi mbalimbali na dawa. Changamoto zote hizi zinafanya utekelezaji wa Sera hii kuwa mgumu sana.
Hali kadhalika katika Wilaya ya Bunda, Butiama na Musoma Mjini katika mkoa wa Mara, wajawazito wanapokwenda kliniki wanachangia huduma za upimaji kama kupima wingi wa damu wanalipia shilingi 1,000, kadi la kliniki wananunua shilingi 1,000.
Hivi ni lini hasa wajawazito hapa nchini watapata huduma bora za kliniki, tena bila ya kuchangia chochote kile! nani anastahili kuwajibika katika hili ni watoa huduma katika vituo vya afya mbalimbali hapa nchini! au uwongozi wa wilaya unaosimamia utoaji wa huduma za afya kwa jamii!
Kila mtu anatakiwa kujua wajibu wake sehemu ya kazi ili kuhakikisha huduma ya upimaji kwa mjamzito inakuwa bora na ya uhakika, maana akipatiwa huduma bora itasaidia kujua mjamzito kama ana tatizo kama la kupungukiwa damu, mtoto amekaa vibaya, mtoto mkubwa, mama ana maambukizi ya magonjwa ya kuambukiza.
Hii itasaidia kumsaidia mjamzito wakati wa kujifungua mtoto asiye kuwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi kama ilivyokuwa katika kijiji cha Matekwe kata ya Kilimarondo wilaya ya Nachingwea, wajawazito wamewaambukiza watoto zao kwa kukosa dawa za ARV, pia itapunguza vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua na baada.
0 comments:
Post a Comment