Wednesday, February 6, 2013

USAFIRI WA MTUMBWI TATIZO KWA WAJAWAZITO RUFIJI

“Nilijifungua kando ya mto Rufiji kutokana  na mtumbwi kuwa ng’ambo ya pili” anaeleza Sina  Mlimile 22 mkazi wa kijiji cha Nyaminywiri kata ya kipugira wilayani Rufiji.


Sina Mlimile anaishi ng’ambo ya pili ya kijiji cha Nyaminwiri ambacho kimegawanyika sehemu mbili kutokana na kuwepo kwa mto Rufiji, eneo analoishi Sina hakuna huduma ya kituo cha afya hali inayowalazimu wakazi wa eneo hilo kuvuka ng’ambo ya pili ya mto ili kupata huduma za afya.

Kutokana na hali hiyo akina mama wajawazito wamekuwa wakilazimika kutumia mitumbwi kuvuka toka upande mmoja kwenda upande wa pili na wakati mwingine kukumbana na hali hiyo ya kuchelewa kufika kituo cha afya cha Nyaminywiri   umbali wa kilometa tatu toka  upande huo wa kijiji mpaka ng’ambo ya pili.

Sina mwenye mtoto wa Kiume Mwalimu Rajabu Mkuka ambaye ana miaka 4 sasa anasema alikumbana na adha hiyo ya kuchelewa kituo cha afya kwenda kujifungua   kutokana na mtumbwi kuwa ng’ambo ya pili.
sina

PICHA: Sina Mlimile akiwa na mwanae aitwaye Mwalimu Rajabu
 Anasema alilazimika yeye na ndugu zake kusubiri mtumbwi huo kwa muda wa saa mbili huku akiendelea kuugulia uchungu lakini hakuwa na namna nyingine isipokuwa kusubiri majaliwa ya mtu yeyote kutoka ng’ambo nyingine na kuleta mtumbwi.

Anasema aliongozana na  baba yake Abdalah Said Mlimile, Mume wake Rajabu Mwalimu, mama yake Tano Abdalah, shangazi yake Fatuma Rashid, Mkunga na bibi yake, anasema pamoja kuwepo kwa wanaume katika safari ile hakuna aliyepata ujasiri wa kuogelea kufuata mtumbwi ng’ambo ya pili kutokana na kuwepo kwa mamba wengi na viboko ndani ya mto Rufiji.

Anasema baada ya kusubiri kwa muda wa saa moja mara wakaona mtu akitokezea ng’ambo ya pili wote wakapaza sauti kumuomba afanye haraka kutokana na hali ya Sina kuendelea kuwa mbaya.

Baada ya mtumbwi kufika sehemu waliyokuwepo Sina alikuwa hana uwezo wa kutembea hali iliyowalazimu waliomsindikiza kumbeba na kumuingiza kwenye mtumbwi ili kuwahi kituo cha afya cha Nyaminywiri.

Haikuwa  kama walivyopanga kwani baada  ya mtumbwi kufika ngambo ya pili anasema tayari mtoto alikawa anachungulia hali iliyowalazimu waliomsindikiza kumbeba na kumsogeza karibu na kichaka, na kazi ya kumzalisha ikifanywa na mkunga wa jadi Mwajuma Likwayu pamoja na mama yake mzazi  yake Sina , Tano Abdalah.

“Bahati nzuri tulitembea na kiwembe na tochi ambayo ilitumika kumulika zoezi zima kwani tayari ilikuwa ni usiku” anaeleza.

Anasema alijifungua salama na wakarudi nyumbani lakini anakiri kwamba ni siku ambayo hawezi kuisahau katika maisha yake, kwani muda aliotumia kusubiri mtumbwi ulimpa wakati mgumu na maumivu ambayo hayaelezeki.

Kwa upande wa shangazi yake Sina Fatuma Mkugwa ambaye  alikuwa katika msafara wakumpeleka sina kituo cha afya anasema, hali hiyo ya kuchelewa kwenda kituo cha afya ilitokana na mambo mengi moja ikiwa ni mhusika kutokuwa na uhakika ni lini atajifungua.

Anasema  tayari alishaambiwa bado mwezi mmoja ,  kwa hiyo alikuwa kwenye makadirio hivyo akajisahau na kujikuta uchungu unampata akiwa shamba  lakini kuchelewa kupata mtumbwi kwa wakati pia ni tatizo lingine.

Anasema wanamshukuru Mungu kwani halikutokea tatizo japokuwa walikuwa na hofu kubwa baada ya kuona yuko tayari kujifungua  kabla ya kufika kituo cha afya.

Kwa upande wa mwendesha mtumbwi Omary Ulwe (57) anasema hali hiyo ilitokea kutokana na kutokuwepo kwa utaratibu maalum ambapo kila mtu alikuwa anajiendesha mwenyewe hali iliyokuwa ikiwapa akina mama wakati mgumu kwani wengi hawawezi kuendesha mtumbwi.

“Kwa sasa kuna madereva maalum kama mimi ambao tunafanya kazi hapa na kujipatia kipato kutokana na kazi hiii lakini pia kwa sasa mtumbwi unalala ng’ambo hii ambako ndiko wakazi wengi wanauhitaji” anaeleza

Ulwe anasema yeye na madereva wenzake wamekuwa tayari kuendesha mtumbwi hata usiku hasa inapotokea kuwepo kwa mama mjamzito ambaye anatakiwa kupelekwa kituo cha afya kwa ajili ya kujifungua.

Mganga mkuu wa kituo cha afya cha Nyaminywiri Dk Tarcis Bwakila anakiri kuwepo kwa akina mama ambao huchelewa kufika kituo cha afya kutokana na matatizo ya kupata usafiri wa mtumbwi kwa wakati na hivyo wengi kujikuta wakijifungulia njiani.

Bwakila ameeleza kuwa anatoa ushauri kwa akinamama wanaoishi nga’mbo ya pili kuhamia upande wa pili yaani sehemu ambayo kituo cha afya kinapatikana  pale wanapokuwa na ujauzito wa miezi nane,  ili kuepusha matatizo ya kushindwa kufika kwa wakati katika kituo cha afya na kujifungua katika mikono salama ya madaktari na manesi.

“Unajua watu wa ng’ambo ile wengi wana ndugu zao na marafiki zao huku   hivyo nawashuri wakae huku wanapokaribia kujifungua, lakini wengi hawafanyi hivyo na kujikuta wakikutana na matatizo ya kujifungulia njiani” anaeleza Bwakila.

Anasema  akinamama wengi hawachukulii kwa uzito suala la ujauzito kwani hata wanapokuwa katika hatua za mwisho, wanaendelea na kazi za shamba bila kujali hali iliyoko mbele yao ya kujifungua, na kujikuta hali hiyo inawakuta kama ajali wakati wanafahamu ni wakati gani wanatakiwa kujiandaa.

Kaimu mwenyekiti wa kijiji cha Nyaminywiri Yusuph Magenge anasema yamekuwepo matatizo mbalimbali yanayohusiana na kivuka kwa upande wa wakazi wanaoishi ng’ambo ya pili ya kijiji chake.
Anasema pamoja na akina mama wajawazito kupata matatizo wakati wa kwenda kituo cha afya,  anasema hata wanafunzi wamekuwa wakipata wakati mgumu wakati wa masika ambapo mto hujaa na kuhatarisha maisha yao.

Anasema mwaka 2010 kiboko alipindua mtumbwi uliokuwa umebeba wanafunzi wa shule ya msingi Nyaminywiri na kusababisha wanafunzi  tisa kufariki.
usafiri-mtumbwi
PICHA: Mwendesha mtumbwi aliyetambulika kama Omari Ulwe akiwavusha wanafunzi wa Darasa la Kwanza toka Shule ya Msingi Nyaminywiri
“Mkuu wa mkoa aliyekuwepo wakati wa msiba wa wanafunzi  Mwantumu Mahiza aliahidi kutuletea boti ili kuondoa adha wanayopata akina mama wajawazito na wanafunzi lakini bado hatujaletewa” anafafanua Magenga.

0 comments:

Post a Comment