Friday, February 8, 2013

RUNGWE WAFANIKIWA KUPUNGUZA VIFO VYA WAJAWAZITO

  
SERIKALI wilayani Rungwe mkoani Mbeya imesema kuwa imefanikiwa kupunguza vifo vya akina mama wajawazito vitokanavyo na uzazi ambapo kwa kipindi cha mwaka 2005 vifo vilikuwa 214 kati ya vizazi hai 100,000 na kufikia vifo 9 mwaka 2012 kati ya vizazi hai 100,000.

Taarifa hiyo imetolewa hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya ya hiyo Chrispin Meela, akiwasilishaji taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na Serikali kwa kipindi cha miaka saba ya serikali ya awamu ya nne.
Aliwaambia waandishi wa habari kuwa katika kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wa chini ya umri wa miaka mitano idadi ya akina mama wajawazito waliojifungulia hospitalini na vituo vya afya waliongezeka kutoka 4,432 hadi kufikia 7, 397.
‘’Kuongezeka kwa akina mama wanaojifungulia hospitalini na vituo vya afya inatokana na wazazi hao kupata huduma iliyobora na salama wakati wa kujifungua hivyo wananachi wenyewe wamekuwa wakihamasishana wao kwa wao kwenda kujifungulia sehemu iliyosalama zaidi tofauti na hapo awali’’ alisema Mkuu huyo wa wilaya.
Alitanabaisha kuwa katika kuhakikisha sekta ya afya inaimarishwa zaidi wilayani humo, hadi kufikia mwaka 2012 kumekuwepo hospitali 3 ambapo kati ya hizo hospitali moja ni ya Serikali na mbili ni za madhehebu ya dini, zahanati 54 na vituo vya afya vitano.
Mbali na mafanikio hayo alikiri kuwepo kwa changamoto kadhaa zinazoikabili sekta hiyo kama vile upungufu wa dawa na vifaa vya kutolea huduma kwa wagonjwa.

0 comments:

Post a Comment