Monday, February 18, 2013

SIKIKA YAMPONGEZA WAZIRI WA AFYA KWA KUWAJIBIKA

Sikika inapenda kumpongeza Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi kwa kuweka bayana na kukiri kwamba kuna uhaba mkubwa wa dawa muhimu za kutibu malaria, maarufu kama dawa mseto (Alu) katika vituo vingi vya huduma za afya vya umma nchini.

Akizungumza na vyombo vya habari hivi karibuni, waziri Mwinyi alikiri kuwepo kwa uhaba wa dawa hizo za kutibu malaria kama zilivyoripotiwa na mtandao wa Wizara hiyo kupitia mfumo wa kielektroniki ujulikanao kama ‘SMS for Life.’ Dk. Mwinyi alinukuliwa  akiwataka watanzania kutokuwa na wasiwasi kwani suala hilo lilikuwa linashughulikiwa na kwamba usambazaji wa Alu ulishaanza.


Tunampongeza kwa dhati waziri Mwinyi kwa  kukiri uwepo wa tatizo hili na kuchukua hatua. Sikika tunaamini kwamba hatua hiyo  ni muhimu katika kukuza uwajibikaji na uwazi. Wiki mbili zilizopita, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Regina Kikuli na Msemaji wa wizara hiyo, Nsachris Mwamwaja walikanusha taarifa iliyotolewa  na Sikika kwamba kuna uhaba wa Alu   kwa takribani asilimia 26, katika vituo vya huduma za afya nchini.  Taarifa hizo zilipakana kutoka kwenye  mfumo huo huo wa Wizara (SMS for life).


Taarifa ya Kikuli pia ilikaririwa na vyombo vya habari ikiueleza  umma kwamba kuna dawa nyingine za malaria ambazo haziripotiwi kupitia SMS for life, jambo ambalo si kweli.


Sikika inaiomba Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuharakisha usambazaji wa dawa hizi na ilichukulie suala hili kama dharura kwani kuna baadhi ya vituo vya huduma vina uhaba mkubwa wa Alu kwa takribani siku 300 sasa. Pia tunaishauri Wizara kubadili mfumo wa uagizaji wa dawa kwa zahanati na vituo vya afya  ambao huvilazimu vituo kuagiza dawa kila baada ya miezi mitatu (robo mwaka), wakati usambazaji wake unachukua muda wa miezi miwili hadi mitatu. Ni vyema vituo viwe vinaagiza dawa kila mwezi ili kupunguza tatizo la uhaba wa dawa muhimu unaojitokeza mara kwa mara.


Ikumbukwe kwamba msimu wa mvua unakaribia kuanza katika maeneo mengi hapa nchini na hivyo kuwepo kwa uwezekano wa kuongezeka kwa maambukizi ya malaria. Ugonjwa wa malaria unaongoza kwa kusababisha vifo vingi nchini.  Hivyo basi,  uwepo wa dawa za ALu za kutosha katika vituo vya huduma utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo hivyo.


Ni jambo la kushangaza kuona kuwa ALu zinakosekana katika vituo vingi hapa nchili wakati kuna fedha za kutosha kutoka kwa wafadhili kwa ajili ya ununuzi wa dawa hizo. Kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita, Tanzania ilipokea kiasi cha dola za Marekani 331,112,207 kutoka Global Fund pekee, ambapo kiasi cha dola za Marekani 294,975,327 tayari zimeshatumika. Ukiachilia mbali Global fund, malaria pia imekuwa ikifadhiliwa na Mfuko wa Ufadhili wa Rais wa Marekani (PMI – USAID), Benki ya Dunia (World Bank) pamoja na wahisani wengine.


Yapo makampuni makubwa manne ambayo yameteuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa ajili ya kuleta dawa hizo hapa nchi. Makampuni haya yanatambulika kimataifa kwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha na kusambaza dawa hizo kwa vipindi maalum. Tatizo tunaloliona hapa ni Wizara yetu kushindwa kufanya makadirio na kuagiza dawa hizo kwa wakati.


Ni wakati sasa kwa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria (NMCP), Bohari ya Dawa ya Taifa (MSD), Kitengo cha Dawa cha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii (PSS) na Waganga Wakuu wa Wilaya (DMOs) kuchukua hatua madhubuti za kutatua tatizo la uhaba wa Alu. Suluhu ya tatizo hili ni kwa wote wanaohusika kuwajibika kwa dhati ili kuokoa maisha ya watanzania.


Vilevile, tunaishauri serikali kupanua wigo wa matumizi ya mfumo wa ‘SMS for Life’ ili kuongeza dawa zingine muhimu na vifaa tiba. Mfumo huu unasaidia sana kutoa taarifa zenye ukweli na uhalisia na kuhusu uhaba wa dawa ili wizara  ijipange kukabiliana na tatizo hilo kwa kusambaza dawa zinazohitajika kwa wakati. Mfumo huu pia utasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha uwazi na uwajibikaji katika usambazaji wa dawa,  hatimaye kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini.


Kwa namna ya pekee, Sikika inavipongeza vyombo vya habari kwa juhudi zao za dhati katika kuuhabarisha umma juu ya tatizo la uhaba wa Alu. Vyombo hivyo vilitanguliza zaidi maslahi ya umma bila kujali matamko ya wazi ya baadhi ya viongozi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ya kuupindisha ukweli. Kwa mara nyingine tena, vyombo vya habari vimeweza kuonesha uzalendo kwa kuweka maslahi ya taifa mbele.

0 comments:

Post a Comment