Tuesday, February 12, 2013

SONGEA WAJAWAZITO WALALAMIKIA KUTOZWA FEDHA KWENYE ZAHANATI NA VITUO VYA AFYA

  
Wakati Sera ya afya na ustawi wa jamii ya mwaka 2007 inasema, kila mjamzito na mtoto wa chini ya umri wa miaka mitano anatakiwa kutibiwa bure katika hospitali, kituo cha afya na zahanati.

Lakini kwa Kijiji cha Ifinga Kata ya Matumbi Wilaya ya Songea Mkoa wa Ruvuma, wanatozwa pesa ya kujifungua, kupima ujauzito, mtoto akiumwa na kuuziwa dawa za malaria na kadi za kliniki.
"Tunauziwa kadi ya kliniki Tshs. 1000, mtoto akiuwa kumpima ili kujua kama anaumwa malaria unatakiwa kulipia Tshs. 500, mtoto akiandikiwa dawa ya malaria na dripu ya maji unatakiwa kulipia Tshs. 8000, mjamzito kujifungua Tshs. 15,000,"alisema Ifigania Ngura
kadi-ya-kliniki
Ifigania alisema kuwa, hata ukianza kwenda kliniki kwa mara ya kwanza unatakiwa kupima kujua unaujauzito wa miezi mingapi nayo pia unalipia Tshs. 2000, pia dawa za mseto tunauziwa Tshs. 15,00 kwa wajawazito na watoto Tshs. 1000.
Kutokana na ugumu wa maisha katika kijiji hicho, wajawazito wengi wanakwepa kwenda katika zahanati hiyo kuhofia ghalama kubwa na kukimbilia kwa mkunga wa jadi kujifungua bila ya kupimwa kliniki wakiwa na ujauzito.
mama-mjamzito
PICHA: Ifigania Ngura (mjamzito)
Hali hiyo inasababisha ongezeko la vifo vya wajawazito na watoto wa changa, kwa sababu mkunga wa jadi hana utaalamu wa kujua kama mtoto amekaa vema tumboni, njia kubwa, mtoto anapumua vema, mtoto anauzito gani? hili ni tatizo serikali inatakiwa kulifanyia kazi.
"Bora uwende kwa Bi. Amina Mwichande ambaye ni mkunga wa jadi uchungu ukianza kuuma kuliko kwenda katika zahanati ya hapa kijijini, maana ghalama zake ni kubwa na uwezo sina wa kulipa Tshs.15,000 wakati kwa mkunga wa jadi unatoa Tshs. 2000 hadi 3000,"alisema Anna Komba
Tobias Millinga Mganga katika zahanati ya Ifinga alisema kuwa, huduma zote za afya zinalipiwa kwa wajawazito, watoto chini ya miaka mitano na wazee, kwa sababu zahanti inaongozwa na Kanisa Katoliki.
"Napewa madawa na Mratibu wa Jimbo Mama Lugongo, ananiandikia na ghalama za kila dawa alivyonunua na bei ya kuuza kila dawa, napenda nitoe huduma bure lakini kwa sababu bosi wangu mama Lugongo ananiandikia mpaka pesa ninayotakiwa kurudisha nikienda kuchukua madawa mengine, kiufupi zahanati hii iko kibiashara zaidi japo kuwa inatoa huduma za kijamii," alisema Mganga Millinga.
Zaituni Mango ni Afisa Mtendaji katika Kijiji cha Ifinga alisema kuwa, ni kweli wanatozwa pesa wajawazito na watoto wa chini ya umri wa miaka 5 wakienda katika zahanati hiyo.
"Tumeshapeleka malalamiko kwa Mganga Mkuu wa Wilaya juu ya wajawazito na watoto kutozwa pesa, wakati huduma hiyo inatakiwa kutolewa bure, kwa sababu zahanati iko chini ya Kanisa Katoliki ndio wanatoza pesa,lakini Mganga mkuu aliniambia atafuatilia tatizo hilo na kulitatua," alisema Afisa Mtendaji Zaituni
Kwa upande wake Father Haule wa Kanisa Katoliki katika Kijiji cha Ifinga alisema kuwa, wajawazito na watoto wote Ifinga wanatibiwa bure kama kuna nesi na mganga anatoza pesa basi atachukuliwa huduma za kisheria.
Mkunga wa jadi Amina Mwichande alisema kuwa, anapokea akinamama wengi wanaokwenda kwake kujifungua na wengine kumuita kwenda nyumbani kwake mjamzito ili kumsaidia kujifungua.
"Kazi ya ukunga nimeanza toka mwaka 1989 kipindi ambacho mume wangu alikuwa mganga katika zahanati hii, alinifundisha jinsi ya kumzalisha mjamzito na kabla ya kufariki mwaka 1996 alinihusia kwamba nisiache kazi ya kuzalisha wanaifinga nami sijaacha naendelea mpaka leo hata idadi sijui ya watu niliowazalisha mpaka sasa sina sehemu ya kutunza kumbukumbu ila mie ndio tegemeo kubwa hapa kijijini," alisema Amina.
Aidha alisema kuwa amepewa mafunzo ya siku moja tuu na uwongozi wa hospitali ya wilaya, mwaka 2002 mpaka sasa hajapewa mafunzo mengine bado anatumia njia zake zile zile za kizamani, pia alisema nikimzalisha mjamzito ananilipa Tshs. 2000 hadi Tshs. 3000, napokea kwa moyo mmoja kwa sababu nawasaidia kwa kukimbia ghalama kubwa katika zahanati ya Ifinga.
mkunga
PICHA: Amina Mwichande, mkunga wa jadi
Mkunga huyu hana vifaa na madawa ya kutosha ya kumuweza mjamzito kujifungu pale atakapopatwa na tatizo la kutokwa na damu nyingi, mtoto kushindwa kutokwa hana kifaa cha mvuta vema ili atoke, kondo la nyuma la uzazi kugoma kutoka hana dawa ya kumchoma sinda ili kusaidia kutoka kwa kondo la uzazi.
Pamoja sindano ya kumchoma mjamzito baada ya kujifungua ili mfuko wa uzazi usinyae na mama asiendelee kutokwa na damu nyingi pamoja na mashine ya kutoa uchafu kwa mtoto kama hapumui vema baada ya kuzaliwa.
Hili ni tatizo kubwa sana katika sekta ya afya nchini, kama serikali haitaweka mipango madhubuti ya kuhakikisha kwamba mjamzito anajifungua katika mikono salama ya wataalam wenye ujunzi na vifaa tiba vya kumuwezesha mjamzito kujifungua vema idadi ya vifo itang'ang'ania hapo hapo haita shuka.
Utafiti wa kitaifa katika masuala ya afya uliofanywa mwaka 2010 (Tanzania Demographic and Health Survey analysis) unaonesha kuwa, idadi ya vifo vya wajawazito na watoto itaendela kuwa kubwa siku hadi hadi siku kwa sasa wajawazito 85,00 wanapoteza maisha kila mwaka na kila siku ni wajawazito 23 kati ya hao asilimia 46 wanapoteza maisha kwa tatizo la kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.
Kwa upande wa watoto wa chini ya umri wa miaka 5, watoto 5,000 wanapoteza maisha kila mwaka na watoto 137 wanapoteza maisha kila siku, wingi wa vifo hivi kwa watoto sawa na ndege ya abiri ya air Tanzania inayotoka dar kwenda mwanza kila siku ipate ajali na abiria wake wote wapoteze maisha.
Kijiji cha Ifinga kina wakazi 3,220  kati ya hao wajawazito ni 100 kwa mwaka jana, wajawazito  waliojifungua ni 70 kati ya 50 wamejifungua kwa mkunga wa jadi na 30 bado hawajajifungua na wenye umri wa kushika mimba ni 150.

0 comments:

Post a Comment