Thursday, February 14, 2013

BAJAJ ZA KIKWETE NA CHANGAMOTO YA USAFIRI KWA WAJAWAZITO VIJIJINI

  
WAKATI wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010, Rais Jakaya Kikwete aliahidi kusambaza pikipiki za matairi matatu (bajaj) zipatazo 400,000 katika hospitali, zahanati na vituo vya afya nchini kwa nia ya kusaidia wagonjwa hususani wanawake wajawazito kuwahishwa hospitali wakati wa kujifungua.

Ahadi yake ilizua maswali kutokana na ukweli kuwa haikueleweka ni jinsi gani bajaj au pikipiki hizo zenye matairi matatu zitakuwa na uwezo wa kubeba wagonjwa hususani wajamzito wenye uchungu.
nachingwea
Wilayani Nachingwea Mkoani Lindi, Bajaji hizo hazitumiki kubeba wajawazito kama ilivyokusudiwa kutokana na ubovu wa barabara
Akizungumza na Mtendaji Mkuu wa shirika la kimataifa lisilokuwa la kiserikali la Pathfinder International, Dk Purnima Mane, Ikulu, Dar es Salaam Julai 19, 2012, Rais Kikwete alisema ni jambo lisilokubalika kwa mwanamke kupoteza maisha wakati akijifungua kwa sababu uja uzito siyo ugonjwa.
Miongoni mwa maamuzi ambayo Serikali imechukua kukabiliana na tatizo hilo ni pamoja uamuzi wa kupunguza umbali wa kufikia huduma za afya kwa kujenga zahanati kila kijiji na kituo cha afya kila kata na hivyo kuhakikisha kuwa huduma hizo zinapatikana katika umbali usiozidi kilomita tano.
Serikali pia imeamua kuwa kila kituo cha kutolea huduma lazima kiwe na huduma za wazazi na wajawazito na kuzidisha harakati za kukabiliana na ugonjwa wa ukimwi ambao ni moja ya chimbuko kubwa la vifo vya akinamama wajawazito.
Maria Kasege (20) ni mmoja wa wajawazito wanaoshindwa kufika katika vituo vya kutolea huduma kwa wakati kutokana na tatizo la usafiri wa uhakika na miundombinu mibovu ya barabara.
Anaishi kilomita 18 kutoka hospitali teule ya Rufaa ya Ilembula; barabara ya kuelekea katika kijiji chake cha Lugoda wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe, haipitiki kwa kuwa ina mashimo.
kasege
Maria Kasege akiwa katika wodi ya wazazi baada ya kujifungua kwa upasuaji
Alitumia saa sita kufika hospitalini hapo zikiwa zimesalia siku saba kabla hajajifungua (alijifungua Oktoba 4, mwaka jana). Uchovu wa safari ulimfanya apoteze nguvu nyingi mwilini na hivyo kufanyiwa upasuaji badala ya kuzaa kwa njia ya kawaida.
Katika simulizi yake, Michael Mgaya ambaye pia ni mkazi wa kijiji hicho anasema, Septemba 13, 2011 alifiwa na mkewe Santina Mwinami.
Anasema mkewe huyo alipatwa na uchungu mwezi mmoja kabla ya tarehe aliyotarajia kujifungua.
“Nikiwa katika shughuli zangu za shamba, sikujua kwamba nitakaporudi nitamkuta mke wangu amefariki, alitokwa na damu nyingi wakati akijifungua bila msaada wowote,” anasema.
Kwasababu ya tatizo la usafiri, Mgaya anasema ilikuwa ngumu kwa mkewe kuhudhuria kliniki ili achunguzwe afya yake.
“Hesabu yangu ilikuwa nimpeleke hospitalini Ilembula wiki moja kabla ya tarehe aliyodhaniwa angejifungua,” anasema na kuongeza kwamba tangu apate mimba hiyo, mkewe huyo alihudhuria mara moja tu katika kliniki ya hospitali ya Ilembula.

Wakati Kasege na Mgaya wakihuzunika, tayari halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe na Njombe kwa pamoja zimepata pikipiki tatu za kubeba wagonjwa maarufu kama Bajaj za Kikwete.
Oktoba mwaka jana, mbili kati ya bajaj hizo zilipelekwa katika vijiji vya Makoga (halmashauri ya wilaya ya Njombe) na Kichiwa (halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe); hata hivyo hadi Januari mwaka huu bajaj moja ilikuwa katika yadi ya halmshauri ya wilaya ya Njombe ikiwa haijaunganishwa na kitanda chake.
bajaj
Bajaj hii ilitelekezwa kwa muda mrefu katika yadi ya halmashauri ya wilaya ya Njombe
Pamoja na kupelekwa katika vijiji hivyo, Afisa Mipango wa Halmashauri hiyo, Shadrack Muhagama anasema pikipiki hizo aina ya eRangers, zina tatizo la kiufundi.

“Huwezi kukata kona upande wa kushoto kwasababu kitanda chake kinafika hadi tairi la mbele, na ni matatizo zaidi kuzitumia kwenye barabara za vumbi, zenye kona, miinuko, na mawe kwasababu zinapoteza nguvu,” anasema.

Hata hivyo Kaimu Mganga Mkuu wa halmashauri hiyo, Dk Conrad Ugonile anasema bajaj hizo zina uwezo wa kupenya na kufika alipo mgonjwa na kisha kumbeba na kumpeleka hospitali yoyote kulingana na maelekezo bila kucheleweshwa na foleni za barabarani hali inayoweza kuondoa tatizo la usafiri kwa wagonjwa mahututi wanaohitaji usafiri wa haraka.   
                                             
Anasema zikipatikana kwa wingi na zilizotengenezwa kwa ustadi, bajaj hizo zitasaidia kuleta ukombozi wa wananchi hususani wajawazito wenye kuhitaji matibabu ya haraka katika hospitali za rufaa au zile za mikoa.

Anasema matatizo katika sekta ya afya ni mengi, hata hivyo tatizo la wajawazito kushindwa kufika katika vituo vya kutolea huduma kutokana na ukosefu wa usafiri ni tatizo kubwa linalohitaji kupatiwa ufumbuzi utakaoleta suluhu.

Dk Ugonile, anasema asilimia 23 ya wanawake wajawazito kutoka katika vijiji visivyo na huduma muafaka wanalazimika kuzaa wakiwa majumbani, wengine bila msaada wowote.

Halmashauri ya wilaya ya Njombe na Wanging’ombe kwa pamoja zina vituo 65 vya 
kutolea huduma. Kati yake, hospitali iko moja (hospitali teule ya rufaa ya Ilembula), vituo vya afya vinne (kati yake vitatu vya serikali), zahanati ziko 60 (kati yake 53 za serikali, sita za mashirika ya dini na moja ya kampuni ya chai).

Kuna kata 28 zenye jumla ya vijiji 145 ambavyo kati yake 50 havina zahanati.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Valance Kabelege anasema halmashauri yake haina mpango wa kununua bajaj zaidi ya hizo kwasababu ya kuwa na hali ngumu ya fedha.

“Tuna hali ngumu hasa baada ya mji wa Makambako kupata hadhi ya halmashauri, mapato makubwa ya halmashauri yetu yalikuwa yanatoka katika mji huo wa kibiashara.” anasema.

Mwenyekiti wa Muungano wa Mashirika yasio ya Kiserikali Wilaya ya Njombe (Njodingo), Alatanga Nyagawa anasema bajaj tatu haziwezi kukidhi mahitaji ya wajawazito wanaohitaji msaada wa kufikishwa katika vituo vya kutolea huduma.

“Vijiji visivyo na vituo vya huduma, njia ya kufika sehemu zenye vituo ni kwa kutumia miguu, baiskeli, na pikipiki, aina hii ya usafiri ni kwa huduma za haraka na zisizo za haraka, aina ya usafiri huu unaweza kumletea madhara ya kiafya mjamzito au mgonjwa,” anasema.

Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Estalina Kilasi anasema uboreshaji wa huduma za usafiri ni lazima ziendane na jitihada zingine zinazofanywa katika kuboresha afya ya uzazi.
Anazitaka halmashauri hizo kupunguza matumizi yasio ya lazima kama matumizi ya magari mengi wakati wa ziara za viongozi, posho za vikao na safari zisizo na tija ili fedha zake zisaidie kukabiliana na tatizo la magari ya kubeba wagonjwa.

Vyombo vya usafiri kama mabasi, magari ya wagonjwa, pikipiki na vinginevyo ni muhimu katika kufikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia (Millenium Development Goals) yanayoelekeza kupunguza kwa asilimia 75, vifo vya wajawazito na watoto ifikapo 2015.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), usafiri ni nyenzo muhimu sana katika kuboresha na kuzifikia huduma bora za afya; unawawezesha watu kuzifikia huduma, watoa huduma kuifikia jamii hususani ya maeneo ya mbali ya vijijini na usambazaji wa vifaatiba na dawa.

0 comments:

Post a Comment