Friday, February 22, 2013

MIUNDOMBINU,USAFIRI BADO NI KITENDAWILI KWA WAJAWAZITO MARA?

Ni saa 8:30 mchana Nyangeta Makori ambaye ni mjamzito anatoka kijiji cha Nyambono wilaya ya Musoma vijijini,usafiri unaofaa kwa mjamzito haupo hali iliyomlazimu kuchukua pikipiki na kupita katika barabara mbovu kwa saa nne, huku akisikilizia uchungu kutoka Msoma vijijini mpaka Kituo cha afya cha Manyamanyama wilaya ya Bunda mkoa wa Mara.

Alifika saa 11:30 jioni alipokelewa katika kituo cha afya cha Manyamanyama, bila ya kufahamu kama anamapacha katika tumbo lake,  kwa bahati nzuri baada ya muda saa moja alijifungua watoto wakiume wazuri, Doto akiwa na kilo 3.1 na Kulwa naye ana kilo 3.5 ndani ya mfuko mmoja wa uzazi.

Nyangeta huu ni uzazi wake wa tano ana watoto sita wote wakiume, watoto wa nne amejifungulia nyumbani akisaidiwa na wifi yake kwa kumshika sehemu ya mgongo wakati wa kujifungua na yeye kusukuma na kutoa mtoto, kitu kinachosababisha Nyangeta kuzaa nyumbani watoto wanne ni kijiji anachokaa hakuna zahanati na hospitali iko mbali ni mwendo wa saa 6 kwa pikipiki.

Wifi yake Nyangeta ni 'SHUJAA' amemuokoa Nyangeta asipoteze maisha kwa kumshawishi kwenda katika kituo cha afya kujifungua pamoja na kumsindikiza kutoka musoma vijijini mpaka Bunda, lakini pia ndiye mwanamke aliyemsaidia kujifungua nyumbani watoto wanne.

Ni wajawazito Tanzania wanaokumbana na shida wakati wa kutafuta huduma za kujifungua ikiwa pamoja na umbali, usafiri usio wa uhakika na barabara mbovu, kwa mujibu wa utafiti wa masuala ya afya ya uzazi ya Kitaifa wa serikali mwaka 2010(TDHS) unaeleza kuwa kila siku wajawazito 23 wanapoteza maisha kwa matatizo mbalimbali ya uzazi wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.

0 comments:

Post a Comment