Lusiana Danda (26) alipokuwa na mimba ya miezi nane (Oktoba 2012), alikuwa anatokwa na damu ya mwezi. Hali hii ambayo ni hatarishi kwa mjamzito na mimba yake ilianza wakati ana mimba ya miezi minne, baada ya yeye kuugua malaria.
Lusiana, ambaye ni mkulima na mkazi wa kijiji cha Ifinga, Songea, alipata matibabu katika zahanati ya Ifinga. Alivyokutwa na malaria, alipewa dozi ya dawa ya mseto ambayo hakumaliza.
“Niliamua kuacha kumeza dawa baada ya kusikia naendelea vema. Pia, nilipokuwa nameza dawa hizo nilikuwa nasikia maumivu chini ya kitovu; nikahofia mimba yangu isije kutoka,” alisema Lusiana.
Lusiana hajaolewa na hana mahusiano na mwanaume aliyempa mimba aliyokuwa nayo wakati huu. Kwa kuwa tayari ana watoto wawili na pasipokuwa na mtu mwingine wa kumtegemea, Lusiana aliendelea na kazi za kulima kama kibarua bila ya kupumzika, japokuwa alikuwa mjamzito na japokuwa alikuwa anaumwa.
Siku moja, Lusiana akiwa shambani na baada ya kulima kwa saa mbili, ghafla aliaanza kusikia maumivu makali chini ya kitovu. Maumivu hayo yalikuwa yakizidi kadiri muda ulivyokwenda na alikuwa akijisikia hali ya kutaka kujisaidia haja ndogo. Alipoenda msalani kujisaidia, ndipo akashtukia kuwa haukuwa mkojo bali ilikuwa ni damu.
Damu hii iliendelea kutoka kidogokidogo kwa siku tatu bila kukatika, ndipo Lusiana aliamua kwenda zahanati ya Ifinga kupima kama ujauzito wake bado ulikuwa salama.
“Nilipofika zahanati niliambiwa nitoe Tsh. 2,000 ili nipimwe kujua kama mimba bado ipo. Nilikuwa sina pesa kwa hiyo nilirudi nyumbani nikiwa sina raha,” alisema Lusiana.
Japokuwa damu ilikoma kutoka siku hiyo hiyo ya tatu, baada ya wiki mbili, Lusiana alifanikiwa kupata Sh10, 000 na kurudi tena kwenye zahanati kufanya kipimo cha ujauzito. Kipimo kilionesha kwamba bado alikuwa mjamzito lakini, mwezi uliofuata damu iliendelea kutoka tena na Lusiana aliporudi kwenye zahanati ya Ifinga kwaajili ya kujua kwa nini, hakufanikiwa.
“Niliambiwa hakuna vifaa vya kuchunguza kujua kama damu inayotoka inasababishwa na nini; na mhudumu wa afya aliniambia kuwa hajasomea kujua damu inayotoka kwa mjamzito inasababishwa na nini,” alisema Lusiana.
Kwa mujibu wa Dk. Ahmed Makuani, mtaalam wa magonjwa ya wanawake na uzazi salama kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kutokwa na damu kwa mjamzito ni kiashirio cha hatari sana. Mjamzito akiona damu inatoka anatakiwa kuwahi haraka hospitali.
Dk. Makuani alisema wanawake walio na umri wa zaidi ya miaka 35 wakishika mimba wako katika hatari ya kupoteza damu kwa sababu ya kondo la nyuma kuning’inia katika shingo ya kizazi upande wa ndani. Tatizo hili linajulikana kama placenta previa. Kitendo cha kondo la nyuma kuvumba kinaweza kusababisha kuachia sehemu iliyojishika na kutoa damu sehemu ile iliyoachia, pamoja na kuziba njia ya uzazi kuwa ndogo na mtoto kushindwa kutoka vizuri, kuzaliwa mtoto mfuu kwa kukandamizwa na kondo hilo, kuzaliwa mtoto njiti pamoja na kuzaliwa mtoto mwenye uzito mdogo
Naye Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Seif Rashid anasema kuwa tatizo la mjamzito kupoteza damu ni tatizo sugu na kubwa sana hapa nchini Tanzania na ndio chanzo kikubwa cha wajawazito kufariki. Dk. Rashid alisema kuwa, wataalam wa kulitatua tatizo hilo wapo wachache sana katika zahanati mbalimbali za vijijini ambako asilimia 75 ya watanzania ndio wanaishi huko.
“Kwa sasa tupo katika mkakati wa kuboresha zahanati mbalimbali kwa kuwapeleka watumishi wa sekta ya afya kusoma, masuala ya uuguzi kwa miaka miwili ili muuguzi anapokutana na tatizo hilo awe na ujuzi wa kumsaidia mjamzito,”alisema Dk. Rashid.
Wakati Sera ya Afya ya 2007 inasistiza utoaji wa huduma bora na bure kwa mjamzito, hili bado ni changamoto kwa maeneo kama Ifinga, Songea. Zahanati ya Ifinga ina nesi mmoja na muhudumu wa afya aliyefika darasa la saba mmoja. Pia, katika zahanati hiyo, kuna mganga moja na mpimaji magonjwa maabara mmoja.
Hakuna mtaalam wa magonjwa ya mjamzito na wala hakuna vifaa tiba kama mashine ya kumsaidia mtoto kupumua akizaliwa. Kwa wakati huu, ambapo Lusiana alikuwa ni mjamzito na kuhitaji huduma hizi, kulikuwa hakuna dawa za kumchoma sindano mama ili mfuko wa uzazi usinyae baada ya kujifungua na mzani wa kupimia mtoto akizaliwa mbovu.
Japokuwa ameshindwa kupata ufumbuzi wa tatizo lake, Lusiana anatarajia kujifungua katika zahanati ya Ifinga. Hana uwezo wa kwenda katika hospitali ya Peramiho inayomilikiwa na Kanisa Katoriki Jimbo la Ruvuma, ambapo ni kilometa 243 kutoka katika kijiji cha ifinga. Nauli ya kwenda ni Tsh.38,000 na gharama za kujifungua ni Tsh. 11,000; hapo bado gharama za kuishi.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Songea Dk. Daniel Masawe alisema kuwa katika wilaya hiyo, wajawazito 95 kati ya 100,000 kila mwaka wanapoteza maisha kwa sababu ya upungufu wa damu. Alithibitisha kwamba vifo hivi vinachangiwa na ukosefu wa vifaa tiba pamoja na wataalam wa kumsaidia mjamzito kujifungua salama katika zahanati mbalimbali kwenye wilaya hiyo.
"Kwa sasa watalaam wa kumsaidia mjamzito kujifungua salama ambao wamebobea katika ukunga hapa Songea ni wanne tu, ukilinganisha na zahanati 35 tulizonazo," alisema Dk. Masawe.
Mtaalam wa magonjwa ya akinamama katika hospitali ya Peramiho Dk. Marieta Mtumbuka alisema kuwa mwezi Septemba mwaka 2012, wajawazito wawili walifika katika hospitali hiyo wakiwa na tatizo la kupoteza damu. Kati ya hao ni mmoja alikuwa na miaka 37.
Mjamzito akiumwa malaria na kucheleweshwa au kutokumaliza matibabu, anakuwa hatarini kupatwa na tatizo la kutokwa na damu. Ndiyo maana, kwa mujibu wa Dk. Rashid kuna umuhimu wa mjamzito kutumia dawa ya mseto kwa sababu ndio dawa pekee iliyofanyiwa utafiti na kugundulika inaweza kutibu na kumkinga mjamzito na mtoto aliye tumboni na malaria akitumia kipindi ambacho haumwi malaria.
“Wizara imeamua kupitisha dawa ya mseto baada ya tafiti mbalimbali kubaini dawa ya chloroquin inausugu wa kuzoeleka na wadudu wa malaria. Tulipotoka katika dawa ya chloroquin tukaanza matumizi ya dawa ya fansider lakini nayo ikaonesha uwezo mdogo wa kukabiliana na wadudu wa malaria. Baada ya utafiti ndio tumegundua dawa mbadala ya kumkinga mjamzito na malaria ni dawa mseto,” alisema Dk. Rashid
Mjamzito anapewa dawa ya mseto akiwa na mimba ya wiki 20 na wiki ya 28.
Katika kitabu cha hotuba ya makadilio ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha 2012/2013, kinafafanua kuwa jumla ya dozi 9,196,080 za dawa mseto pamoja na kusambaza vyandarua vya hati punguzo vyenye viuatilifu 5,412579 kwa wanawake wajawazito lakini Lusiana hana chandarua.
"Nilipoanza kwenda zahanati kupima ujauzito wangu, sikupewa chandarua. Niliambiwa vimekwisha na sina uwezo wa kununua chandarua hivyo nalala bila ya kutumia hicho chandarua,"alisema Lusiana.
Aidha kwa mujibu wa bajeti ya afya ya mwaka 2012/2013, kumekuwa na ongezeko la vituo vya afya na zahanati za serikali na binafsi, kuanzia mwaka 2005 kutoka zahanati 4,322 hadi zahanati zahanati 4,679 mwaka 2012.
wa upande wa vituo vya afya, kumekuwa na ongezeko kutoka 481 mwaka 2006 hadi kufikia 742 mwaka 2012 na kwa upande wa hospitali kutoka 219 hadi kufikia 241. Hata bado kuna wanawake kama Lusiana wanaoshindwa kupata huduma za afya zenye ubora na kwa gharama wanazoweza kuzimudu.