Thursday, March 14, 2013

SABABU ZINAZOWAKIMBIZA WAJAWAZITO 'LEBA' BUNDA HIZI HAPA

  
Sababu kubwa inayopelekea wajawazito kujifungulia kwa mkunga wa jadi pamoja na nyumbani, ni lugha chafu za manesi, ukosefu wa vifaa tiba na madawa muhimu kwa mjamzito baada ya kujifungua.

Asilimia 100 ya wajawazito wanaohudhulia kliniki kipindi cha ujauzito katika wilaya ya Bunda mkoa wa Mara, lakini 68 pekee ndio wanaorudi kujifungulia katika zahanti, kituo cha afya na hospitali, asilimia 32 wanajifungua kwa mkunga wa jadi na nyumba kwa kusaidiwa na ndugu zao.

Ni kwa nini hasa manesi na wauguzi wa Bunda wanakuwa na lugha chafu kwa wajawazito mbalimbali, kwa sababu wako wachache na watejao wao ni wengi na hawana muda wa kumpunzika na hawalipwi pesa ya ziada katika kazi wanayoifanya.

Kwa mfano nesi na muuguzi mmoja katika wilaya hiyo kwa siku anahudumia wateja 60, wateja hao wakiwemo wajawazito kwa hali hiyo nesi na muuguzi huyu hawezi kutoa huduma bora kwa wateja zake kwa kutokana na wingi wa wateja kwa siku na malipo ya ziada baada ya kazi hayaoni.

Sofaeti Majanjara ni muuguzi katika hospitali teule ya bunda anasema kuwa, kwa siku anapokea wajawazito kuanzi 15 hadi 20 wote wanataka huduma ya kujifungua na yeye yuko zamu peke yake hana mtu mwengine wa mkumsaidia.

"Huwezi amini nafanya kazi hii kwa shida sana kwa sababu natoa huduma muhimu kwa wajawazito kujifungua, lakini naingia leba peke yangu bila ya kuwa na nesi au muuguzi wa kunisaidia, muda mwengine mama anajifungua peke yake kwa sababu nashindwa kujigawa na muda mwengine unakuta wajawazito sita wote wanaumwa uchungu wanataka kujifungua muda mmoja," alisema Majanjara

Majanjara alisema kuwa sio tuu wingi wa wateja zangu lakini pia hakuna vifaa vya kutosha kuweza kumsaidia mjamzito kujifungua vema, kwa mfano grove, sindano ya (oxytocin) kwa ajili ya kusinyaa kwa mfuko wa uzazi ili mama asipoteze damu nyingi baada ya kujifungua.

Sindano nyingine ni (maginesiam salfute) hii inamsaidia mjamzito mwenye tatizo la kifafa cha uzazi, anapoanza kuumwa anatakiwa kuchomwa dawa hii ili apone na kujifungua salama, hakanu nyuZi za kumshona mama ambaye amefanyiwa upasuaji.

Vifaa hivi ni vya muhimu sana kwa mjamzito anapoingia labe lakini katika zahanati, kituo cha afya na hospitali havipo, hivyo inamlazimu mjamzito kuvinunua katika maduka ya madawa na kukwenda navyo labe wakati wa kujifungua.

Kama mjamzito hana pesa ya kununua vifaa na dawa je anawezaje kukubali kwenda kujifungua katika hospitali wakati hana kifaa chochote, ndio hiyo asilimia 32 wanakwenda kujifungulia kwa mkunga wa jadi na nyumba kwa kukosa pesa ya kununua vifaa na kukimbia matusi, kashifa na vipigo kwa manesi na wauuguzi.
Kitanda-mkunga-jadi
Kitanda cha mtoto kwa mkunga wa jadi
Wilaya ya Bunda ina watumishi wapatao 362 lakini mahitaji ni 96, lakini kuna vijiji 106 na kila kijiji kina wakunga wajadi wawili jumla wanafika wakunga wa jadi 212 katika wilaya hiyo, wakunga hao sio tuu kuzalisha kinamama bali hata lugha na tabia kwa wateja zao ni nzuri ukilinganisha na hospitali ambako kuna mtaalamu.

Bunda inawakazi wasiopungua 3,75000 lakini vifo vya wajawazito kuanzia mwaka 2007 vilikuwa 310 kwa vizazi hai 100,000 kwa mwaka jana vimeshuka mpaka kufikia 77 kwa vizazi hai 100,000, lakini je takwimu hizi ni kwa wale wanaofika kujifungua hospitali na wanaojifungua nyumbani.

Mganga Mkuu wa wilaya hiyo Dokta Rainer Kapinga anakili kwamba vifo vilivyolipotiwa kwa wajawazito ni kwa wale wanaojifungua katika zahanati, kituo cha afya na hospitali, lakini kwa ile asilimia 32 wanaojifungua kwa mkunga wa jadi na nyumbani haijui kwa sababu ya kutojifungulia katika vituo vya kutoa huduma.
Mganga-Mkuu-Bunda
Mganga Mkuu wa wilaya Bunda Dokta Rainer Kapinga akifafanua matatizo ya wajawazito Wilayani Bunda
"Idadi ya vifo itakuwa kubwa kwa sababu wanaojifungua nyumbani ni wengi sana na hakuna taalifa yoyote tunayoipata kutoka kwa watendaji wa vijiji kwa sababu mjamzito amejifungulia nyumbani au kwa mkunga kwa hiyo wengi hawatoi hiyo taalifa," alisema Dokta Kapinga.

Katika kijiji cha Kambubu nakutana na mkunga wa jadi maalufu kama mama Nyangi, yeye ameanza kazi ya ukunga wa jadi akiwa na miaka 20, kwa sasa anamiaka 62 bado anafanyakazi ya ukunga wa jadi tena ndio tegemeo kwa wajawazito katika kijiji cha kambubu  ambacho kinazidi ya wakazi 4,000.
Nyangi
Nyangi, Mkunga wa jadi akinionesha dawa ya asili inayomsaidia mjamzito kusukuma kondo la nyuma la uzazi kama limegoma kutoka
"Kazi ya ukunga nimerithi kutoka kwa mama yangu alikuwa ananifundisha kuzalisha wajawazito mbalimbali kipindi cha uhai wake, nami nimejua mpaka sasa naendelea kutoa huduma hii kwa wateja zangu mbalimbali hapa kijijini kwa malipo ya sh. 2,000 hadi 3,000, maana hii ni kazi nimepewa na Mwenyezi Mungu ya kuwazalisha wajawazito,"alisema Nyangi.

Aidha alisema kuwa mjamzito anapofika nyumbani kwake anampokea vema, anamuandalia chai ya rangi ya moto anampatia mjamzito anakunywa huku akimwangalia kwa jicho la huruma na ukaribu na kumuuliza unajisiaje kwa sasa? mtoto anataka kuja? pia anampima kwa kutumia grove za mteja na kama hana anatumia za kwake akijifungua salama anarudisha zile grove ili azitumie kwa mwengine kama amefika kwake hana.

Kabla ya kumzalisha Nyangi lazima apige goti kwa Mwenyezi Mungu aswali ili kumuomba yeye kwa kazi ile anayofanya kwa mjamzito yule, akimaliza kumzalisha namuwekea maji ya moto choo na kwenda kumuogesha kisha mjamzito anapatiwa kikombe cha uji na kurudi nyumbani kwake.

"Kondo la nyuma likigoma kutoka anamchemshia maji ya vugu vugu kikombe kimoja na kuchanganya pamoja na chimvi kisha kumpatia anywe au anatumia majani ya kiasili kumtengenezea kama juice kisha kumpatia mjamzito anywe baada ya nusu saa kondo linatoka, pia anakitanda maalumu kwa kujifungulia mjamzito na kitanda kingine kwa ajili ya kumuweka mtoto changa," alisema Nyangi

Devota Chacha ni mjamzito wa miezi sita na mkazi wa kijiji cha Kambubu, anahudhulia kliniki kama kawaida lakini hayuko tayali kwenda kujifungulia katika kituo cha afya cha Ikizu au hospitali teule ya bunda, kwa sabau ya lugha chafu za wauguzi na manesi, ghalama ya usafiri mpaka mjini pamoja na ghalama za vifaa akiingia leba.

"Nitajifungulia kwa mkunga wa jadi Nyangi kwa sababu sina uwezo wa kughalamia huduma ya kujifungua kama kituo cha afya ikizu ukiingia lazima ulipie sh. 7,500 kwa ajili ya kitanda na mchango wa mafuta ya gari wakati kituo hakina gari, mpaka unajifungua ni zaidi ya sh.20,000 hadi 30,000 wakati kwa mkunga ni sh. 2,000 hadi 3,000," alisema Devota.

Hii ndio hali halisi ya upatikanaji wa huduma kwa wajawazito mbalimbali katika wilaya ya Bunda, lakini hali bado ni tete kwa sababu kati ya wajawazito 10 basi wawili wanaupungufu wa damu kwa kukosa kula samaki wenye madini mengi, inawezekana wajawazito hawa wawili kati ya 10 wenye tatizo la upungufu wa damu ndio wanaojifungulia kwa mkunga wa jadi kama Nyangi.

Hali itakuwa mbaya zaidi kwa vifo vya wajawazito katika wilaya ya Bunda, lakini hii ni wilaya moja tuu na Tanzania ni kubwa sana na asilimia 80 ya wakazi wake wanaishi vijijini, huko nako hali ikoje ambako mimi mwandishi sijafika na kujionea kwa macho yangu.

Nani wa kuwajibika juu ya hili wananchi, wakunga wa jadi kuacha kuzalisha, viongozi wa afya upande wa wilaya au viongozi wa afya wizara? ni lini hasa Tanzania itakuwa haina vifo vya wajawazito? kila mtu anatakiwa kuangalia jukumu lake na kufanyakazi ya kuokoa wajawazito wa Tanzania kwa pamoja kwani umoja ni nguvu.

0 comments:

Post a Comment