HAKUNA anayejali kama mjamzito iwe kijijini au mjini anapotaabika
na mimba yake wakati mtoto anayezaliwa ni mali ya taifa. Hakuna mtaalam
wa afya anayejali kuona mjamzito anateseka na kushindwa kusukuma mtoto
wakati wa kujifungua na hakuna anayejali kuona watoto wachanga hasa
vijijini wanapokufa baada ya kuzaliwa.
Hakuna anayejali kuona wanawazito kukokotwa kwenye mikokoteni ya
punda na baiskeli kufuata huduma ya kujifungua. Hakuna anayejali wakunga
wa jadi wanaosaidia wajawazito kujifungua salama na hakuna anayejali
kutimiza ahadi kuhakikisha huduma bora za afya kwa mama na mtoto chini
ya miaka mitano.
Hakuna anayejali kutenga bajeti za uhakika kwa ajili maji safi
vijijini. Hakuna anayejali kusogeza kwa vitendo huduma za afya katika
vitongoji na hakuna anayejali kuona kupunguza mila na desturi kwamba
wajawazito kujifungulia nyumbani ni ujasiri.
Hakuna anayejali kusikia wajawazito wakitolewa kauli chafu kutoka kwa
baadhi ya watoa huduma za afya. Hakuna anayajali kutatua kwa dhati
tatizo la uhaba wa vitendea kazi katika huduma za afya. Hakuna anayejali
ukosefu wa maji safi katika vituo vya afya hospitali na zahanati.
Hakuna anayajali kutenga na kuweka sehemu ya kupumzika wajawazito
kabla na baada ya kujifungua hasa kwenye zahanati. Hakuna anayejali
kutoa elimu ya uzazi wa mpango kwa jinsi zote badala yake elimu hiyo
inatolewa kwa upande wa wanawake ambao ‘’wanaiba’’ kutumia huduma hiyo
na wakibainika na waume zao wanapigwa na wengine wamepoteza maisha.
Hakuna anayejali kuona mimba za utotoni zikiendelea kutokea kila siku
kutokana na mila na desturi, hakuna anayejali sheria mbaya ya ndoa na
mkanganyiko kati ya sheria ya ndoa inayoruhusu msichana wa miaka 14
kuolewa kwa idhini ya wazazi wake na katiba inayomtambua mtu mzima kuwa
ni yule mwenye miaka 18.
Hakuna anayejali kuona wanaume wananyanyaswa na wake zao na
kulazimika kukimbia ndoa na kuwaacha watoto wakiteseka huku wengine
wakipoteza maisha na hakuna anayejali kuona watoa huduma za afya
wakiishi umbali mrefu na maeneo yao ya kazi.
Inasikitisha kuona hakuna anayejali malalamiko ya wataalamu wa afya
kuendelea kununua dawa za wagonjwa kwa mfumo mbovu wa MSD wakati mfumo
huo ni mbovu na dawa zinazotakiwa kuuzwa kwa shilingi 10,000 zinauzwa
shilingi 30,000 kupitia watendaji wa serikali wanaohusika na manunuzi.
Hakuna anayejali kuona mtumishi anaacha taaluma yake ya awali na
kujiunga na masomo ya ununuzi wa umma kwasababu huko ndiko kwenye rushwa
na uchafu usioandikika wa wizi wa fedha na mikataba mibovu.
Mambo kadhaa niliyoyaanisha hapo juu yapo wilayani Bunda mkoani Mara
ambako kuna idadi kubwa ya vifo vya akina mama na watoto wenye umri
chini ya miaka mitano vinavyotokana na uzazi nchini Tanzania.
Baadhi ya wananchi wanaopata huduma za afya katika kituo cha afya cha
Ikizu kilichopo katika kijiji alichozaliwa Jaji Joseph Sinde Warioba
wananungunika kuwa Rais Jakaya Kikwete ameshindwa kutekeleza ahadi yake
ya kupeleka gari la wagonjwa katika kituo hicho.
Wanasema kuwa kukosa gari kwa kituo hicho cha afya kunasababisha
wagonjwa wakiwemo wajawazito wanaotakiwa kufanyiwa upasuaji kukodi
‘’Toyo’’pikipiki ili kupelekwa hospitali teule ya wilaya.
‘’Tunalazimika kukodi ‘’Toyo’’ au ‘’michomoko’’ tax kwa Sh.30,000
ili kuwapeleka wagonjwa ‘’DDH’’ hospitali ya wilaya’’ walisema baadhi ya
wananchi ambao waliomba hifadhi ya majina yao.
Mbali na hilo, baadhi yao wanaulalamikia uongozi wa kituo hicho cha
afya cha Ikizu kuwa unawauzia damu ya kuongezea wagonjwa kati ya
Sh.15,000 mpaka Sh. 20,000 kwa unit moja(mfuko).
Mganga mkuu kiongozi wa kituo hicho cha afya cha Ikizu kilichopo eneo
la kata ya Nyamuswa tarafa ya Ikizu Dr.Abahehe Kanora, anasema kuwa
kituo hicho hakina gari la wagonjwa na walitegemea kuwa Rais Kikwete
angewapelekea kutokana na ahadi yake alipokuwa akiomba kura kwa wananchi
wa eneo hilo mwaka 2010.
‘’Hapa kulikuwa na gari Pick up lakini iliuzwa na kuharibika mwaka
1996 na wilaya ina ambulance moja tu, tegemeo letu kubwa pamoja na
wananchi ilikuwa ni kutimia ahadi ya Rais Kikwete ambapo aliahidi pale
njia panda kwenye mti wa kumbukumbu ya Chifu Makongoro aliposimamishwa
na wananchi mwaka 2010’’ anasema Dr. Kanora.
Kuhusu usafiri kwa wajawazito wanaokwenda kujifungua katika kituo
hicho, anasema wanasafiri kwa pikipiki na wanaotakiwa kufanyiwa upasuaji
wanalazimika kukodi gari maarufu kwa jina la michomoko kisha kupelekwa
hospitali teule ya wilaya (DDH) iliyopo umbali wa kilomita 24.
Akizungumzia uhalisia wa kituo hicho ha afya, Dr. Kanora anasema kuwa
mbali na tatizo la gari la wagonjwa, pia kuna tatizo la upatikanaji wa
dawa kutokana na mfumo wa manunuzi ya umma unaowalazimisha kununua dawa
zote katika bohari ya serikali yaani MSD ambapo dawa hupelekewa pungufu
tofauti na mahitaji.
Alipoulizwa kama wajawazito na watoto hupatiwa matibabu bure kama
inavyoelekezwa na sera ya afya ya mwaka 2007 ili kupunguza vifo vya
makundi hayo, alisema kuwa kwanza hakuna dawa zinazopelekwa maalumu kwa
ajili ya makundi hayo lakini wajawazito hupatiwa bure huduma za
kujiandikisha Kliniki, kujifungua na vipimo.
Kuhusu wagonjwa wakiwemo wajawazito kuuziwa damu kwa Sh. 15,000 mpaka
20,000. Alisema malalamiko hayo si ya kweli bali uongozi wa kituo
ulikubaliana na kamati ya afya ya eneo hilo kuwa kutokana na uhaba wa
vitendanashi ikiwemo vifaa na dawa za kupimia damu kila anayeongezewa
damu anachangia Sh. 2000.
‘’Malalamiko hayo si kweli bali kumekuwa na tabia kwa baadhi ya
wagonjwa na ndugu zao wanaohitaji damu wakiambiwa kuwa hatuna damu ndipo
wanalazimika kuwatafuta watu nje ya kituo na kuja nao ili kuwatolea
damu hao ndiyo wanaowauzia lakini sisi hapa anayechangia damu na
anayeongezewa kila mmoja hutozwa Sh. 2000’’ alisema Dr. Kanora.
Kuhusu maji alisema kuwa mpaka sasa kuna tatizo kubwa la maji na kila
mgonjwa wakiwemo wajawazito lazima aende na ndugu yake ambapo baadhi ni
lazima waende na maji eneo la kituo hicho cha afya.
Mpaka waandishi wa habari wanaondoka eneo hilo la kituo cha afya,
wameacha na kushuhudia familia mbili za watumishi wa kituo hicho wakiwa
hawana vyoo na kulazimika kujisaidia katika choo cha wagonjwa kilichopo
umbali wa mita 25 baada ya choo walichokuwa wakichangia kubomoka.
Baadhi ya wajawazito na akima mama wanaonyonyesha wanaoishi katika
maeneo ya Bukama, Makongoro kata ya Nyamuswa, Nyabuzumu na kijiji cha
Kambubu kata ya Nyamang’uta walisema kuwa kutokana na huduma
zisizoridhisha katika kituo hicho cha afya na hospitali teule ya wilaya
hiyo, wanaona ni bora kujifungulia kwa wakunga wa jadi.
‘’Mimi uzao wangu huu ni wa nane lakini nina watoto watato walio hai
na wengine nilijifungulia kwa mkunga wa jadi Mama Nyangi Kisizile
kwasababu hospitalini kuna matusi na fedheha nyingi na wala
hatusaidiwi’’ alisema Anna Japhet(35) mkazi wa Kijiji cha Kambubu.
Utafiti nilioufanya umebaini kuwa katika kijiji hicho kuna wakunga wa
jadi watatu ambapo eneo la Mugara linaongoza kwa wajawazito
kujifungulia kwa wakunga wa jadi.
Takwimu zinaonesha kuwa akina mama mama 185 walijifungulia kwa
wakunga wa jadi waliopata mafunzo na akina mama 71 walijifungulia kwenye
zahanati ya Mugara mwaka 2009.
Ingawa wakunga wa jadi wanapuuzwa na kudharaulika na wasomi wengi
lakini ukweli wa utafiti unaonesha kuwa kujifungulia kwa wakunga wa jadi
hasa waliopata mafunzo kunapunguza kama si kuondoa kabisa tatizo la
vifo vya akina mama wajawazito, lakini hakuna msomi anayejali kuwapa
mafuzo kwa dhati wakunga wote wa jadi nchini.
Naye mjamzito Agness Baraka (23) anasema mimba aliyonayo ni ya nne
lakini ana mtoto aliye hai mmoja na kwamba anahudhuria kliniki lakini
bado halidhishwi na huduma za hospitalini hivyo anaona bora kujifungulia
kwa mkunga wa jadi ama nyumbani kama alivyojifungua mtoto wake wa
kwanza.
‘’Ukienda hospitali mfano kule DDH, wanasema kuwa mjamzito
anayepaswa kusaidiwa kujifungua ni yule mwenye mimba ya kwanza lakini
tuliowahi kuzaa wanatulazimisha tujifungue wenyewe bila msaada wao na
kama hauna pesa unaweza kufa’’ anasema Anna.
Mkunga wa jadi Veronica John Leopard(64), alisema kuwa yeye ni mmoja
wa wakunga wanaosaidia wajawazito kujifungua katika wilaya ya Bunda na
hata hospitali wanamjua lakini halidhishwi na huduma zinazotolewa na
kituo cha afya cha Ikizu maana kila kitu ni pesa na hivi karibuni
alimpeleka mwanaye kujifungulia katika kituo hicho na kujionea huduma
zisizoridhisha.
Umefika wakati kama taifa kujisahihisha kwa vitendo mfano suala la
bajaji za kubeba wajawazito bila kutafuna maneno hazifai na mpaka sasa
hazitumiki kwasababu hazikati kona upande wa kushoto hivyo rai yangu kwa
Rais Kikwete ni kuliona hilo na kutatua kero hizo hapo juu kwa vitendo
ili kujenga taifa imara lenye watu wenye afya njema kwa kuanzia katika
makundi hayo yaani wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.
Wednesday, March 13, 2013
"HAKUNA ANAYEJALI VIFO VYA WAJAWAZITO NA WATOTO WACHANGA!"
2:11 AM
No comments
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment