Thursday, March 21, 2013

KARUNGUYEYE, MUUGUZI ASIYE NA TAALUMA YA AFYA ANAYETOA HUDUMA KWA MIAKA 22

Benjamin  Karunguyeye  (55)  amefanya kazi ya kuwahudumia wagonjwa mbalimbali katika kijiji cha Ifinga, Songea kwa takriban miaka 22 sasa, pasipo kusoma katika darasa lolote la uuguzi au udaktari.


Anapima na kuwazalisha wajawazito na kuhudumia watoto wa chini ya umri wa miaka mitano kwa kuwapa chanjo.

 Kwa kipindi cha mwaka mmoja, kuanzia Agosti mwaka 2011 mpaka Agosti 2012, alikuwa akisimamia na kuendesha huduma zote katika zahanati ya Ifinga peke yake.

Alikuwa akiwapima na kuwatibu watu wenye dalili za magonjwa mbalimbali yakiwemo ya ngono kama kaswende, kisonono, maambukizi ya gono na ukimwi. Alikuwa akiwachoma sindano, kuwasafisha vidonda na kuwang’oa meno.

“Nimeanza kazi hii ya kuwahudumia wanaifinga rasmi toka mwaka 1990, katika zahanati hii ya kijijini kwetu. Kabla ya hapo nilikuwa najaribu jaribu kwa kutoa huduma ndogo kama kusafisha vidonda,”alisema Kalunguyeye.

Kalunguyeye, ambaye hana sifa zozote za kitaaluma, alianza kutoa huduma katika zahanati ya Kanisa Katoliki, ambayo inasimamiwa na Jimbo Kuu la Songea, baada ya waganga na manesi walioletwa hapo na uongozi wa Kanisa Katoliki kuondoka.


"Ndipo hapo nami nikaanza kuibia ibia kutoa huduma mbalimbali kwa wanakijiji wenzangu, kwa sababu nilikuwa nashuhudia wakifariki kwa kukosa kuhudumiwa,"alisema Kalunguyeye.

Kwa upande wake Father Roja Haule alisema kuwa, yeye amefika ifinga mwaka 2005 amemkuta Kalunguyeye akitoa huduma katika zahanati hiyo.
Kalunguyeye alianza kufanya kazi katika zahanati hii mwaka 1985. Kazi zake zilikuwa ni kufanya usafi kama kufagia, kupiga deki, kuchota maji, kusafisha vyoo na kuosha vifaa mbalimbali wanavyotumia kuoshea vidonda.

“Kipindi hicho nilikuwa anafanya usafi tu, na nikimaliza naondoka kwenda nyumbani. Lakini, ilipofika mwaka 1988, nilikuwa nabaki nikimaliza kufanya uasfi, ili kuangalia jinsi gani huduma mbalimbali zinazotolewa na  mganga na nesi, lengo langu lilikuwa kujua wananchi wanavyotibiwa ili nami niwatibu,”alisema Kalunguyeye.

Alifanikiwa kujifunza namna ya kuosha vidonda, kuchoma sindano na kutoa chanjo kwa watoto.Kalunguyeye alisema kuwa mwaka 1989 nesi na mganga waliondoka na kumuacha na zahanti bila ikiwa chini yake.

Kalunguyeye alisema kuwa kipindi hiki ambacho mganga na nesi waliondoka na kuniacha kwa muda wa miezi mitatu, ndio alianza kazi ya kutibu kama tatibu aliyesomea katika chuo cha matatibu.
Mganga na nesi waliletwa mwezi March mwaka 1989, kilikuwa kipindi cha mvua na barabara ilikuwa mbaya sana, walifika ifinga kwa shida sana, walioa huduma kwa muda wa miezi mitatu kisha wakaondoka na kuniachia zahanati peke yangu.
“Mwaka huo ndio ilikwa mara ya kwanza kuanza kazi ya kutibia watu nikiwa peke yangu, ilikuwa ngumu sana kwa sababu mambo mengi sikuwa nayafahamu, nitoa huduma ile niliyokuwa kama kuchoma sindano, kutoa dawa za malaria, kupima watoto na kupima wajawazito, ugonjwa ninaoshindwa namueleza aende kituo cha afya mabada ambako ni kilometa 87 kutoka Ifinga,”alisema Kalunguyeye.
Kazi ya kutoa huduma aliifanya kwa muda wa miezi mitatu kuanzia mwezi wa Juni hadi September, walipoletwa mganga na nesi.
Lakini, zahanati ya Ifinga ina changamoto nyingine kama  kuchelewa kupatiwa madawa pale yanapokwisha. 

“Ukienda mjini kuchukua dawa kwa Rosyita Lugongo Katibu wa afya wa Jimbo la Songea pia ndio msimamizi wa zahanati zote za Kanisa Katoriki Songea, unafikia kwenye nyumba za kulala wageni. Una weza kukaa mjini kwa wiki moja ukisubiri madawa yanunuliwe ndipo upatiwe na kurudi ifinga,gharama za kusubiri madawa unajilipia mwenyewe kwa muda wote huo, ukidai unaambiwa ofisi haina pesa, unaambulia kupewa nauli ya kurudi ifinga tu. Hicho ndio kitu kingine kinachowakimbiza waganga na manesi Ifinga. Mie nikifika mjini, nafikia kwa ndugu yangu kwa hiyo huwa sina gharama kubwa,”alisema Tobias Millinga, ambaye ni mganga wa zahanati hiyo kwa sasa.

Wakati sera ya afya ya mwaka 2007 inaeleza kuwa, serikali itashirikiana na wadau mbalimbali kuimarisha afya ya uzazi ya wanawake na wanaume, watu wenye ulemavu na wazee. Pia anaendelea kueleza kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itahakikisha utoaji wa huduma bora za afya ya uzazi katika vituo vya kutolea huduma za afya vinovyowavutia wanawake, wanaume na vijana.
Huku sera hii ikisema hivi lakini uhalisia wake haupo kabisa, kwa mfano katika zahanati ya Ifinga ambayo iliyojengwa na Kanisa Katoliki hakuna miundombinu ya maji, umeme, chombo cha darubini kinatumia mwanga wa jua, pia jengo lake ni chakavu sana na mhusika wa kujua hali halisi ya zahanati yupo lakini hawajibiki.
Rosyita Lugongo katibu wa afya Jimbo la Songea,ndiye anayesimamia utoaji wa huduma za afya na ubora wa majengo hayo ya zahanati 14 na hospitali ya peramiho zilizojengwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Songea.
Kwa mujibu wa Father Roja Haule alisema kuwa sio ubovu wa zahanati tuu hata Kanisa la Ifinga limechoka sana, lakini Katibu wa Jimbo anaomba pesa katika mashirika ya dini huko Ujerumani lakini pesa haifanyi kazi yake inayotakiwa ya kuboresha miundombinu ya maji, umeme na kukarabati majengo.
Juhudi za kumtafuta Katibu wa Jimbo hilo, kujibu matatizo mbalimbali ya zahanati ya Ifinga, mpaka kupitia kwa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Ruvuma Dokta. Daniel Malecela kwa kumpigia simu na kwenda kuongea ili niweze kumuhoji changamoto hizo, alikata kata kata kuona na mimi na kumwambia hataki kuongea na Mwandishi wa Habari.
Serikali inatakiwa kuwajibika katika suala la kuangalia ubora wa huduma zinazotolewa katika zahanati mbalimbali nchini, kama sera ya afya inavyosema na sio kuwaachia washikadau mbalimbali kutekeleza upatikanaji wa huduma bora.
Milinga anasema kuwa walipofika Ifinga walipokelewa na Kalunguyeye, aliwaonesha mazingira ya zahanati hiyo. Lakini alisema kuwa Kalunguyeye ni mchapakazi sana anafanya kazi ya kutoa huduma kama amesomea, kwa mfano atoa chanjo kwa watoto, anawapima wajawazito, anatoa dawa za usubi majumbani.

Tobias Milinga ndiye msimamizi wa zahanati ya Ifinga kuanzia mwezi Agosti mwaka 2012, lakini yeye anataaluma ya maabara tuu aliyosomea katika chuo cha maabara katika hospitali ya Litembo Mbinga kwa muda wa miaka miwili, na kuuza kazi ya kuchunguza magonjwa mbalimbali.
 Kutokana na uhaba wa watumishi katika zahanati hiyo ambayo ina nesi nay eye mganga wa maabara lakini anafanya kazi ya kuwaona wagonjwa na kisha kupima magonjwa yao maabara,ndio maana hata yeye alivyofika akamuachia Kalunguyeye aendelee kuzalisha wajawazito.
Kalunguyeye alisema anaipenda kazi yeka na anaifanya kwa ajili ya ndugu zake wa Ifinga, kwani walikuwa wakipata shida ya kutopata huduma za afya baada ya mganga na nesi kuondoka.
Kijiji cha Ifinga kiko mbali na kituo cha afya cha madaba ni umbali wa kilometa 87, na hospitali ya peramiho ipo umbali wa kilometa  243 kutoka katika kijiji hicho, kwa sababu hiyo mganga Milinga na Kalunguyeye ndio msaada pekee katika zahanati hiyo.

Kijijni Ifinga Kalunguyeye anafahamika kwa jina la ofisa tabibu na anajulikana hivyo kwa kazi yake ya kutoa huduma za afya kwa wanakijiji hao.

“Huduma anayotoa Kalunguyeye ni nzuri sana. Amenizalisha mtoto huyu ana miaka (22) kwa sasa unayemuona hapa, ambaye amekuwa vema mpaka nayeye ameowa na sasa nina wajukuu kutoka kwa mtoto huyu  aliyenizalisha Kalunguyeye. Nampenda sana kwa kazi ya kutoa huduma,” alisema Devota Ndunguru (40)

Kwa upande wake, Kalunguyeye anasema, “Siku ya kwanza kumzalisha mjamzito nilipata taabu kidigo. Alifika mjamzito akiwa anaumwa  uchungu na nikamwambia panda kitandani. Nikavaa gloves na kumpima kama njia ya uzazi imefunguka. Nikaona imefunguka kwa sentimita 6 hivyo nikamwambia bado. Baada ya saa mmoja kupita, nikampima tena na nikakuta njia imefunguka kwa sentimita 8. Nikamwambia sukuma. Akasukuma na mtoto akatoka vema. Baada ya hapo, kutoa kondo la nyuma ndio ilikwa  tatizo maana halikutoka haraka nami nilikuwa sijui vema kulitoa kwa mkono. Ilibidi ni mtume ndugu yake yule mjamzito akamwite mkunga wa jadi aje kulitoa na, alipofika aliingiza mkono na kulitoa nje lile kondo nami hapo ndio nikajua jinsi ya kutoa kondo,” alisema Kalunguyeye.

Kalunguyeye alisema kuwa nimejua kipimo cha sentimita ya njia ya uzazi kupitia kwa manesi mbalimbali waliofanya kazi ya kuzalisha kipindi cha nyuma.

Aidha, alisema kuwa wiki moja baada ya tukio hilo, alikuja mtoto anaumwa jino mpaka shavu limevimba kwa maumivu. Kitu cha kwanza alicho kifanya ni kumwambia mzazi wake ambane vema.
“Kisha nilamwambia ufunue mdomo wake na nikachukua kifaa cha kung’olea jino.Nikaanza kuyagonga meno yote mpaka nilipofikia katika jino bovu ndipo mtoto huyo alipiga kelele na nikajua kuwa jino hilo ndio bovu. Nikaweka ganzi kwenye bomba la sindano na kumchoma pale kwenye lile jino bovu. Baada ya nusu saa ndio nikalitoa kwa umakini ili lisivunjike.”

Changamoto kubwa anayokutana nayo katika kazi hii, ni kulipwa kiasi cha shillingi 7,000 kwa mwezi, kwani anatambulika rasi kama anafanya kazi ya usafi. Malipo yake yanatolewa na uwongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Ruvuma.Lakini anasema hela anayopewa haitoshi ukilinganisha na gharama za maisha zilivyo.
“Napata pesa ya kujikimu kwa kupitia kazi ninazozifanya.Kung’oa meno ni shillingi 3,000, kusafisha kidonda ni shilling 2,000 na kupasua jipu ni shilling 1,500. Napata pia hela nyingine kutokana na kutibu magonjwa mengine. Hapo ndio napata pesa ya kula na familia yangu,” alisema Kalunguyeye.

Diwani wa kata ya Ifinga Rogatusi Kianjali, alisema kuwa mwaka 2009, walikaa katika vikao vya kila mwezi vya kujadili maendeleo ya kata, na katika kikao hicho kulikuwa na wajumbe mbalimbali wa kila kata, pamoja na Father Roja Haule ambaye ni kiongozi wa Kanisa katika zahanati hiyo. Kikao hicho kiliamua kuthibitisha Kalunguyeye kuwa mhudumu wa afya wa kijiji na kumfutia majukumu ya kuchangia katika kijiji.

"Natamani kusoma kama waganga wengine juu ya taaluma hii, ambayo ninaifanya kwa muda wa miaka 22. Ningekwenda chuo cha matabibu ningeweza kufanyakazi vizuri zaidi,”alisema Kalunguyeye.

Vigezo vya kujiunga na chuo cha utabibu cha serikali hapa nchini kama Lindi, Bugando , Muhimbili na Musoma, kwa ngazi ya stashahada lazima uwe umefaulu kwa kiwango cha alama C katika masomo ya Phisikia, Bailogia na alama D kwa soma la Kemia na masomo yake ni ya muda wa miaka mitatu chuoni. Ada yake ni shilingi 600,000 na shilingi 15,0,000 kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo. Kama mhusika hana bima, analipia shilingi 50,400  zaidi na jumla yake ni shilingi 800,400 kwa kila mwaka.

Kwa upande wa utabibu ngazi ya cheti, anatakiwa  awe amefauru somo la Bilogia na alama ya C, somo la Kemia na alama ya D na katika somo la Fizikia anatakiwa kuwa na alama D. Ada yake kwa mwaka ni shilingi 550,000 na 150, 000 ya kujifunza kwa vitendo. Pia, kama mhusika hana bima ya afya anatakiwa kutoa shilingi 50,400 na kufanya jumla ya shilingi 750,400.

Kwa upande wa vyuo binafsi kama chuo cha uuguzi cha Kanisa Katoliki ambacho kipo Ndanda, Mtwara, vigezo vinafanana na vile vya vyuo mbalimbali vya serikali ambavyo vinafundishwa utabibu, gharama kwa stashahada na cheti ni milioni 1.150,000.

Mratibu wa masomo ya kujiendeleza kwa watumishi wa afya mkoa wa Lindi, Dokta Betram Mnyani alisema kuwa kuna, umuhimu wa kijiendeleza kwa mhudumu wa afya au mfanya usafi katika seheumu za kutoa huduma. Umuhimu wake unakuja pale kunapotokea upungufu wa watumishi katika zahanati, na kulazimika huyu mhudumu kupewa kazi ya ziada ambazo yeye hajaisomea chuoni. Hii inaweza kutokea na kazi anazoweza kupewa ni kama  kugawa dawa, kumuwekea damu mgonjwa, kuchoma sindano, kusafisha vidonda, kuzalisha na kazi zingine za kitabibu wakati yeye ameajiriwa kwa kazi ya kufanya usafi katika zahanati, kituo cha afya na hospitali.

Japokuwa Kalunguyeye amekata tama ya kusoma kwa sababu elimu yake haimruhusu kuendelea mbele na,  hana uwezo wa kulipa ada ya chuo cha utabibu, anasema hana mpango wa kuacha kufanya kazi hiyo.

Pia baadhi ya wanakiji wa Ifinga wanatambua umuhimu na mchango wake.
Stella Ngonyani (27) ni mwanakijiji wa Ifinga ambaye alisema wanawake katika kijiji hicho wanamtegea sana Kalunguyeye.

Naye Mashaka Komba (32), ambaye ni mkazi wa Ifinga anaongezea kwa kusema, “tunatibiwa vizuri. Kama unaumwa homa, Kalunguyeye anakuchoma sindano. Binafsi, leo nimemleta mtoto kung’oa meno mawili, la juu na la chini. Ameng’oa asubuhi vema na jioni hii huyu mtoto anacheza kama unavyomuona.” Alisema Mashaka.

Hata hivyo, zahanati ya Ifinga inakabiliwa na changamoto mbalimbali, hususan kwenye vifaa. Mfano, haina kifaa cha kumtoa mtoto uchafu baada ya mjamzitokujifungua na haina kifaa cha kumsafisha mama ambaye mimba iliharibika. Pia, japokuwa Kalunguyeye ni msaada mkubwa kwa wanakijiji, anakosa utaalam  wa kutoa huduma hii.


Anna Ndunguru (30) ambaye ana ujazito wa miezi saba anasema Kalunguyeye ndiye anaye mpima akienda kliniki kila tarehe inapofika. Ndunguru anasema changamoto kubwa iliopo ni kukosekana au upungufu kwa vifaa.
Kuhusu huduma, Ladilaous Nyamakilau (65)  alisema, “Mzee kama mie na wanakijiji wote hapa kijijini tunamtegemea kwa huduma  nzuri ya kututibu magonjwa mbalimbali.”alisema Nyamakilau

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Ifinga, Zaituni Mango alisema Kalunguyeye ndiye mkombozi wa wanakijiji, kwa kuwatibu magonjwa na kuwasambazia dawa za  magonjwa ya milipuko kama surua, kuhara, usubi, tetekuanga na kipindupindu.
“Bila ya Kalunguyeye mambo yangezidi kuwa mabaya. Anafanya kazi ya kutibu wanakijiji kwa moyo mmoja na anatembea kwa saa nne hadi tano  mpaka kijiji cha pili cha Luhuji kwa mguu kutoa dawa za magonjwa ya kuambukiza na kuwapima akinamama wajawazito na watoto wa chini ya miaka mitano,” alisema Mango.

Kwa upande wake Kaimu mganga mkuu wa Wilaya ya Songea Dokta Daniel Masawe, alisema kuwepo kwa Kalunguyeye katika zahanati ya Ifinga ni kwa sababu ya uhaba wa waganga na manesi.

“Serikali kupitia Wizara husika ya afya, watuletee watumishi wa kada mbalimbali ya afya, ili kuweza kuziba pengo la ukosefu wa wakunga, manesi na waganga. Sio Ifinga tuu kwenye tatizo hili;  zahanati zetu zote zinaupungufu wa watumishi. Tunatambua mchango wake kwa wanaifinga na anawatibu lakini kwa mujibu wa sheria na taratibu za utumishi wa umma, hana vigezo vya kuajiriwa kama mhudumu wa afya. Kilichofanyika na Serikali ya kijiji cha Ifinga ni kumfutia kutoa michango ya maendeleo ya kijiji kama kutoa ushuru na kutoa tofali za ujenzi wa shule.”  

Kitabu cha ikama cha mwaka 1999 kinaeleza kuwa watumishi katika zahanti wanatakiwa kuwa watano, wa kada mbalimbali. Wanaohitajika ni afisa tabibu wawili wenye kiwango cha elimu cha stashahada ya juu ya tabibu na stashahada ya tabibu.

Kwa upande wa nesi, wanatakiwa kuwa wawili; mmoja anatakiwa na stashahada ya uuguzi na mwengine anatakiwa kuwa na cheti cha uuguzi Pia, zahanati inapaswa kuwa na mhudumu wa afya aliyependekezwa na kijiji husika, lakini kabla ya kuanza kutoa huduma, anatakiwa kupewa mafunzo ya msingi ya mwaka mmoja.

Kituo cha afya kinatakiwa kuwa na watumishi 28. Wanahitajika waganga wawili wenye elimu ya stashahada ya juu na ofisa tabibu mwenye stashahada. Nesi wanatakiwa kuwa wanne wa kada mbili tofauti, kada ya kwanza ya nesi ni ya elimu ya stashahada ya juu na kada ya pili ni ya stashahada uuguzi. Pia  anahitajika msaidizi, awepo mtaalamu wa teknologia ya maabara mmoja, na anatakiwa mgawa dawa mmoja mwnye elimu ya stashahada ya madawa. Wengine ni, afisa afya  msaidizi wenye elimu ya stashahada na msaidizi wa  afya ya mazingira mwenye elimu ya ngazi ya cheti.

Aidha, katika kituo cha afya pia kunatakiwa kuwa na wahudumu wa afya wasiopungua watano  wenye  elimu ya kidato cha nne pamoja na kusomea kozi ya mhudumu wa afya kwa mwaka mmoja, mhasibu, seketari, fundi wa umeme na vifaa mbalimbali vya hospitali, mfanya usafi na  mlinzi.

Kwa upande wa hospitali, kunatakiwa kuwa na watumishi wa kada mbalimbali wapatao 195.

Changamoto kubwa iliyopo kwa sasa katika serikali ya Tanzania  ni uhaba wa watumishi mbalimbali katika kada ya afya. Kwa sasa, daktari mmoja anahudumia wagongwa 30,000 na nesi mmoja anatibu wagonjwa 23,000. Hi ni kwa mujibu wa Rais Jakaya Kikwete, katika hutuba yake ya kila mwezi Agosti mwaka jana.

Katika hotuba hiyo, rais alisema  kuwa wanalijua tatizo hilo na wameanza kulitatua kwa kujenga vyuo mbalimbali vya madaktari kama Chuo cha Mloganzila, shule ya kufundisha madaktari pamoja na kupanua mafunzo ya manesi na wakunga

0 comments:

Post a Comment