Zarula Rajabu (30) anaishi na virusi vya ukimwi,anawatoto wanne kati ya hao mtoto mmoja ana maambukizi ya virusi vya ukimwi, anishi katika kijiji cha Matekwe katika kata ya Kilimarondo wilaya ya Nachingwea mkoa wa Lindi.
Zarula aligundulika na vvu akiwa na ujauzito wa miezi sita, alipohudhuria kliniki ya zahanati ya Matekwe kwa mara ya kwanza. Lakini hakupewa dawa za ARVs za kumkinga mtoto aliyetumboni asipate na maambukizi ya virusi vya ukimwi.
“Ningepatiwa dawa za ARVs kipindi cha ujauzito wangu, na wakati wa kuumwa uchungu, ningemzaa mtoto wangu bila ya kupata maambukizi ya virusi vya ukimwi na angeishi maisha marefu,”alisema Zarula.
Muuguzi katika zahanati ya Matekwe Lidia Urio (51) alisema kuwa, Zarula alipohudhulia mara ya kwanza kliniki alimpima na kugundua kuwa ana maambukizi ya virusi vya ukimwi.
“Nilimpompima na kugundua kuwa ana virusi vya ukimwi nilitakiwa kumuanzishia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo, pamoja na kumkinga mtoto aliyetumboni asipate maambukizi ya virusi vya ukimwi, lakini kutona na kuharibika kwa dawa nimeshindwa kumuanzishia hiyo dozi,”alisema Muuguzi Urio.
Aliendelea kuhudhuria kliniki mpaka muda wa kujifungua ulipofika, alijifungulia katika Zahanati ya Matekwe, lakini hata alipokuwa anaumwa uchungu hakupata dawa za ARVs ambazo zinamkinga mtoto asipate maambukizi wakati wa kuzaliwa. Ndio chanzo cha yeye kumuambukiza mtoto wake wan ne mwenye miezi saba virusi vya ukimwi.
Baada ya miezi mitatu kupita toka amejifungua, Zarula alilazimishwa kumpeleka mtoto wake ktika hospitali ya wilaya ya Nachingwea, ili atolewe damu na kupimwa kama mtoto amepata maambukizi au hajapata.
Zarula alikwenda alifanikiwa kupata pesa ya kwenda hospitali ya wilaya kumpima mtoto wake, utaratibu wa kupima watoto wa chini ya miezi 18 ni lazima mtoto anatolewa damu katika kisigino cha mguu kwa sababu umri aliokuwa nao ukimpima kwa kumtoa damu kama unavyowapima watoto wenye miezi 18 na watu wazima, huwezi kugundua kuwa anamaambukiz kwa sababu bado kuna antibody za mama mwili kwa mtoto wa chini ya miezi 18 na hapo mtoto anatakiwa kupimwa antijen zake au DNA.
Aidha damu hiyo ikipatikana inahifadhiwa kwa utaratibu maalumu, kisha kusafirishwa kwenda katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa vipimo vya hali ya juu , ili kugundua kama mtoto wa chini ya miezi 18 amepata maambukizi au hajapata.
Mashine maalumu za kupima maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa watoto wa chini ya miezi 18 hapa nchini, ziko katika kanda nne nazo ni Muhimbili Dar es salaam, Bugando Mwanza, Kcmc Moshi na Mbeya.
Katika mkoa wa Lindi na Mtwara hawana mashine hizo, inabidi damu zote za watoto waliozaliwa na mama wenye maambukizi ya virusi vya ukimwi, inawalazimu kupeleka damu zao katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ni gharama kubwa sana na kila baada ya wiki mbili au tatu wanapeleka damu za watoto hao.
Zarula anaficha kuwaeleza familia yake kwamba anaishi na virusi vya ukimwi, kwa sababu anahofia kutengwa kama alivyotengwa mjomba yake baada ya kusema anaishi na virusi vya ukimwi.
“Naogopa kuwaeleza ndugu zangu kwamba ninaishi na virusi vya ukimwa, wanajaziba sana; wanaweza kunitenga katika familia kama walivyomtenga mjomba, ni mume wangu pekee ndio anafahamu afya yangu kwa sasa,” alisema Zarula.
Mume wake Zarula, hajapima maambukizi ya virusi vya ukimwi toka mwezi Julai mwaka 2011, mkewe akiwa na ujauzito wa miezi sita mpaka sasa mtoto anamiezi saba, mkewe amemshauri kwenda kupima lakini amekataa.
“Mume wangu alikata kupima maambukizi ya virusi vya ukimwi, muuguzi Lidia amejitahidi kumshawishi kupima na kumueleza umuhimu wa kupima maambukizi ya vieusi vya ukimwi lakini amekataa mpaka sasa,” alisema Zarula.
Kwa mujibu wa muuguzi wa zahanati ya Matekwe Lidia alisema kuwa, umuhimu wa kupima maambukizi ya virusi vya ukimwi ni kujua kama umeambukizwa au bado, na kama umeambukizwa utapimwa kujua kinga zako za mwili zipo kwa kiasi gani, kama zimeshuka utaanzishiwa dawa za ARVs, pia ukijua kama unamaambukizi utachukua tahadhari kuwaambukiza wengine ambao hawana maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Athumani ni mzaliwa wa mkoa wa Tanga, lakini kwa sasa anaishi katika kijiji cha Matekwe, anafanyakazi ya uchimbaji madini ya dhahabu na rubi katika machimbo ya mbwemkuru.Katika kipindi cha ujauzito wake, Zarula hakuweza kwenda katika kituo cha afya kilimarondo, kupatiwa dawa za ARVs, kwani nauli ya kwenda huko kutoka Matekwe kwa pikipiki ni zaidi ya shilingi 20,000. Ni zaidi ya kilometa 28, na hakuna usafiri mwengine. Pia hana uhakika kama akienda kituo cha afya cha kilimarondo atafanikiwa kupatiwa ARVs.
Kijiji cha Matekwe kina wakazi 2,548 kati ya hao wajawazito kwa mwaka 2012 walikuwa 84, waliojifungua 33, kati ya hao wenye maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) watatu.
Muuguzi wa Zahanati ya Matekwe Lidia, alikili kuwepo kwa tatizo hilo kwa akinamama hao waliogundulika na maambukizi ya ukimwi (VVU), kushindwa kupewa dawa za ARVs ndio imechangia kuwaambukiza watoto wakati wa kuzaliwa.
Watoto watatu walizaliwa na mama hao, ambao hawakupata dawa za ARVs walivyokuwa wajawazito, watoto wao wote watatu wamepata maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Ulio alisema kuwa toka mwezi Juni 2011kulikuwa hakuna dawa za ARVs katika zahanati ya Matekwe, mpaka Desemba 2011, ndio dawa hizo zililetwa, muda huo wajawazito watatu walikuwa wameshajifungua na watoto walipata maambukizi ya virusi vya ukimwi.
"Dawa nilizonazo za kumkinga mtoto na maambukizi akiwa tumboni kwa mama zilikuwa zimekwisha matumizi yake, sikuweza kuwapatia dawa hizo, zingeweza kumletea madhara yeye na mtoto aliyetumboni, ulipofika muda wa kujifungua basi nikawazalisha hivyo hivyo”alisema Uliyo.
Ulio alitoa ushauri kwa wajawazito hao kwenda katika kituo cha afya kilimarondo kupatiwa dawa za ARVs, lakini walisema hawana pesa ya kukodi pikipiki mpaka katika kituo cha afya.
Zubeda Abasi (23), ni mkazi wa kijiji cha Matekwe, anaishi na virusi vya ukimwi, naye pia ana mtoto wa miezi tisa kwa sasa, alipokuwa mjamzito alihudhulia katika zahanati ya Matekwe lakini, kwa sababu dawa zilikuwa zimekiwsha muda wake katika zahanati hiyo,hakupewa dawa za ARVs, ndio chanzo cha mkumzaa mtoto wake akiwa ameambukizwa virusi vya ukimwi.
"Nilipokuwa na ujauzito wa miezi mitano, nilikwenda kliniki kupima nikaambiwa ninamaambukizi ya virusi vya ukimwi, nilishauriwa kumleta bwana aliyenipa mimba kupima, alikubali alivyopimwa akagundulika hana maambukizi, alinikimbia na kuniacha pekee yangu na mimba mpaka sasa nimejifungua mtoto anamiezi saba," alisema Zubeda.
Hakuweza kwenda katika kituo cha afya cha kilimarondo, kupewa dawa za kumkinga mtoto asipate maambukizi.
Kabla ya kushika mimba, Zubeda alikuwa anafanyakazi ya kunyoa nywele za katika saloon za kiume huko kilwa, amefanya kazi hiyo kwa muda wa miezi nane, akaamua kurudi kwao matekwe.
Zubeda aliporudi Matekwe alipata bwana mwengine, wakaanza mahusiano bila ya kupima, baada ya mwezi mmoja katika mahusiano alishika ujauzito.Baada ya miezi mitano kupita alikwenda zahanati ya matekwe kuanza kliniki, hapo ndipo alipogundulika kuwa anamaambukizi ya virusi vya ukimwi.
"Sikupewa dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huu nikaanza kuumwa na kudhohofu mwili, na pesa sina ya kwenda kituo cha afya cha kilimarondo kuchukua dawa niliendelea kuumwa homa za mara kwa mara mpaka nimejifungua mtoto wangu ambaye naye amepata maambukizi wakati wa kuzaliwa,"alisema Zubeda.
Dk. Daniel Magesa Mkurugenzi msaidizi wa tiba kutoka Pasada alisema kuwa, mjamzito anashauriwa kwenda kliniki mapema na kupima maambukizi ya virusi vya Ukimwi, akigundulika kama anamaambukizi anaazishiwa dawa ya nevirapine ya kumkinga mtoto asipate maambukizi akiwa tumboni.
Kwa mjamzito mwenye (VVU) akiwa na kinga chini ya 350 anatakiwa kutumia dawa ya kumkinga mtoto na maambukizi ijulikanayo kama zidovudine, na anatakiwa kutumia dawa za ARVs. Lakini, kama anakinga za juu zaidi ya 350 akiumwa uchungu anapewa dawa aina ya nevirapine.
Dawa hizo zote zinasaidia kupunguza kasi ya virusi vya ukimwi kuzaliana, na kama virusi vitapunguza kasi ya kuzaliana mjamzito atakuwa na kinga ya hali ya juu zaidi na kuweza kupambana na maradhi nyemelezi pamoja na kujifungua salama na mtoto pia kutopata maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Mkoa wa Lindi Dk. John Sijaona alisema kuwa, upatikanaji wa dawa za ARVs ni changamoto kubwa sana kutokana na bohari ya dawa kuchelewesha madawa hayo, unaweza kuagiza na ukaletewa baada ya miezi miwili hadi mitatu na unaweza ukaletewa dawa ambazo sio unazozihitaji.
"Tatizo ni bohari ya madawa kuchelewesha madawa ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya ukimwi, hayaji kwa muda ule ambao tumeomba, na sio kwa dawa za kupunguza makali ya ukimwi hata vitendanishi vya kupimia maambukizi ya virusi vya ukimwi, ukienda unapewa boxi tano ambazo hazitoshi kulingana na wingi wa watu wanaohitaji upimaji, pia kuletewa dawa ambazo sio ulizoomba" alisema Dk. Sijaona
Kwa mujibu wa Dk. Sijaona alisema kuwa, upatikana duni wa dawa mbalimbali zikiwemo za ARVs, unachangiwa na baadhi ya wahudumu wa afya katika zahanati mbalimbali kukosea kujaza fomu za bohari ya madawa (MSD), fomu hizo zikikosewa hata herufi moja tuu bohari ya madawa wanaiweka pembeni hawatoi dawa, hivyo basi dawa zinakuja pungufu kwa sababu hiyo.
Dk. Sijaona alisema kuwa changamoto nyingine ni wilaya ya Nachingwea kugawanyika mara mbili, kuna kanda a na kanda b, wanaweza kupeleka dawa kanda a kumbe na kanda b nako hakuna dawa.Pia uletaji wa dawa bila ya kushirikisha watendaji wa vijiji na hospitali ya wilaya kwa msd na kulazimishwa kusaini fomu ya madawa bila ya kukagua dawa au kujua kwamba zimefika sehemu husika, hilo nalo ni tatizo sugu kwa msd kanda ya Mtwara.
Dk. Sijaona alisema kuwa mjamzito hawezi kuanza kupewa dawa za kupunguza makali ya virusi vya ukimwi mpaka apimwe, kujua kama ana maambukizi au hana akionekana na maambukizi ndio anaanzishiwa dawa hizo.
Mahitaji ya upamaji yameongezeka kwa wajawazito kuanzia mwaka 2010 walipima wajawazito 4,472. Wanaume walipima maambukizi ya virusi vya ukimwi na wake zao walikwa 1,948.
Dk. Sijaona alisema kuwa, kwa sasa wilaya ina vituo 58 vya kupima maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa kupitia njia ya shawishi, kupitia vituo hivyo idadi kubwa ya watu wanaohitaji huduma hiyo imeongezeka kutoka 1500 kwa mwezi hadi kufikia watu 3000 hadi 4000 wanapima. Nachingwea kuna wakazi 1,95,755.
Asilimia 28 hadi 33 ya wajawazito wanaohudhulia kliniki na kupimwa nchini Afrika Kusini wanamaambuki ya virusi vya ukimwi, mwezi Agosti mwaka 2009 zaidi ya wajawazito 776 kati ya 100,000 walipoteza maisha kwa sababu ya kuwa na kinga za mwili chini ya 200 na kutotumia dawa za ARVs ipasavyo.
Kufuatia hali hiyo nchi hiyo ikaweka mkakati mahususi wa kutumia dawa za ARVs kwa wajawazito mbalimbali, pamoja na kuwaangalia kwa ukaribu jinsi gani ya kupata dawa na matumizi ya dawa hizo pamoja na chakula na wakafanikiwa kuwapatiwa dawa wajawazito 2,000 kutoka katika mradi wa (RHRU)
Pia nchini Kenya maambukizi ya virusi vya ukimwi yameshuka kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kutoka silimia 11 hadi asilimia 4 mwezi mei mwaka 2010, sababu kubwa ya kushuka ni kutumia vituo vya afya kuanzi 17 hadi 26 katika eneo la magharibi mwa nchi hiyo kwenye wilaya ya vijijini kama Ndhiwa. Kwa kuwahamasisha wajawazito wakifika kliniki kupima na kuwapatia dawa za ARVs ili kumkinga mtoto aliyetumboni asipate maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Kwa mujibu wa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Hussein Mwinyi, huduma za kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda mtoto, (PMTCT) zimekuwa zikitolewa nchini tangu mwaka 2000. Hadi kufikia mwezi Desemba 2011 huduma hii imetolewa bila ya malipo katika vituo 4,603 sawa na asilimia 93.
Mwaka 2011 jumla ya wajawazito 86,875 wenye maambukizi ya Virusi vya Ukimwi walipatiwa dawa za ARVs kuzuia maambukizi kwenda kwa mtoto. Hii ni sawa na asilimia 71 ya wajawazito 122,146 waliokadiriwa kuwa na maambukizi ya VVU.
Kwa mujibu wa kitabu cha bajeti cha mwaka 2012/2013, cha wizara ya afya na ustawi wa jamii, kinaeleza kuwa jumla ya shilingi 253,468,765,171.00 pesa hizi zimetengwa kwa ajili ya kununua na kusambaza dawa, vifaa tiba na vitendanishi katika zahanati, vituo vya afya na hospitali za umma. Kati ya fedha hizo shilingi 147,423,200.00 zimetolewa na Global Fund kwa ajili ya kununua na kusambaza dawa za malaria na ukimwi nchini.