Tuesday, April 16, 2013

WAJAWAZITO NA WATOTO MSAKUZI KINONDONI BADO WANAPIMWA CHINI YA MTI MKAMVU

Kutoka katika mti mkavu huo, ambao unatumika kupima watoto wa chini ya miaka mitano na wajawazito kwa miaka miwili, katika eneo la Msakuzi mtaa wa Ruguruni katika kata ya Kwembe wilaya ya Kinondoni. Mpaka kuingia katika jengo ndogo la kliniki lililojengwa kwa ufadhili wa mfuko wa Jimbo la Ubungo.

 Akinamama wakiwa na watoto wao walikuwa wakinyeshewa mvua na kuchomwa na jua kali. Adha hiyo inawapata kwa kufuata huduma ya vipimo mbalimbali, kwa wajawazito na watoto wao katika mti huo mkavu.

Kwa sasa adhabu hiyo itaanza kusahaulika kwa kujengewa jengo ndogo, la vyumba vitatu ambalo litakuwa linatumika kwa upimaji wa watoto na wajawazito.


Lakini sio tu kuwapima bali, hata kujifungua katika jengo hilo ambalo lililojengwa kwa ufadhili wa mfuko wa jimbo. Kwa zaidi ya mwaka mmoja na miezi sita sasa, toka Mbunge wa Jimbo la Ubungo John Mnyika kufungua jengo hilo, mpaka sasa bado halijaanza kutoa huduma bado akimama wanaendelea kutaabika kwa kuendelea kupimwa katika mti huo.


Mganga Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Dk. Gunini Kamba akimkabidhi vifaa mbali mbali vya jengo hilo, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi tawi la Msakuzi Leard Kitunga. 

 Dk. Kamba alisema kuwa, amesikia kilio cha wanawake wa Kwembe juu ya tatizo hilo, la kuwapima wajawazito chini ya mti na watoto kwa muda wa miaka miwili.

"Tumesikia kilio cha wajawazito na mama wenye watoto wadogo, wanaonyeshewa mvua na kuchomwa na jua, kwa kukosa jengo pamoja na vifaa na wahudumu, leo tumewaletea vitanda vitatu, kimoja kwa ajili ya kujifungulia na vitanda viwili vya kawaida, mzani wa kupimia watoto na mzani wa kupimia watu wazima na Makintoshi mita 25 ambayo inatumika kutandikia katika kitanda cha kujifungulia,"alisema Dk. Kamba.

Dk. Kamba alisema kuwa vifaa hivyo walivyowakabidhi siku ya leo katika kituo hicho cha kutoa huduma ya kupima na kujifungua, kitasaidia kutoa huduma ya wajawazito na watoto katika eneo hilo, ambalo akina mama wamekuwa wakitumia gharama kubwa kufuata huduma hiyo katika hospitali ya Mwananyamala, Tumbi Kibaha na Sinza.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wa tawi hilo Kitunga alisema kuwa, wanamshukuru Dk. Kamba kwa kuwasikia kilio chao cha muda mrefu kwa kuwapelekea vifaa hivyo vya msingi, kwa ajili ya upimaji wa wajawazito, kujifungu na upimaji wa watoto.


"Tunamshukuru sana Dk. Kamba kwa kujali na kuguswa na suala la matatizo ya wajawazito na watoto katika eneo hili la Msakuzi, tunamuomba asisahau kutuletea muuguzi na nesi katika kituo hiki ili huduma ianze kwa kuwapunguzia adha wakazi wa Kwembe,"alisema Kitunga.


Rafail Maria mkazi wa eneo hilo alisema kuwa, kuletwa kwa vifaa hivyo katika kituo hicho kidogo cha upimaji, itasaidia kupunguza usumbufu wa kwenda mbali na kunyeshewa na mvua na kuchomwa na jua kwa watoto na wajawazito, wanaofika kila mwisho wa mwezi kupima na kupatiwa chanjo.


Jannet Liytuu (36) ni mama mwenye watoto watatu, kwa sasa anamtoto mwenye miezi nane naye anapima katika mti huo mkavu siku ya kliniki, kwa sababu ya jengo hilo toka limezinduliwa hakuna vifaa wala muuguzi.


"Nimejifungulia katika hospitali ya Mwananyamala, kwa sababu hakuna zahanati wala kituo cha afya katika eneo hili, basi unatakiwa kwenda Mwananyamala maana ukienda hospitali ya Tumbi unarudishwa hata ukiwa unaumwa uchungu wanakataa kukupokea,"alisema Liytuu.


Aidha ukitaka huduma ya wajawazito na watoto inakulazimu kwenda mabwepande na Kibamba ambako, ni lazima uvuke mito miwili ili ufike katika zahanati ya Kibamba kama mto wa Kibwegere na Mdidimu, mito hii ikijaa maji hakupitiki kiurahisi kwa sababu hakuna madajara.


Anastazia Mwakalinga (37) mkazi wa eneo la Msakuzi amajifungua miezi miwili iliyopita katika hospitali Tumbi Kibaha, alipata shida sana kwa sababu alipofika katika hospitali hiyo, akiwa anaumwa uchungu waligoma kumsaidia kujifungua, mpaka alipokwenda katika zahanati mmoja ya wilaya ya Kibaha kumuandikia kwenda kujifungulia hospitali yaTumbi, alipofika Tumbi alijifungua mtoto aliyefariki kwa sababu alichukua muda mwingi kupata karatasi ya maelekezo ya kujifungua hapo.


"Kituo hiki kingekuwa na vifaa na muuguzi ningejifungulia hapa na wala nisingehangaishwa nilipofika katika hospitali ya Tumbi, na wala mtoto wangu asingefikia hatua ya kupoteza maisha kwa kuchelewa kupata huduma ya kujifungua,"alisema Mwakalinga.

Dk. Kamba alisema, Kwa sasa wamepata eneo la heka kumi katika kata ya Kibamba, mtaa wa Hondogo kwa Neema, kwa kujenga kituo kikubwa cha afya ambacho kitatoa huduma kwa wakazi wa kata, Kwembe, Kibamba, Msigani, Mbezi, Kimara na Saranga.

Kwa sasa wako katika fidia ya kuwalipa wakazi wa eneo hilo, malipo ambayo ni zaidi ya shilingi milioni 100, aidha eneo la Msakuzi lina kaya zipatazo 1,000, kaya zote hizo zinategemea kupata huduma ya afya katika kata ya Kibamba na Mabwepande. Gharama za kukodi tax kwenda hospitali ya Mwananyamala ni shilingi 400,000, hospitali ya Sinza ni shilingi 30,000, hospitali ya Tumbi shilingi 20,000.


Uwajibikaji wa aina hii ni kama wa Dk. Kamba, katika kuhakikisha wajawazito na watoto wanapata huduma bora sehemu wanakoishi, ndio unaohitajika kwa watendaji mbalimbali hapa nchini.

Kama tunajali na kuguswa na changamoto mbalimbali zinazohusu masuala ya wajawazito na watoto, vifo vya kizembe haviwezi tena kuendelea  kutokea kwa sababu, kila mmoja anajua wajibu wake na nini cha kufanya ili kuweza kupunguza vifo vya wajawazito hapa nchini.

Lakini Dk. Kamba amejitahidi kupeleka vifa hivyo katika kituo kidogo cha kupima wajawazito na watoto, bado anahitajika muuguzi na nesi kuweza kutoa huduma hiyo kwa walengwa wa eneo la Msakuzi na maeneo jira, usichoke pambana ili uweze kumpata muuguzi na nesi mwenye kiwango cha juu katika kutoa huduma kwa Msakuzi, hiyo ndio kazi uliopewa na Mwenyezi Mungu ya kuwaokoa wajawazito na watoto wa chini ya miaka mitano.

0 comments:

Post a Comment