Ukizungumzia suala la kupanga uzazi katika mkoa wa Mara, ni tatizo kubwa sana hasa kwa wanaume wa mkoa huo, hawataki wake zao na wao wenyewe wanaume wafunge uzazi.
Sababu kubwa ya wanaume wa mkoa wa Mara kukataa kufunga uzazi, ni kutokana na kulipa ng'ombe au mbuzi nyingi kama mahali nyumbani kwa mwanamke anayemtaka kumuowa, kuanzia ng'ombe au mbuzi watano hadi 20.
Mahali hiyo inachangia usugu wa wanaume wengi wa mkoa wa Mara, kukataa wake zao na wao wenyewe kupanga uzazi, kwa sababu ng'ombe au mbuzi alizopeleka kwenu 'zina zaa kwa nini yeye aliyelipa mahali hiyo kubwa kwake usizae', wakati ametumia ghalama kubwa.
Pili Makuli (18) ni mkazi wa kijiji cha Bweri katika wilaya ya Musoma vijijini, ana watoto wawili wote amejifungua kwa kufanyiwa upasuaji, mtoto wa kwanza amejifanyiwa upasuaji mwaka 2011 akiwa na miaka 16 na mwaka huu pia amefanyiwa upasuaji.
Sababu kubwa ya Pili kufanyiwa upasuaji ni nyonga zake hazijakomaa kiuzazi na kushindwa kusukuma vema mtoto, kutokana na umri wake kuwa mdogo sana.
Naabu Giraluma ni muuguzi katika wodi ya akimama wajawazito katika hospitali ya mkoa wa Mara, alisema kuwa pili nyonga zake za uzazi bado hazikomaa kuweza kusukuma vema mtoto kutokana na umri wake umdogo sana, ndio sababu kubwa ya kufanyiwa upasuaji kwa watoto wake wote wawili.
Pili ni mke wa kumi na mmoja kwa mume wake Joseph Thomas (60) ambaye alitoa alitoa ng'ombe 3 na mbuzi 3 kwa mama yake, Pili alishika mimba akiwa darasa la tano katika shule ya msingi ya Nasurula iliyopo katika wilaya ya Musoma Vijijini.
"Mume wangu hataki kufunga uzazi mpaka nikimzalia watoto 10, lakini uzazi wangu ndio unatatizo kila kinifika hapa hospitali nafanyiwa upasuaji, natamani kufunga uzazi lakini nahofia kupigwa na mume wangu akijua kama nimefunga uzazi, maana mke wake wa nane alifunga bila ya kumshirikisha alimpiga mpaka amezimia kwa kufunga uzazi,"alisema Pili.
Pili alirubuniwa kwa kununuliwa chipsi pamoja na nguo nzuri na Joseph mpaka akampa ujauzito akiwa na miaka 16, kwa sababu hiyo hakuweza kuendelea na masomo yake ya shule ya msingi, ndoto zake zimefutika hawezi tena kusoma kwa sababu ameolewa na kulipiwa mahali kubwa.
"Natamani kusoma kwa sasa lakini siwezi tena kwa sababu mume wangu haki kabisa masuala ya mimi kujiendeleza japo nimeshazaa, ndoto zangu za kuwa nesi zimeishia kizani, siwezi tena kuzifikia maana kwa sasa hata kusoma vema sijui na ndio hivi nazaa kila mwaka," alisema Pili
Aidha Pili alisema anampenda mume wake japo ana umri mkubwa ukilinganisha na yeye maana kwa hapo kijijini kwao ndio mwanaume mwenye ng'ombe na mbuzi nyingi kuliko wanaume wengine katika kijiji Bweri alikozaliwa yeye.
Kwa mujibu wa Dk. Ahmed Makuani mtaalamu wa magonjwa ya kike ambaye pia amefanya kazi nchi mbalimbali kufundisha masuala ya uzazi salama kutoka wizara ya afya na ustawi wa jamii alisema kuwa, mjamzito akijifungua kwa upasuaji anatakiwa apumzike kwa muda wa miaka miwili bila ya kushika ujauzito mwengine, hii ina msaidia mama kuboresha afya yake na mtoto aliyemzaa kwa upasuaji.
Tatizo la mama kuzaa mfurulizo tena kwa uzazi wa kufanyiwa upasuaji ni hatari sana, anaweza akapata tatizo la upungufu wa damu, mfuko wa uzazi kupasuka kama hakupata huduma nzuri wakati wa kujifungua, anashauri kupunzika kwa miaka miwili toka amefanyiwa upasuaji hadi mtoto anapomaliza kunyonya.
Dk. Makuani anasema kuwa mjamzito akifanyiwa upasuaji kovu la kidonda linapona kwa muda wa miezi mitatu tu, ila mama anatakiwa kupata nafasi ya kulea mtoto wake vema kwa muda wa mwaka mmoja na miezi sita, pamoja na kuapata chakula bora yeye na mtoto wake ili awe na afya njema itakayo msaidia atakapo amua kushika ujauzito mwengine.
Pili hana uhakika wa kuishi maisha marefu kwa sababu ya uzazi wake wakufanyiwa upasuaji, na mume wake hataki yeye afunge uzazi kwa sababu ya kulipa ng'ombe nyingi kwa wazazi wake.
Kaira Moyo (35) mkazi wa kijiji cha Ifinga wilaya ya Songea mkoa wa Ruvuma ana watoto tisa, anapenda kupanga uzazi wa mpango lakini muwe hataki kabisa swala hilo, nitafanya kwa siri sana mtoto huyu akikuwa.
“Kila mwaka nashika mimba na kuzaa, nimechoka sasa, unaniona nilivyozeeka kwa kuzaa kila mara, hata hamu na ndoa yangu sina, muda mwengi nalea watoto,”alisema Kaira.
Kaira alisema kuwa huduma ya uzazi wa mpango isongezwe karibu vijijini, kama kuweka kitanzi, kufunga mirija ya uzazi, pamoja na kutolewa bure ili kuweza kuwafikia akina mama wengi vijijini wanaohitaji kufunga uzazi.
Nyangeta Makori (38) mkazi wa kijiji cha Nyambono katika wilaya ya Musoma Vijijini, anawatoto sita katika mzao wa tano,anapenda kufunga uzazi lakini mume wake hataki kusikia suala hilo kwa sababu ametoa mahali ya ng'ombe 20 kwao anastahili kushika mimba na kujifungua kama ng'ombe zinavyozaa kwao.
"Natamani kufunga uzazi lakini mume wangu ndio kikwazo kikubwa hataki kufunga uzazi ananiambia ng'ombe alizotoa mahali kwetu zinazaa kwa nini nami nisizae kwake, basi ndio nazaa kila wakati na kwa sasa ndio nimepata watoto wawili mapacha,"alisema Nyangeta.
Juma Hasani (45) na mkewe Salma Shomari (35) wana watoto sita wakazi wa Ajentina katika Kata ya Manzese wilaya ya Kinondoni katika mkoa wa Dar es salaam, yeye na mkewe wamefunga uzazi kwa pamoja katika zahanati ya Tandale.
"Tumeamua kufunga uzazi kwa pamoja mimi na mke wangu kwa sababu mtoto huyu amejifungua kwa kufanyiwa upasuaji kwa kutokana na nyonga zake kushindwa kusukuma vema, kwa sabau hiyo nimeamua kufunga uzazi ili kuwalea vema watoto tuliowapata na kumlinda mke wangu asipoteze maisha kwa uzazi," alisema Juma.
Kwa upande wake John Chikomo mratibu wa afya ya msingi katika jamii manispaa ya Kinondoni mkoa wa Dar es salaam alisema kuwa, mwaka huu jumla ya wanaume saba wamejitokeza na wake zao kufunga uzazi katika vituo vya afya mbalimbali katika wilaya hiyo.
Chikomo alifafanua kuwa hii imetokana na wanaume kuhamasika kwa kupitia njia maalumu ya kushawishi kwa kutumia kikundi maalumu cha kuhamasisha kwa kupita nyumba hadi nyumba kushawishi, akinababa kwenda kliniki na wake zao pamoja na kufunga uzazi na wake zao.
Lakini Veronica Michel (45) mkazi wa kijiji cha Kiegei katika kata ya Kiegei wilaya ya Nachingwea mkoa wa Lindi, ana watoto 14 lakini bado anaendelea kuzaa kwa sababu mume wake hataki yeye afunge uzazi na umri mkubwa alionao.
Hapa nchini kuna njia za kupanga uzazi mbalimbali, kuna za muda mrefu na mfumpi pamoja na njia za asili.
Njia za muda mfupi ni kama vidonge, ambavyo vinakiwango kidogo cha kichochea kimoja au viwili, vichochea hivyo vinafanana na vichochea asili vya mwili wa mwanamke.
Mwanamke anatakiwa kumeza kidonge kimoja kila siku, ili kuzuiya mimba, vidonge hivi pia hurekebisha matatizo wakati wa siku za hedhi.
Njia nyingine ni sindano ambayo ina kichochea kimoja, ambacho kinafanana na kichochea cha asili katika mwili wa mwanamke, sindano hii huchomwa kwenye msuli wa bega au tako la mwanamke kila baada ya miezi mitatu, hutolewa na muhudumu wa afya, mama mjamzito anaruhusiwa kuchoma kwa sababu haipunguzi wingi wa maziwa.
Mpira wa kike na kiume pia unasaidia kupunguza mimba, na kuziya maambukizi ya VVU, kwa mama na baba wakiutumia inavyotakiwa kipindi cha kujamiaana.
Njia ya asili kipindi mama ametoka kujifungua mpaka miezi sita, anakoma kupata hedhi ya mwezi kipindi hiki ni kizuri sana kwa mama na baba kupanga uzazi.
Njia nyingine ya asili ya kupanga uzazi, ni mwanamke kuchunguza mabadiliko ya ute ndani ya uke kwa kutumia kidole chake, kipindi cha ute mzito unaoteleza ni wakati wa rutuba au yai kupevuka.
Kipindi hiki mama na baba, wanaweza kuacha kufanya tendo la ndoa, kwa kuepuka kwa mama kushika mimba nyingine.
Njia za muda mrefu ni kipandikizi, ambacho ni kifaa kidogo cha plastiki mfano kama njiti ya kibiriti, ina kichocheo kinachofanana na mwili wa mwanamke, kipandikizi hiki hutumika kuzuiya mimba kwa mwanamke kwa muda wa miaka miwili hadi mitano.
Lupu ni kifaa kidogo cha plastiki chenye madini ya shaba, huwekwa kwenye mji wa mimba ili kuzuiya ujauzito, njia hii hutolewa na muhudumu wa afya na inadumu kwa muda wa miaka 12, pale mama anataka kuzaa basi hutolewa.
Kufunga uzazi kwa mwanamke ni njia ya kudumu ya uzazi wa mpango, inayofanywa na mtaalamu wa afya, kwa kufunga na kukata mirija ya uzazi ya mwanamke.
Njia hii hufanywa kwa hiyari na wale walioridhiana idadi ya watoto walionao, kwa kawaida hufungaji huu hufanywa kwa muda mfupi tuu, mwanamke hatohitaji kulazwa hospitali.
Kutumia njia hii hakutoathiri hamu ya kujamiiana, mwanamke ataendelea kupata siku za hedhi kama kawaida.
Kufunga uzazi kwa mwanaume pia ni njia nzuri ya uzazi wa mpango, mwanaume atakwatwa mirija ya uzazi , baada ya makubaliano ya wawili kwa idadi ya watoto walionao, njia hii haitoathiri hamu ya kujamiiana wala kupunguza nguvu za kiume.
Mratibu wa uzazi wa mpango Taifa Maurice Hiza ,alisema kuwa ni asilimia 27.4 ya watanzania ndio wanaotumia uzazi wa mpango, kwa mujibu ya sensa ya mwaka 2012 Tanzania inaidadi wa watu milioni 45.
Lengo la kuanzishwa uzazi wa mpago ni kupunguza vifo vya mama wajawazito, kuwa na maisha bora kwa mama na watoto anaowazaa, mpaka kufikia mwaka 2015 asilimia 60 ya wanawake na wanaume wajue na kutumia uzazi wa mpango.
Mikoa ambayo iko nyuma katika matumizi ya uzazi wa mpango ni kama Mara asilimia 10, Mwanza asilimia 12, Shinyanga asilimia 13, Kigoma asilimia 14 na Tabora asilimia 19.
Mikoa ambayo imefanya vizuri ni kama Kilimanjaro asilimia 50, Morogoro asilimia 40, Ruvuma asilimia 43, Tanga asilimia 41, Dar es salaam asilimia 34.8, na asilimia 25 ya wanawake kote nchi hawatumii njia yoyote ya uzazi wa mpango.
Changamoto wanazokabiliana nazo katika uzazi wa mpango, ni ungezeko la idadi ya watu, kiwango kikubwa cha uzazi, kiwango kidogo cha matumizi ya kisasa ya uzazi wa mpango.
Changamoto zingine ni mila potofu, upungufu wa dawa na vifaa mbalimbali vya uzazi wa mpango, wanaume kutowaruhusu wake zao kutumia njia za uzazi wa mpango pamoja na elimu ndogo juu ya matumizi ya dawa navipandikizi mbalimbali.
Katika sera ya taifa ya uzazi wa mpango ya mwaka 1994, uzazi wa mpango ni haki ya kimsingi kwa kila mtu bila ya kujali umri, ameolewa au ameowa au amezaa au hajazaa.
Aidha sera hiyo inasema kuwa vijana wote wanahaki ya kupata taalifa, elimu ushauri nasaha juu ya uzazi wa mpango, vijana ambao wanakiri kwamba wanajamiiana, wanahaki ya kupewa njia za uzazi wa mpango wanazopendelea zinazowafaa baada ya kupata ushauri nasaha.
0 comments:
Post a Comment