Mama

Nani kama Mama .

Afya ya Mimba

Mwanamke anayetaka kubeba mimba anashauriwa aache kunywa pombe na kuvuta sigara.

Mama na Mtoto

Mazingira mazuri ya Afya ni Moja ya njia ya kuepuka matatizo ya mama wakati wa kujifungua.

Tuwalinde watoto

watoto 200 kati ya 100,000 wanapoteza maisha wakati wa kuzaliwa na baada ya kuzaliwa, idadi hii ya vifo ni kubwa sana hapa nchini Tanzania.

Karibu kwenye blog hii kwa Habari za Afya ya Mama na Mtoto.

Kufikia mwaka 2010, takwimu zilikuwa zinaonesha kwamba kila wanawake 454 katika vizazi hai 100,000 walikuwa wanapoteza maisha wakati wa ujauzito au kujifungua kwa matatizo mbalimbali ya uzazi.

watoto 200 kati ya 100,000 wanapoteza maisha wakati wa kuzaliwa na baada ya kuzaliwa, idadi hii ya vifo ni kubwa sana hapa nchini Tanzania..

Sunday, April 14, 2013

UKOSEFU WA VIPIMO VYA KASWENDE NA GONOREA KWA WAJAWAZITO KATIKA HOSPITALI YA SINZA KUNACHANGIA KUZALIWA WATOTO WALIO FARIKI KWA KUAMBUKIZWA MAGONJWA HAYO WAKIWA TUMBONI

"Leo nimeanza kuhudhuria kliniki katika Hospitali ya Sinza kwa mara ya kwanza. Nimefika hapa nimetoa historia ya muhimu kuhusu ujauzito wangu, nikapelekwa kwenye vipimo na nimepimwa kujua kama nina maambukizi ya UKIMWI. Hata hivyo kuna baadhi ya vipimo sikupimwa. Vipimo hivyo ni pamoja na kipimo cha wingi wa damu (HB test), maambukizi ya kaswende na gonorea (VDRL test) na mfumo wa mkojo. Nimeambiwa kuwa vipimo hivyo havipo hospitalini, hivyo natakiwa nikatafute huduma hii kwenye hospitali zingine  hususani za binafsi," alisema Mwanahawa Mohamed (25) mkazi wa Sinza Madukani.
 Mwanahawa alipomaliza kipimo cha maambukizi ya virusi vya UKIMWI, aliamua kurudi nyumbani kujitayarisha ili kesho yake aende kupima vipimo alivyovikosa kuvipata Hospitali ya Sinza.

Gharama za vipimo katika hospitali za binafsi kama kipimo cha wingi wa damu (HB test) shilingi 3,000, kipimo cha maambukizi ya kaswende na gonorea (VDRL test) shilingi 5,000 pamoja na kipimo cha kutambua kama mkojo mchafu shilingi 3,000.


Tatizo la ukosefu wa vipimo muhimu kwa akina mama wajawazito katika Hospitali ya Sinza ni la muda mrefu sana zaidi ya miezi sita toka mwezi Oktoba  mwaka 2012. Toka kipindi hicho kumekuwa na upungufu wa vipimo vya kuangalia magonjwa ya kaswende, maambukizi katika mfumo wa mkojo, kisonono na kujua wingi wa damu.


Mratibu wa Afya ya Mama na Mtoto katika hospitali hiyo Milka Maganga alisema kuwa, tatizo la ukosefu wa vipimo vya wingi wa damu, maambukizi ya kaswende, kisonono na maaumbukizi katika mfumo wa mkojo  kwa wajawazito katika hospitali ya Sinza ni la muda mrefu.
Maganga alisema kuwa vipimo hivyo ni muhimu sana kwa akina mama wajawazito wakati wa mahudhurio ya kliniki kwa mara ya kwanza na katika marudio.

Aidha alisema kuwa wajawazito wanashauriwa kutumia na kupewa dawa za kuongeza damu na kupewa ushauri juu ya matumizi ya chakula bora, bado anatakiwa kuchukualiwa kipimo cha wingi wa damu kila anapohudhulia kliniki, ili kujua kama  damu aliyonayo inatosha au anahitaji tiba ya kuufanya mwili wake utengeneza damu zaidi. 


Pia alifafanua kuwa, tutahitaji kujua kama mkojo hauna shida kila mara afikapo kliniki. Huduma zote hizi zinachangia kwa mjamzito kujifungua salama na kuwa na mtoto mwenye afya nzuri.


Maganga alisema kuwa, kuna kipindi wanazaliwa watoto wakiwa na maambukizi ya magonjwa ya zinaa, kwa sababu mjamzito alishindwa kupata huduma hizi muhimu kipindi alichokuwa anahudhulia kliniki, kwa sababu vituo vya afya vya binafsi ambako tunamshauri kwenda kupima kuna huduma za kulipia. Na wajawazito wengi wanashindwa kwenda katika vituo hivyo, kwa sababu ya gharama za vipimo hivyo kuwa ni kubwa ukilinganisha na hapa katika hospitali ya sinza tunatoa bure.


Kwa mujibu wa Maganga alisema kuwa, mwaka jana jumla ya wajawazito 24 walioshindwa kwenda katika vituo vya afya vya binafsi kupima maambukizi ya kasendwe na kisonono, walijufungua watoto walikuwa na maambukizi ya magonjwa hayo na watoto wote walikuwa wamefariki kwa kuugua magonjwa hayo wakiwa tumboni.


Katika Hospitali ya Sinza kwa siku hupokea wajawazito wapya wanaoanza kuhudhuria kliniki wapatao 20. 


Kwa upande mwingine wajawazito wa marudio ya kliniki kwa siku hufikia kiwango cha 90 hadi 100. Lakini kwa upande wa zanati ya Tandale wanaohudhuri kwa mwezi Febuari ni 347. Idadi hii ni kubwa ukilinganisha na upatikanaji wa vipimo mbalimbali vinavyohitajika wakati wa ujauzito.

Maganga alisema kuwa, pamoja na wingi huu wa wateja, katika mwanzo wa mwezi tunapewa kikopo kimoja cha vipimo vya wingi wa damu na ndani ya kikopo hicho kunakuwa na vipimo 100 tu. Kikopo hiki kinatakiwa kitumike kwa mwezi mmoja! Hali hii ndivyo ilivyo kwa vipimo vya kaswende,kisonono, damu na mkojo.



Kwa upande wake Mganga Mkuu wa hospitali hiyo Dk. Benedict Luoga alisema kuwa, sio vipimo tu kwa wajawazito wakihudhulia kiliniki, pia kuna uhaba wa upatikanaji wa damu salama kwa wajawazito mbalimbali wanaohitaji huduma hiyo kwa hapa hospitali ya sinza ni tatizo kubwa sana. Mwaka jana zaidi ya wajawazito 120 walifika katika hospitali hii wakiwa na tatizo la upungufu wa damu, na kwa mwezi zaidi ya wajawazito 10 wanahitaji damu.

Mjamzito anaweza kuingia katika chumba cha kujifungulia akiwa na upungufu wa damu na anahitaji kuongezewa damu ili aweze kujifungua salama, kama hukuweza kumuongezea damu basi utakuwa unahatarisha maisha  yake, kitendo cha kumuongezea damu ni muhimu sana kwa lengo la kuokoa maisha yake wakati wa kujifungua.

Mahitaji ya damu salama kwa siku katika chumba cha kujifungulia wajawazito mbalimbali katika hospitali hiyo ni chupa kumi za damu, lakini kuna kipindi wanakosa hizo chupa kumi na kulazimika kuomba katika hospitali ya mkoa mwananyamala.


Aidha alisema kuwa kama kutakuwa na wajawazito ambao wengi wana damu ya kutosha, basi chupa kumi zinatumika kwa muda wa siku tatu, kisha wanakwenda tena benki ya damu katika hospitali ya Taifa muhimbili wakiwa na damu ya kutoa ili waweze kupata damu nyengine.


 "Wajawazito wengi wanafika katika chumba cha kujifungulia wakiwa na damu ya units saba, ambayo haitoshi kumsaidia kujifungua salama tunalazimika kumuongezea damu kuanzia units mbili hadi tatu ili aweze kujifungua salama," alisema Luoga.


Mwaka jana tarehe 14 mwezi wa Disemba ilikuwa ni historia kwa kituo hiki. Mheshimiwa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alifungua jengo la Kituo cha Afya Sinza, na kukipa hadhi kuwa Hospitali ya Wilaya ya Kinondoni. 


Mabadiliko hayo yalileta matumaini makubwa ya kuboresha huduma za hospitali ikizingatiwa kuwa mabadiliko haya yana maana ya kuongezewa bajeti. Tofauti na mategemeo yaliyokuweko, mabadiliko hayo hayakuenda sambamba na ongezeko la bajeti toka Serikali Kuu pamoja na kupandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Wilaya ya Kinondoni.


"Toka Rais Kikwete afungue jengo la wazazi idadi ya wajawazito imeongezeka mara dufu kutoka 20 kwa siku wanaohitaji huduma ya kujifungua mpaka kufia 50 hadi kufikia 70, hawa wanajifungua kwa njia ya kawaida,"alisema Luoga


Lakini kwa wale wanaofanyiwa upasuaji kwa siku wanafanyiwa watano hadi 10 kulingana na idadi ya vitanda viko 11 tu, hivyo inalazimika kusubiri muda wa siku tatu ili kidonda cha upasuaji kipone kisha ndio anaruhusiwa na kuweza kuwafanyia upasuaji wajawazito wengine. Kwa mwezi wanapokea wajawazito wanaohitaji huduma ya upasuaji kuanzi 87 hadi 100. Pia ongezeko la wahitaji huduma haliendi sambamba na watumishi, dawa na vifaa tiba kwa sasa.


"Kuna wauguzi na manesi 18 tu katika jengo la wazazi,waliokuwa na stashahada 9 na wenye cheti 9, wanatoa huduma kwa zamu asubuhi wanaingia wauguzi na manesi watano, mchana wanaingiza watatu na usiku wanakuwa watatu hawatoshi ukilinganisha na wajawazito wanaofika kwa siku," alisema Luoga.


Tatizo la uhaba wa dawa na vifaa tiba lipo pia katika zahanati ya Tandale, ambako kuna idadi kubwa ya wajazito wanaofika kuhitaji huduma ya vipimo kwa siku wanapokea wajawazito 50 na kwa mwezi wanapokea wanawazito 300 hadi 320.


"Khafsa Shabani (32) mkazi wa Manzese ni uzazi wake wa nne anasema kwa masikitiko, nimefika toka saa 3:00 asubuhi siku ya kwanza kuanza kliniki ndio namaliza muda huu wa saa 6:30 mchana. 

 Nimepimwa urefu wangu, uzito na urefu wa mtoto alietumboni na  hatimae nimepimwa maambukizi ya virusi vya ukimwi, lakini vipimo vya wingi wa damu, kaswende, kisonono na mkojo sijapimwa nimeambiwa vipimo hivyo vimeisha na ninatakiwa kwenda kupima katika hospitali za binafsi." alisema Khafsa.
Kwa upande wake Mratibu wa afya ya mama na mtoto wilaya ya Kinondoni Mary Massay alisema kuwa, tatizo la wajawazito kukosa vipimo muhimu wanahudhuria kliniki mbalimbali, ni tatizo kubwa katika vituo vingi vya afya kunakuwa na idadi kubwa wa wajawazito ukilinganisha na vipimo hivyo.
Massay alisema kuwa sio tu vipimo kukosekana, bali hata kadi za kliniki kwa wajawazito na watoto wadogo nalo ni tatizo sugu kwa sasa, mpaka kunakipindi ofisi ya mganga mkuu inachapisha kadi 10,000 kila mwaka ili kuweza kuziba pengo la upungufu wa kadi za kliniki kwa wajawazito na watoto wadogo.


Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Dk. Gunini Kamba alisema kuwa, kuna tatizo la upatikani wa vipimo hivyo vya (VDRL test)
na (HB test) katika hospitali ya sinza kwa sababu ya wateja kuwa wengi tofauti na dawa na vifaa tiba.
Dk. Kamba alisema kuwa, kwa sasa wanatumia njia ya kupima (HB test) kwa kutumia Hamemoque machine ambayo inagharama kubwa sana kununua ni shilingi 900,000 na vipimo vyake katika kopo moja vinakuwa 50 hadi 100. kwa kununua duka la kawaida kwa kikopo ni shilingi 89,000. 

Kwa  kutumia utaratibu wa manunuzi kwa kikopo kimoja cha (HB test) kinauzwa kati ya shilingi135,000 hadi 15,0000 kwa kikopo, lakini kupitia bohari ya madawa wananunua kwa kikopo kimoja ni shilingi 75,500.

Dk. Kamba alisema kuwa, ufumbuzi wa tatizo hilo unafanyiwa kazi itakapopatikana mashine aina ya (Tallquist Method) kutoka nchini German ambayo inauzwa kwa gharama nafuu sana na kikopo kimoja kilichokuwa na vipimo vya (HB test) kinauzwa kuanzi shilingi 45,000 hadi shilingi 50,000. Ila kwa sasa vipimo hivi havipatikani bohari ya madawa (MSD)
 
Aidha kwa upande wa vipimo vya (VDRL) wapo katika mchakato wa kufanya manunuzi, ukikamilika basi watakuwa na vipimo hivyo vya kutosha na wajawazito watakuwa na fulsa ya kupima kila anapopangiwa kuhudhulia kliniki.

Aidha alisema kuwa idadi ya wajawazito imeongezeka kuanzia mwaka jana, kutoka 4,23 wajawazito waliopima mwaka 2011, hadi kufikia 6,908 mwa ka 2012 kuanzia mwezi January hadi Novembar, waliojifungua kwa kufanyiwa upasuaji walikuwa 7,22.

Kwa mwaka huu matarajio yao kuwazalisha akina wajawazito  100,000 katika hospitali ya Sinza pekee, wajawazito hao ambao wanatarajiwa kuhudhuria kliniki mara tatu kwa kila mjamzito, kwa hivyo basi tunatakiwa kuwa na boxi 600 za vipimo vya damu, sawa na shilingi milini 53,4000 kwa mwaka.

Dk. Kamba alisema kuwa, kwa sasa wilaya ya Kinondoni kwa upande wa zahanati, vituo vya afya na hospitali, wanapewa  bajeti ya Serikali Kuu katika wilaya ya Kinondoni ni shilingi 766,438,000 na wafadhili wamechangia shilingi 2,480,746,600. 

Aidha Dk. Kamba alifafanua kuwa, Fedha hii hugawanywa katika zahanati, vituo vya afya, hospitali na ofisi ya mganga mkuu wa wilaya kwa kuzingatia asilimia iliyowekwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Dk. Kamba alifafanua kuhusu mgawanyo wa fedha hizo alisema, Ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya hupata asilimia 15 hadi 20, hospitali ya wilaya asilimia 25 hadi 30, vituo vya afya asilimia 15 hadi 20, zahanati asilimia 20 hadi 25 na jamii ni asilimia 2 hadi 5.


Kiasi hicho cha pesa hakikidhi mahitaji halisi ya wagonjwa wanaostahili kupatiwa huduma kwa siku na mwezi katika vituo vya afya mbalimbali katika wilaya ya Kinondoni. 


Akionyesha kuwa kunahitaji mtazamo mpya, Dk. Kamba aliiomba  Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kubadilisha utoaji wa pesa za bajeti katika wilaya mbalimbali na wanatakiwa kupanga bajeti kulingana na idadi ya watu wanaohitaji kupatiwa huduma za afya.

Kwa kutumia kigezo hicho suala la upungufu wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya mbalimbali hapa nchini, vitakuwa havipati changamoto ya kukosa dawa za muhimu hasa kwa watoto wa chini ya miaka mitano na wajawazito.


Kwa mfano takwimu zinaonyesha kuwa mwaka jana Zaidi ya wajawazito 40,000 walikadiliwa kujifungua katika wilaya ya Kinondoni kwa mwaka jana, lakini kati ya hao wajawazito 31,000 walijifungua katika vituo vya afya mbalimbali katika wilaya hiyo.


Kwa upande wa wilaya ya Ilala na Temeke nako hali itakuwa inafanana na ya wilaya ya Kinondoni, wajawazito ni wengi lakini kutakuwa na upungufu wa madawa na vifaa tiba. 


Tatizo hili limelikuta katika wilaya ya Nachingwea mkoa wa Lindi, idadi ni kubwa ya wajawazito lakini wanakosa huduma bora ya kujifungua salama kwa sababu ya ufinyu wa bajeti. 


Pia katika wilaya ya Songea mkoa wa Ruvuma hali sio nzuri katika upatikanaji wa huduma za kliniki, katika zahanati Ifinga kwenye kijiji cha Ifinga wajawazito wanachingia huduma mbalimbali za kliniki, kupima ujauzito unalipia shilingi 2,000, kupima wingi wa damu unalipa shilingi 15,00, kama damu yako pungufu kupewa dawa za kuongeza damu unalipa shilingi 1,000.


Sera ya Afya ya mwaka 2007 inasema wajawazito wanatakiwa kutibiwa bure, lakini utimizaji wa  sera hii una changamoto nyingi zikiwamo ukosefu wa vitendea kazi mbalimbali na dawa. Changamoto zote hizi zinafanya utekelezaji wa Sera hii kuwa mgumu sana.


Hali kadhalika katika Wilaya ya Bunda, Butiama na Musoma Mjini katika mkoa wa Mara, wajawazito wanapokwenda kliniki wanachangia huduma za upimaji kama kupima wingi wa damu wanalipia shilingi 1,000, kadi la kliniki wananunua shilingi 1,000.


Hivi ni lini hasa wajawazito hapa nchini watapata huduma bora za kliniki, tena bila ya kuchangia chochote kile! nani anastahili kuwajibika katika hili ni watoa huduma katika vituo vya afya mbalimbali hapa nchini! au uwongozi wa wilaya unaosimamia utoaji wa huduma za afya kwa jamii!


Kila mtu anatakiwa kujua wajibu wake sehemu ya kazi ili kuhakikisha huduma ya upimaji kwa mjamzito inakuwa bora na ya uhakika, maana akipatiwa huduma bora itasaidia kujua mjamzito kama ana tatizo kama la kupungukiwa damu, mtoto amekaa vibaya, mtoto mkubwa, mama ana maambukizi ya magonjwa ya kuambukiza.


Hii itasaidia kumsaidia mjamzito wakati wa kujifungua mtoto asiye kuwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi kama ilivyokuwa katika kijiji cha Matekwe kata ya Kilimarondo wilaya ya Nachingwea, wajawazito wamewaambukiza watoto zao kwa kukosa dawa za ARV, pia itapunguza vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua na baada. 

Wednesday, April 10, 2013

TRANSFOMA LAZUA KIZAAZAA KARIAKOO JIONI YA LEO

Transfoma ya umeme imezua kizaazaa Kariakoo majira ya saa 17:15 jioni katika mtaa wa Kongo na Muhonda baada ya Transfoma hiyo kuripuka moto na kuanza kutoa moshi mzito uliopelekea baadhi ya wafanyabiashara wa maduka katika mtaa huo kufunga maduka yao kwa kuhofia wizi na kuripuka kwa moto mkubwa katika eneo hilo. 

Transfoma hiyo imekuwa ikiripuka moto na kutoa moshi mzito mara kwa mara na kuleta hofu kwa wafanyabiashara wanaofanya biashara katika eneo hilo na wapita njia, Aidha wafanyabiashara katika eneo hilo wanaiomba Tanesco kuwabadilishia Transfoma hiyo ili kuepukana na madhara makubwa ya moto utakaosababishwa na Transfoma hiyo.

Tuesday, April 9, 2013

NG'OMBE ZANGU NILIZOLIPA MAHALI KWENU ZINAZAA KWA NINI WEWE KWANGU USIZAE

Ukizungumzia suala la kupanga uzazi katika mkoa wa Mara, ni tatizo kubwa sana hasa kwa wanaume wa mkoa huo, hawataki wake zao na wao wenyewe wanaume wafunge uzazi.

Sababu kubwa ya wanaume wa mkoa wa Mara kukataa kufunga uzazi, ni kutokana na kulipa ng'ombe au mbuzi nyingi kama mahali nyumbani kwa mwanamke anayemtaka kumuowa, kuanzia ng'ombe au mbuzi watano hadi 20.


Mahali hiyo inachangia usugu wa wanaume wengi wa mkoa wa Mara, kukataa wake zao na wao wenyewe kupanga uzazi, kwa sababu ng'ombe au mbuzi alizopeleka kwenu 'zina zaa kwa nini yeye aliyelipa mahali hiyo kubwa kwake usizae', wakati ametumia ghalama kubwa.


Pili Makuli (18) ni mkazi wa kijiji cha Bweri katika wilaya ya Musoma vijijini, ana watoto wawili wote amejifungua kwa kufanyiwa upasuaji, mtoto wa kwanza amejifanyiwa upasuaji mwaka 2011 akiwa na miaka 16 na mwaka huu pia amefanyiwa upasuaji.


Sababu kubwa ya Pili kufanyiwa upasuaji ni nyonga zake hazijakomaa kiuzazi na kushindwa kusukuma vema mtoto, kutokana na umri wake kuwa mdogo sana.


Naabu Giraluma ni muuguzi katika wodi ya akimama wajawazito katika hospitali ya mkoa wa Mara, alisema kuwa pili nyonga zake za uzazi bado hazikomaa kuweza kusukuma vema mtoto kutokana na umri wake umdogo sana, ndio sababu kubwa ya kufanyiwa upasuaji kwa watoto wake wote wawili.


Pili ni mke wa kumi na mmoja kwa mume wake Joseph Thomas (60) ambaye alitoa alitoa ng'ombe 3 na mbuzi 3 kwa mama yake, Pili alishika mimba akiwa darasa la tano katika shule ya msingi ya Nasurula iliyopo katika wilaya ya Musoma Vijijini.



 "Mume wangu hataki kufunga uzazi mpaka nikimzalia watoto 10, lakini uzazi wangu ndio unatatizo kila kinifika hapa hospitali nafanyiwa upasuaji, natamani kufunga uzazi lakini nahofia kupigwa na mume wangu akijua kama nimefunga uzazi, maana mke wake wa nane alifunga bila ya kumshirikisha alimpiga mpaka amezimia kwa kufunga uzazi,"alisema Pili.


Pili alirubuniwa kwa kununuliwa chipsi pamoja na nguo nzuri na Joseph mpaka akampa ujauzito akiwa na miaka 16, kwa sababu hiyo hakuweza kuendelea na masomo yake ya shule ya msingi, ndoto zake zimefutika hawezi tena kusoma kwa sababu ameolewa na kulipiwa mahali kubwa.

"Natamani kusoma kwa sasa lakini siwezi tena kwa sababu mume wangu haki kabisa masuala ya mimi kujiendeleza japo nimeshazaa, ndoto zangu za kuwa nesi zimeishia kizani, siwezi tena kuzifikia maana kwa sasa hata kusoma vema sijui na ndio hivi nazaa kila mwaka," alisema Pili

Aidha Pili alisema anampenda mume wake japo ana umri mkubwa ukilinganisha na yeye maana kwa hapo kijijini kwao ndio mwanaume mwenye ng'ombe na mbuzi nyingi kuliko wanaume wengine katika kijiji Bweri alikozaliwa yeye.
 
Kwa mujibu wa Dk. Ahmed Makuani mtaalamu wa magonjwa ya kike ambaye pia amefanya kazi nchi mbalimbali kufundisha masuala ya uzazi salama kutoka wizara ya afya na ustawi wa jamii alisema kuwa, mjamzito akijifungua kwa upasuaji anatakiwa apumzike kwa muda wa miaka miwili bila ya kushika ujauzito mwengine, hii ina msaidia mama kuboresha afya yake na mtoto aliyemzaa kwa upasuaji.


Tatizo la mama kuzaa mfurulizo tena kwa uzazi wa kufanyiwa upasuaji ni hatari sana, anaweza akapata tatizo la upungufu wa damu, mfuko wa uzazi kupasuka kama hakupata huduma nzuri wakati wa kujifungua, anashauri kupunzika kwa miaka miwili toka amefanyiwa upasuaji hadi mtoto anapomaliza kunyonya.


Dk. Makuani anasema kuwa mjamzito akifanyiwa upasuaji kovu la kidonda linapona kwa muda wa miezi mitatu tu, ila mama anatakiwa kupata nafasi ya kulea mtoto wake vema kwa muda wa mwaka mmoja na miezi sita, pamoja na kuapata chakula bora yeye na mtoto wake ili awe na afya njema itakayo msaidia atakapo amua kushika ujauzito mwengine.


Pili hana uhakika wa kuishi maisha marefu kwa sababu ya uzazi wake wakufanyiwa upasuaji, na mume wake hataki yeye afunge uzazi kwa sababu ya kulipa ng'ombe nyingi kwa wazazi wake. 


Kaira Moyo (35) mkazi wa kijiji cha Ifinga wilaya ya Songea mkoa wa Ruvuma ana watoto tisa, anapenda kupanga uzazi wa mpango lakini muwe hataki kabisa swala hilo, nitafanya kwa siri sana mtoto huyu akikuwa. 

 “Kila mwaka nashika mimba na kuzaa, nimechoka sasa, unaniona nilivyozeeka kwa kuzaa kila mara, hata hamu na ndoa yangu sina, muda mwengi nalea watoto,”alisema Kaira.

Kaira alisema kuwa huduma ya uzazi wa mpango isongezwe karibu vijijini, kama kuweka kitanzi, kufunga mirija ya uzazi,  pamoja na kutolewa bure ili kuweza kuwafikia akina mama wengi vijijini wanaohitaji kufunga uzazi.


Nyangeta Makori (38) mkazi wa kijiji cha Nyambono katika wilaya ya Musoma Vijijini, anawatoto sita katika mzao wa tano,anapenda kufunga uzazi lakini mume wake hataki kusikia suala hilo kwa sababu ametoa mahali ya ng'ombe 20 kwao anastahili kushika mimba na kujifungua kama ng'ombe zinavyozaa kwao.

"Natamani kufunga uzazi lakini mume wangu ndio kikwazo kikubwa hataki kufunga uzazi ananiambia ng'ombe alizotoa mahali kwetu zinazaa kwa nini nami nisizae kwake, basi ndio nazaa kila wakati na kwa sasa ndio nimepata watoto wawili mapacha,"alisema Nyangeta.


Juma Hasani (45) na mkewe Salma Shomari (35) wana watoto sita wakazi wa Ajentina katika Kata ya Manzese wilaya ya Kinondoni katika mkoa wa Dar es salaam, yeye na mkewe wamefunga uzazi kwa pamoja katika zahanati ya Tandale.
"Tumeamua kufunga uzazi kwa pamoja mimi na mke wangu kwa sababu mtoto huyu amejifungua kwa kufanyiwa upasuaji kwa kutokana na nyonga zake kushindwa kusukuma vema,  kwa sabau hiyo nimeamua kufunga uzazi ili kuwalea vema watoto tuliowapata na kumlinda mke wangu asipoteze maisha kwa uzazi," alisema Juma.

Kwa upande wake John Chikomo mratibu wa afya ya msingi katika jamii manispaa ya Kinondoni mkoa wa Dar es salaam alisema kuwa, mwaka huu jumla ya wanaume saba wamejitokeza na wake zao kufunga uzazi katika vituo vya afya mbalimbali katika wilaya hiyo.




Chikomo alifafanua kuwa hii imetokana na wanaume kuhamasika kwa kupitia njia maalumu ya kushawishi  kwa kutumia kikundi maalumu cha kuhamasisha kwa kupita nyumba hadi nyumba kushawishi, akinababa kwenda kliniki na wake zao pamoja na kufunga uzazi na wake zao.

Lakini Veronica Michel (45) mkazi wa kijiji cha Kiegei katika kata ya Kiegei wilaya ya Nachingwea mkoa wa Lindi, ana watoto 14 lakini bado anaendelea kuzaa kwa sababu mume wake hataki yeye afunge uzazi na umri mkubwa alionao.

Hapa nchini kuna njia za kupanga uzazi mbalimbali, kuna za muda mrefu na mfumpi pamoja na njia za asili.

Njia za muda mfupi ni kama vidonge, ambavyo vinakiwango kidogo cha kichochea kimoja au viwili, vichochea hivyo vinafanana na vichochea asili vya mwili wa mwanamke.


Mwanamke anatakiwa kumeza kidonge kimoja  kila siku, ili kuzuiya mimba, vidonge hivi pia hurekebisha matatizo wakati wa siku za hedhi.


Njia nyingine ni sindano ambayo ina kichochea kimoja,  ambacho kinafanana na kichochea cha asili katika mwili wa mwanamke, sindano hii huchomwa kwenye msuli wa bega au tako la mwanamke kila baada ya miezi mitatu, hutolewa na muhudumu wa afya, mama mjamzito anaruhusiwa kuchoma kwa sababu haipunguzi wingi wa maziwa.


Mpira wa kike na kiume pia unasaidia kupunguza mimba, na kuziya maambukizi ya VVU, kwa mama na baba wakiutumia inavyotakiwa kipindi cha kujamiaana.


Njia ya asili kipindi mama ametoka kujifungua mpaka miezi sita, anakoma kupata hedhi ya mwezi kipindi hiki ni kizuri sana kwa mama na baba kupanga uzazi.


Njia nyingine ya asili ya kupanga uzazi, ni mwanamke kuchunguza mabadiliko ya ute ndani ya uke kwa kutumia kidole chake, kipindi cha ute mzito unaoteleza ni wakati wa rutuba au yai  kupevuka.


Kipindi hiki mama na baba, wanaweza kuacha kufanya tendo la ndoa, kwa kuepuka kwa mama kushika mimba nyingine. 


Njia za muda mrefu ni kipandikizi, ambacho ni kifaa kidogo cha plastiki mfano kama njiti ya kibiriti, ina kichocheo kinachofanana na mwili wa mwanamke, kipandikizi hiki hutumika kuzuiya mimba kwa mwanamke kwa muda wa miaka miwili hadi mitano.


Lupu ni kifaa kidogo cha plastiki chenye madini ya shaba, huwekwa kwenye mji wa mimba ili kuzuiya ujauzito, njia hii hutolewa na muhudumu wa afya na inadumu kwa muda wa miaka 12, pale mama anataka kuzaa basi hutolewa.


Kufunga uzazi kwa mwanamke ni njia ya kudumu ya uzazi wa mpango, inayofanywa na mtaalamu wa afya, kwa kufunga na kukata mirija ya uzazi ya mwanamke.


Njia hii hufanywa kwa hiyari  na wale walioridhiana idadi ya watoto walionao, kwa kawaida hufungaji huu hufanywa kwa muda mfupi tuu, mwanamke hatohitaji kulazwa hospitali.


Kutumia njia hii hakutoathiri hamu ya kujamiiana, mwanamke ataendelea kupata siku za hedhi kama kawaida.


Kufunga uzazi kwa mwanaume pia ni njia nzuri ya uzazi wa mpango, mwanaume atakwatwa mirija ya uzazi , baada ya makubaliano ya wawili kwa idadi ya watoto walionao, njia hii haitoathiri hamu ya kujamiiana  wala kupunguza nguvu za kiume.


 Mratibu wa uzazi wa mpango Taifa  Maurice Hiza ,alisema kuwa ni asilimia 27.4 ya watanzania ndio wanaotumia uzazi wa mpango, kwa mujibu ya sensa ya mwaka 2012 Tanzania inaidadi wa watu milioni 45.


Lengo la kuanzishwa uzazi wa mpago ni kupunguza vifo vya mama wajawazito, kuwa na maisha bora kwa mama na watoto anaowazaa, mpaka  kufikia mwaka 2015 asilimia 60 ya wanawake na wanaume wajue na kutumia uzazi wa mpango.


Mikoa ambayo iko nyuma katika matumizi ya uzazi wa mpango ni kama Mara asilimia 10, Mwanza asilimia 12, Shinyanga asilimia 13, Kigoma asilimia 14 na Tabora asilimia 19. 


Mikoa ambayo imefanya vizuri ni kama Kilimanjaro asilimia 50, Morogoro asilimia 40, Ruvuma asilimia 43, Tanga asilimia 41, Dar es salaam asilimia 34.8, na  asilimia 25 ya wanawake kote nchi hawatumii njia yoyote ya uzazi wa mpango.


   
Changamoto wanazokabiliana nazo katika uzazi wa mpango, ni ungezeko la idadi ya watu, kiwango kikubwa cha uzazi, kiwango kidogo cha matumizi ya kisasa ya uzazi wa mpango.


Changamoto zingine ni mila potofu, upungufu wa dawa na vifaa mbalimbali vya uzazi wa mpango, wanaume kutowaruhusu wake zao kutumia njia za uzazi wa mpango pamoja na elimu ndogo juu ya matumizi ya dawa navipandikizi mbalimbali.


Katika sera ya taifa ya uzazi wa mpango ya mwaka 1994, uzazi wa mpango ni haki ya kimsingi kwa kila mtu bila ya kujali umri, ameolewa au ameowa au amezaa au hajazaa.


Aidha sera hiyo inasema kuwa vijana wote wanahaki ya kupata taalifa, elimu ushauri nasaha juu ya uzazi wa mpango, vijana ambao wanakiri kwamba wanajamiiana, wanahaki ya kupewa njia za uzazi wa mpango wanazopendelea zinazowafaa baada ya kupata ushauri nasaha.

BUNGE LIJADILI RIPOTI ZA CAG KWA UWAZI

Sikika inapenda kuamini kwamba taarifa zilizochapishwa kwenye magazeti mbali mbali kuhusu Bunge kutojadili ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika mkutano huu wa 11, ama ‘zimenukuliwa vibaya’, au aliyezitoa alikuwa hajawasiliana kikamilifu na viongozi wa juu wa Bunge.

Iwapo habari kwamba Bunge halitajadili ripoti za CAG katika mkutano ni za kweli, basi Bunge limejitenga na wananchi na pia limejipunguzia madaraka yake ya kusimamia serikali kwa niaba ya wananchi. Kwa lugha nyingine, Bunge litakuwa limewaasi wapiga kura wake.

Takribani miaka kadhaa mfululuzo, CAG amekuwa akilalamika kwamba serikali haitekelezi mapendekezo na ushauri wake katika kusimamia vyema matumizi ya fedha za umma. Matatizo mengi ambayo CAG amekuwa akiibua katika ripoti zake kuhusu matumizi ya fedha za umma yamekuwa yakijirudia. Sikika inaamini kwamba kutojadiliwa kwa ripoti za CAG bungeni kwa uwazi kunalenga kuficha mapungufu haya ya serikali.

Katika mkutano wa 10 wa Bunge, tulishuhudia mabadiliko makubwa ya namna Bunge linavyosimamia na kuiwajibisha serikali, ambayo hata hivyo hayakutafuta baraka za wananchi. Wananchi wameiajiri serikali na wameliweka Bunge kuisimamia na kuiwajibisha serikali kwa niaba yao.  Bunge halina mamlaka ya kujiondolea au kujipunguzia majukumu ambayo linatekeleza kwa niaba ya wananchi bila kupata baraka za wananchi.

Katika mabadiliko hayo, mojawapo ni hili la kutokujadili ripoti za CAG ndani ya Bunge. Kifungu cha 63.3.b cha Katiba ya JMT kinalitaka Bunge kujadili utekelezaji wa kila Wizara wakati wa Mkutano wa Bunge wa kila mwaka wa bajeti. Mkutano huu wa sasa wa Bunge ni wa Bajeti.

Kipengele hicho cha Katiba hakikutaja Kamati za Bunge bali Mkutano wa Bajeti. Hivyo hata kama ripoti hizi zitapitiwa kwenye Kamati za Bunge, ni lazima, kwa mujibu wa Katiba zikajadiliwa kwenye Mkutano wa Bunge. Hapo wabunge wote na wananchi watapata fursa ya kujua nini kilichojiri katika kila ripoti ya CAG. Pia mjadala huo utanukuliwa katika kumbukumbu rasmi za Bunge yaani Hansad ambayo iko wazi kwa wananchi kuipitia muda wowote.

Mabadiliko ya pili yalihusu kubadilisha muundo na majukumu ya Kamati za Kudumu za Bunge. Katika mabadiliko hayo, Kamati ya Mashirika ya Umma ilifutwa na baadhi ya majukumu yake kuunganishwa kwenye kamati Hesabu za Serikali Kuu (PAC)

Majukumu ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ambayo hayakuhamishiwa kwenye Hesabu za Serikali Kuu (PAC) ni lile la kushughulikia ubinafsishaji na pia jukumu la kufanya tathmini ya mashirika ya umma. Majukumu haya mawili ni ya msingi kabisa katika kuwezesha wananchi kujua kinachoendelea katika ubinafsishaji ambao umelalamikiwa sana jinsi ulivyoendeshwa, na pia kujua ufanisi wa mashirika ya umma kwa ujumla.

Kwa mantiki hiyo, ni wazi kwamba mabadiliko yote mawili yalikusudia kuongeza usiri kwa namna serikali inavyotumia madaraka na mali za umma, hivyo kulifanya Bunge kukosa mamlaka yake, na kuwafanya wananchi kushindwa kuiwajibisha serikali. Pia inawezekana Bunge limevunja Katiba kwa kujipunguzia majukumu yake kikatiba. Pia ni wazi kwamba Bunge limeasi wananchi waliolichagua kwa kujivua jukumu la kuisimamia serikali.

Sikika inalitaka Bunge kurejea kwenye misingi ya majukumu yake kwa sababu majukumu hayo limepewa na wananchi. Bunge halina mamlaka ya kujipunguzia majukumu ya msingi lililopewa na wananchi bila ridhaa ya wananchi wenyewe. Iwapo Bunge linaamini lina mamlaka ya kufanya mabadiliko hayo na kwamba ndiyo njia bora ya kuongeza uwajibikaji wa serikali, litafute ridhaa ya wananchi kwanza.

Mwisho, Sikika inashauri mijadala inayohusu ripoti za CAG, mapendekezo ya bajeti ya serikali, mapato na matumizi, utekelezaji wa mipango na bajeti za mwaka uliotangulia lazima zijadiliwe katika mkutano wa Bunge ulio wazi ili wananchi nao waone namna wawakilishi wao wanavyotekeleza wajibu wao wa kusimamia fedha za walipa kodi.

Friday, April 5, 2013

HISTORIA YA SHULE YA MSINGI NACHINGWEA IMEBAKI KATIKA 'KAVA' LA DAFTARI

  
Historia ya shule ya msingi Kiegei katika kata ya Kiegei wilaya ya Nachingwea mkoa wa Lindi, imebaki katika kava moja tu la daftari, lakini shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa vitabu, vitendea kazi vya kufundishia na walimu.

Historia-ya-shule
Historia ya shule katika 'kava' la daftari
Shule hiyo iliyojengwa mwaka 1921 na wa Wakoloni, kwa sasa iko katika hali mbaya sana, haina walimu, hakuna vitabu, hakuna makabati ya kutunzia vitabu na majengo chakavu.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Fred Mchekenje alisema kuwa, shule inakabiliwa na changamoto nyingi sana kwa sasa, kuna walimu watatu tuu shule nzima na wanafunzi wako 650, hakuna vitabu vya kufundishia na kujisomea kwa wanafunzi, kwa sasa kuna vitabu 20 tu vya masomo mbalimbali shuleni hapo, pamoja na vitendea kazi kama chaki hakuna pamoja na ubao wa kuandikia umechaa maandishi hayaonekani vema.
Fred-Mchekenje
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Kiegei Fred Mchekenje akinionesha historia ya shule hiyo iliyopo ndani ya kava la daftari
"Uhaba wa walimu, vitabu na vitendea kazi vya kufundishia darasani, vinachangia kushusha ufauru wa wanafunzi hapa shuleni na kuchangia ongezeko la utoro na mimba za umri mdogo kwa wanafunzi wa kike,"alisema Mchekenje.
Mchekenje alisema kuwa  mwaka 2012, matokeo ya darasa la nne yalikuwa mabaya sana, walifanya mtihani watoto 95, walifauru watoto 8 wavulana 6 na wasichana 2. Kwa sasa tunahitaji walimu 15 pamoja na vitabu 300 vya kufundishia masomo mbalimbali na chaki ya kuandikia ubaoni.
Juma Ramadhini ni mwanafunzi wa darasa la tano katika shule hiyo, lakini toka amenza darasa la kwanza hajawahi kusoma kitabu chochote kile zaidi ya mwalimu kuwasomea na kuandika ubaoni anapoingia darasani.
wanafunzi-vitunguu
Baadhi ya wanafunzi wakiwa darasani huku nyuma ya darasa kukiwa kumeanikwa vitunguu vya mwalimu
"Nipo darasa la tano sasa lakini sijawahi kusoma kitabu toka nimeingia darasa la kwanza, naambulia kuliona kava ya nje ya kitabu pale mwalimu apoingia darasani kutufundisha, hata kusoma pia ni tatizo kwangu nachojua ni kuandika jina langu pekee lakini kusoma kitabu au gazeti siwezi,"alisema Juma.
Kwa upande wake Afisa elimu wa shule ya msingi katika wilaya hiyo Makwasa Bulenga alisema kuwa, tatizo la ukosefu wa vitabu na walimu katika shule za msingi wilaya ya Nachingwea ni kubwa sana, ndio chanzo cha wanafunzi kuferi masomo mbalimbali kwa sababu ya kukosa vitabu na walimu shuleni.
Bulenga alisema kuwa, Mwaka 2012 wanafunzi 3,636 walifanya mtihani wa kumaliza darasa la saba, wanafunzi 10,39 ndio waliofauru kujiunga na sekondari, wavulana 583 na wasichana 456 sawa na asilimia 28.5.
"Ufaulu wa wanafunzi unashuka mwaka hadi mwaka kwa sababu ya kutokuwa na walimu na vitabu vya kufundishia kwa wilaya mzima, kwa sasa kitabu kimoja kinatumiwa na wanafunzi zaidi ya 15, sasa hapo kunauwezekano wa mtoto kuelewa na kufauru inavyotakiwa,"alisema Bulenga.
Wilaya ya Nachingwea ina kata 32, kati ya hizo kata sita ziko mjini ambako kidogo kuna vitabu na walimu, lakini kata 26 za vijijini huko ndio hakuna walimu pamoja na vitabu vya kufundishia.
Idadi ya wanafunzi katika shule za mjini, wavulana 2,365 na wasichana 2,424 jumla ni wanafunzi 4,789, katika shule za vijijini idadi wa wanafunzi  wavulana 13,319 na wasichana 13,728 jumla ni 27,047.
Kwa idadi hii ya wanafunzi wa shule za vijijini, ambako hakuna vitabu, walimu na vitendea kazi je? wanafunzi watajua kusoma na kuandika na kufauru katika mitihani mbalimbali? hii ni changamoto inahitaji kuangaliwa kwa jicho la pekee ili tuweze kupata viongozi bora nchini hapo baadae.

Thursday, April 4, 2013

HATA WANAWAKE WANAWEZA

Fatuma Abasi na Bibi Halima wakazi wa kijiji cha Lukuledi wilaya ya Masasi mkoa wa Mtwara, wakiwa shambani wanapalia zao la mahindi, zao hilo linapaliwa mara tatu katika kipindi cha ukuaji wake, kipindi cha kwanza yakiota, kipindi cha pili kiwa kimo cha kati na kipindi cha mwisho cha kupalia yakiwa yamebeba mahindi. Kwa sasa guni moja la mahindi linauzwa kuanzia shilingi 90,000 hadi shilingi 100,000, Fatuma na Bibi Halima wamelima heka mbili kama kutakuwa na mvua za kutosha wanatarajia kuvuna magunia zaidi ya 50.


Chiku Juma mkazi wa kijiji cha Kiegei katika wilaya ya Nachingwea mkoa wa Lindi, akioneakana anapanda mahindi katika shamba la heka tano, shamba hilo amelima yeye mwenyewe akisaidiwa na kaka yake Musa Juma.



Amina Bakari na Hawa Mtumba wakazi wa kijiji cha Ikwiriri wilaya ya Rufiji mkoa wa Pwani wakibeba gunia la mkaa kupeleka katika basi la kutoka Mtwara, Wanawake hao ni wafanyabiaashara ya kaa kwa muda wa miaka mitano sasa wamekuwa wakifanya kazi hiyo ambayo wanafanya wanaume hapa nchini, gunia moja la mkaa kwa sasa ni shilingi 35,000 hadi shilingi 40,000.
Kwa siku wanauza magunia 10 hadi 15 ya mkaa wa wasafiri mbalimbali wanaotoka katika mikoa ya Lindi na Mtwara.





 Baadhi wa Wanawake niliokutana nao katika Barabara ya Bibi Titi jijini Dar es salaam, Wanawake hao wakiwa wameucha usingizi baada ya kazi ya kuombaomba bila ya wasiwasi huku wakiwa na watoto wadogo, lakini Wanawake hao wamekuwa wakikaa eno hilo kwa kuomba wapita njia mbalimbali ili waweze kupata pesa ya matumiazi ya kila siku. Wanawake kama huwa wenye nguvu na viungo vyao vimekamilika na wana uwezo wa kulima na akajipatia kipato na kuitunza familia yake kijijini! kwa nini wanawake hawa wanaomba na kuwatesa watoto ambao hawana hatia!

UHABA WA MAJI SAFI NA SALAMA MTWARA WAKAZI WACHOTA MAJI YA MTO NANGOO

Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Nangoo wakichota maji kwa matumizi ya nyumbani katika mto wa Nangoo uliopo katika wilaya ya Masasi mkoa wa Mtwara, tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika mkoa huo ni tatizo sugu ambalo mpaka sasa bado halijapatiwa ufumbuzi wake. Maji wanayotumia wakazi wakijiji hicho na wakazi wa kijiji cha jirani sio safi na salama, dumu moja la maji hayo linauzwa kati ya shilingi 5,00 hadi shilingi 1,000.

Thursday, March 28, 2013

KUKOSEKANA KWA ARV KWACHANGIA WATOTO KUZALIWA NA VVU

Zarula Rajabu (30) anaishi na virusi vya ukimwi,anawatoto wanne kati ya hao mtoto mmoja ana maambukizi ya virusi vya ukimwi, anishi katika kijiji cha Matekwe katika kata ya Kilimarondo wilaya ya Nachingwea mkoa wa Lindi.

Zarula aligundulika na vvu akiwa na ujauzito wa miezi sita, alipohudhuria kliniki ya zahanati ya Matekwe kwa mara ya kwanza. Lakini hakupewa dawa za ARVs za kumkinga mtoto aliyetumboni asipate na maambukizi ya virusi vya ukimwi.

“Ningepatiwa dawa za ARVs kipindi cha ujauzito wangu, na wakati wa kuumwa uchungu, ningemzaa mtoto wangu bila ya kupata maambukizi ya virusi vya ukimwi na angeishi maisha marefu,”alisema Zarula.

Muuguzi katika zahanati ya Matekwe Lidia Urio (51) alisema kuwa, Zarula alipohudhulia mara ya kwanza kliniki alimpima na kugundua kuwa ana maambukizi ya virusi vya ukimwi.

 “Nilimpompima na kugundua kuwa ana virusi vya ukimwi nilitakiwa kumuanzishia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo, pamoja na kumkinga mtoto aliyetumboni asipate maambukizi ya virusi vya ukimwi, lakini kutona na kuharibika kwa dawa nimeshindwa kumuanzishia hiyo dozi,”alisema Muuguzi Urio.

 Aliendelea kuhudhuria kliniki mpaka muda wa kujifungua ulipofika, alijifungulia katika Zahanati ya Matekwe, lakini hata alipokuwa anaumwa uchungu hakupata dawa za ARVs ambazo zinamkinga mtoto asipate maambukizi wakati wa kuzaliwa. Ndio chanzo cha yeye kumuambukiza mtoto wake wan ne mwenye miezi saba virusi vya ukimwi.

Baada ya miezi mitatu kupita toka amejifungua, Zarula alilazimishwa kumpeleka mtoto wake ktika hospitali ya wilaya ya Nachingwea, ili atolewe damu na kupimwa kama mtoto amepata maambukizi au hajapata.

Zarula alikwenda alifanikiwa kupata pesa ya kwenda hospitali ya wilaya kumpima mtoto wake, utaratibu wa kupima watoto wa chini ya miezi 18 ni lazima mtoto anatolewa damu katika kisigino cha mguu kwa sababu umri aliokuwa nao ukimpima kwa kumtoa damu kama unavyowapima watoto wenye miezi 18 na watu wazima, huwezi kugundua kuwa anamaambukiz kwa sababu bado kuna antibody za mama mwili kwa mtoto wa chini ya miezi 18 na hapo mtoto anatakiwa kupimwa antijen zake au DNA.

Aidha damu hiyo ikipatikana inahifadhiwa kwa utaratibu maalumu, kisha kusafirishwa kwenda katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa vipimo vya hali ya juu , ili kugundua kama mtoto wa chini ya miezi 18 amepata maambukizi au hajapata.

Mashine maalumu za kupima maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa watoto wa chini ya miezi 18 hapa nchini, ziko katika kanda nne nazo ni Muhimbili Dar es salaam, Bugando Mwanza, Kcmc Moshi na Mbeya.

Katika mkoa wa Lindi na Mtwara hawana mashine hizo, inabidi damu zote za watoto waliozaliwa na mama wenye maambukizi ya virusi vya ukimwi, inawalazimu kupeleka damu zao katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ni gharama kubwa sana na kila baada ya wiki mbili au tatu wanapeleka damu za watoto hao.

Zarula anaficha kuwaeleza familia yake kwamba anaishi na virusi vya ukimwi, kwa sababu anahofia kutengwa kama alivyotengwa mjomba yake baada ya kusema anaishi na virusi vya ukimwi.

“Naogopa kuwaeleza ndugu zangu kwamba ninaishi na virusi vya ukimwa, wanajaziba sana; wanaweza kunitenga katika familia kama walivyomtenga mjomba, ni mume wangu pekee ndio anafahamu afya yangu kwa sasa,” alisema Zarula.

Mume wake Zarula, hajapima maambukizi ya virusi vya ukimwi toka mwezi Julai mwaka 2011, mkewe akiwa na ujauzito wa miezi sita mpaka sasa mtoto anamiezi saba, mkewe amemshauri kwenda kupima lakini amekataa.

“Mume wangu alikata kupima maambukizi ya virusi vya ukimwi, muuguzi Lidia amejitahidi kumshawishi kupima na kumueleza umuhimu wa kupima maambukizi ya vieusi vya ukimwi lakini amekataa mpaka sasa,” alisema Zarula.

Kwa mujibu wa muuguzi wa zahanati ya Matekwe Lidia alisema kuwa, umuhimu wa kupima maambukizi ya virusi vya ukimwi ni kujua kama umeambukizwa au bado, na kama umeambukizwa utapimwa kujua kinga zako za mwili zipo kwa kiasi gani, kama zimeshuka utaanzishiwa dawa za ARVs, pia ukijua kama unamaambukizi utachukua tahadhari kuwaambukiza wengine ambao hawana maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Athumani ni mzaliwa wa mkoa wa Tanga, lakini kwa sasa anaishi katika kijiji cha Matekwe, anafanyakazi ya uchimbaji madini ya dhahabu na rubi katika machimbo ya mbwemkuru.Katika kipindi cha ujauzito wake, Zarula hakuweza kwenda katika kituo cha afya kilimarondo, kupatiwa dawa za ARVs, kwani nauli ya kwenda huko kutoka Matekwe kwa pikipiki ni zaidi ya shilingi 20,000. Ni zaidi ya kilometa 28, na hakuna usafiri mwengine. Pia hana uhakika kama akienda kituo cha afya cha kilimarondo atafanikiwa kupatiwa ARVs.

Kijiji cha Matekwe kina wakazi 2,548  kati ya hao wajawazito kwa mwaka 2012 walikuwa  84, waliojifungua 33, kati ya hao wenye maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU)  watatu.

Muuguzi wa Zahanati ya Matekwe Lidia, alikili kuwepo kwa tatizo hilo kwa akinamama hao waliogundulika na maambukizi ya ukimwi (VVU), kushindwa kupewa dawa za ARVs ndio imechangia kuwaambukiza watoto wakati wa kuzaliwa.

Watoto watatu walizaliwa na mama hao, ambao hawakupata dawa za ARVs walivyokuwa wajawazito, watoto wao wote watatu wamepata maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Ulio alisema kuwa toka mwezi Juni 2011kulikuwa hakuna dawa za ARVs katika zahanati ya Matekwe, mpaka Desemba 2011, ndio dawa hizo zililetwa, muda huo wajawazito watatu walikuwa wameshajifungua na watoto walipata maambukizi ya virusi vya ukimwi.

"Dawa nilizonazo za kumkinga mtoto na maambukizi akiwa tumboni kwa mama zilikuwa zimekwisha matumizi yake, sikuweza kuwapatia dawa hizo, zingeweza kumletea madhara yeye na mtoto aliyetumboni, ulipofika muda wa kujifungua basi nikawazalisha hivyo hivyo”alisema Uliyo.

Ulio alitoa ushauri kwa wajawazito hao kwenda katika kituo cha afya kilimarondo kupatiwa dawa za ARVs, lakini walisema hawana pesa ya kukodi pikipiki mpaka katika kituo cha afya.

Zubeda Abasi (23), ni mkazi wa kijiji cha Matekwe, anaishi na virusi vya ukimwi, naye pia ana mtoto wa miezi tisa kwa sasa, alipokuwa mjamzito alihudhulia katika zahanati ya Matekwe lakini, kwa sababu dawa zilikuwa zimekiwsha muda wake katika zahanati hiyo,hakupewa dawa za ARVs, ndio chanzo cha mkumzaa mtoto wake akiwa ameambukizwa virusi vya ukimwi.

"Nilipokuwa na ujauzito wa miezi mitano, nilikwenda kliniki kupima nikaambiwa ninamaambukizi ya virusi vya ukimwi, nilishauriwa kumleta bwana aliyenipa mimba kupima, alikubali alivyopimwa akagundulika hana maambukizi, alinikimbia na kuniacha pekee yangu na mimba mpaka sasa nimejifungua mtoto anamiezi saba," alisema Zubeda.

Hakuweza kwenda katika kituo cha afya cha kilimarondo, kupewa dawa za kumkinga mtoto asipate maambukizi.

Kabla ya kushika mimba, Zubeda alikuwa anafanyakazi ya kunyoa nywele za katika saloon za kiume huko kilwa, amefanya kazi hiyo kwa muda wa miezi nane, akaamua kurudi kwao matekwe.

 Zubeda aliporudi Matekwe alipata bwana mwengine, wakaanza mahusiano bila ya kupima, baada ya mwezi mmoja katika mahusiano alishika ujauzito.Baada ya miezi mitano kupita alikwenda zahanati ya matekwe kuanza kliniki, hapo ndipo alipogundulika kuwa anamaambukizi ya virusi vya ukimwi.

"Sikupewa dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huu nikaanza kuumwa na kudhohofu mwili, na pesa sina ya kwenda kituo cha afya cha kilimarondo kuchukua dawa niliendelea kuumwa homa za mara kwa mara mpaka nimejifungua mtoto wangu ambaye naye amepata maambukizi wakati wa kuzaliwa,"alisema Zubeda.

Dk. Daniel Magesa Mkurugenzi msaidizi wa tiba kutoka Pasada alisema kuwa, mjamzito anashauriwa kwenda kliniki mapema na kupima maambukizi ya virusi vya Ukimwi, akigundulika kama anamaambukizi anaazishiwa dawa ya nevirapine ya kumkinga mtoto asipate maambukizi akiwa tumboni.

Kwa mjamzito mwenye (VVU) akiwa na kinga chini ya 350 anatakiwa kutumia dawa ya kumkinga mtoto na maambukizi ijulikanayo kama zidovudine, na anatakiwa kutumia dawa za ARVs. Lakini, kama anakinga za juu zaidi ya 350 akiumwa uchungu anapewa dawa aina ya nevirapine.

Dawa hizo zote zinasaidia kupunguza kasi ya virusi vya ukimwi kuzaliana, na kama virusi vitapunguza kasi ya kuzaliana mjamzito atakuwa na kinga ya hali ya juu zaidi na kuweza kupambana na maradhi nyemelezi pamoja na kujifungua salama na mtoto pia kutopata maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Mkoa wa Lindi Dk. John Sijaona alisema kuwa, upatikanaji wa dawa za ARVs ni changamoto kubwa sana kutokana na bohari ya dawa kuchelewesha madawa hayo, unaweza kuagiza na ukaletewa baada ya miezi miwili hadi mitatu na unaweza ukaletewa dawa ambazo sio unazozihitaji.

"Tatizo ni bohari ya madawa kuchelewesha madawa ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya ukimwi, hayaji kwa muda ule ambao tumeomba, na sio kwa dawa za kupunguza makali ya ukimwi hata vitendanishi vya kupimia maambukizi ya virusi vya ukimwi, ukienda unapewa boxi tano ambazo hazitoshi kulingana na wingi wa watu wanaohitaji upimaji, pia kuletewa dawa ambazo sio ulizoomba" alisema Dk. Sijaona

Kwa mujibu wa Dk. Sijaona alisema kuwa, upatikana duni wa dawa mbalimbali zikiwemo za ARVs, unachangiwa na baadhi ya wahudumu wa afya katika zahanati mbalimbali kukosea kujaza fomu za bohari ya madawa (MSD), fomu hizo zikikosewa hata herufi moja tuu bohari ya madawa wanaiweka pembeni hawatoi dawa, hivyo basi dawa zinakuja pungufu kwa sababu hiyo.

Dk. Sijaona alisema kuwa  changamoto nyingine ni wilaya ya Nachingwea kugawanyika mara mbili, kuna kanda a na kanda b, wanaweza kupeleka dawa kanda a kumbe na kanda b nako hakuna dawa.Pia uletaji wa dawa bila ya kushirikisha watendaji wa vijiji na hospitali ya wilaya kwa msd na kulazimishwa kusaini fomu ya madawa bila ya kukagua dawa au kujua kwamba zimefika sehemu husika, hilo nalo ni tatizo sugu kwa msd kanda ya Mtwara.

Dk. Sijaona alisema kuwa mjamzito hawezi kuanza kupewa dawa za kupunguza makali ya virusi vya ukimwi mpaka apimwe, kujua kama ana maambukizi au hana akionekana na maambukizi ndio anaanzishiwa dawa hizo.

Mahitaji ya upamaji yameongezeka kwa wajawazito kuanzia mwaka 2010 walipima wajawazito 4,472. Wanaume walipima maambukizi ya virusi vya ukimwi na wake zao walikwa 1,948.

Dk. Sijaona alisema kuwa, kwa sasa wilaya ina vituo 58 vya kupima maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa kupitia njia ya shawishi, kupitia vituo hivyo idadi kubwa ya watu wanaohitaji huduma hiyo imeongezeka kutoka 1500 kwa mwezi hadi kufikia watu 3000 hadi 4000 wanapima. Nachingwea kuna wakazi 1,95,755.

Asilimia 28 hadi 33 ya wajawazito wanaohudhulia kliniki na kupimwa nchini Afrika Kusini wanamaambuki ya virusi vya ukimwi, mwezi Agosti mwaka 2009 zaidi ya wajawazito 776 kati ya 100,000 walipoteza maisha kwa sababu ya kuwa na kinga za mwili chini ya 200 na kutotumia dawa za ARVs ipasavyo.

Kufuatia hali hiyo nchi hiyo ikaweka mkakati mahususi wa kutumia dawa za ARVs kwa wajawazito mbalimbali, pamoja na kuwaangalia kwa ukaribu jinsi gani ya kupata dawa na matumizi ya dawa hizo pamoja na chakula na wakafanikiwa kuwapatiwa dawa wajawazito 2,000 kutoka katika mradi wa (RHRU)

Pia nchini Kenya maambukizi ya virusi vya ukimwi yameshuka kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kutoka silimia 11 hadi asilimia 4 mwezi  mei mwaka 2010, sababu kubwa ya kushuka ni kutumia vituo vya afya kuanzi 17 hadi 26 katika eneo la magharibi mwa nchi hiyo kwenye wilaya ya vijijini kama Ndhiwa. Kwa kuwahamasisha wajawazito wakifika kliniki kupima na kuwapatia dawa za ARVs ili kumkinga mtoto aliyetumboni asipate maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Kwa mujibu wa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Hussein Mwinyi, huduma za kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda mtoto, (PMTCT) zimekuwa zikitolewa nchini tangu mwaka 2000. Hadi kufikia mwezi Desemba 2011 huduma hii imetolewa bila ya malipo katika vituo 4,603 sawa na asilimia 93.

Mwaka 2011 jumla ya wajawazito 86,875 wenye maambukizi ya Virusi vya Ukimwi walipatiwa dawa za ARVs kuzuia maambukizi kwenda kwa mtoto. Hii ni sawa na asilimia 71 ya wajawazito 122,146 waliokadiriwa kuwa na maambukizi ya VVU.

Kwa mujibu wa kitabu cha bajeti cha mwaka 2012/2013, cha wizara ya afya na ustawi wa jamii, kinaeleza kuwa jumla ya shilingi 253,468,765,171.00 pesa hizi zimetengwa kwa ajili ya kununua na kusambaza dawa, vifaa tiba na vitendanishi katika zahanati, vituo vya afya na hospitali za umma. Kati ya fedha hizo shilingi 147,423,200.00 zimetolewa na Global Fund kwa ajili ya kununua na kusambaza  dawa za malaria na ukimwi nchini.

Sunday, March 24, 2013

GOFU LA NYANZA CO-OPERATIVE UNION

Gofu la chama cha ushirika cha Nyanza lililopo katika kijiji cha Nassa katika wilaya ya Nyashimo mkoa mpya wa Simiyu. Ndani ya gofu hilo kuna vinu vya kuchambua pamba na kukamua mafuta ya mbegu za pamba, kwa muda mrefu sasa vinu hivyo havitumiki na wakulima wanapeleka pamba kuchambua katika wilaya ya Bunda mkoa wa Mara. Kwa sasa wakulima wa pamba wako katika kilimo, kilo moja ya pamba kwa mwaka jana ilikuwa shilingi 630.