Mama

Nani kama Mama .

Afya ya Mimba

Mwanamke anayetaka kubeba mimba anashauriwa aache kunywa pombe na kuvuta sigara.

Mama na Mtoto

Mazingira mazuri ya Afya ni Moja ya njia ya kuepuka matatizo ya mama wakati wa kujifungua.

Tuwalinde watoto

watoto 200 kati ya 100,000 wanapoteza maisha wakati wa kuzaliwa na baada ya kuzaliwa, idadi hii ya vifo ni kubwa sana hapa nchini Tanzania.

Karibu kwenye blog hii kwa Habari za Afya ya Mama na Mtoto.

Kufikia mwaka 2010, takwimu zilikuwa zinaonesha kwamba kila wanawake 454 katika vizazi hai 100,000 walikuwa wanapoteza maisha wakati wa ujauzito au kujifungua kwa matatizo mbalimbali ya uzazi.

watoto 200 kati ya 100,000 wanapoteza maisha wakati wa kuzaliwa na baada ya kuzaliwa, idadi hii ya vifo ni kubwa sana hapa nchini Tanzania..

Thursday, February 28, 2013

RAHA ILIOJE KUANGALIA KICHANGA

Malaika huyu ana saa mbili tu baada ya kuzaliwa na  Nyangeta Chacha (29) katika hospitali ya mkoa wa Mara, mtoto ana uzito wa  kilo 3 mama wa mtoto anaishi mtaa wa nyakato katika wilaya ya Musoma mjini mkoa wa Mara. Hospitali hiyo imejengwa mwaka 1932 na kuanza kazi kama kituo cha afya mwaka 1933, lakini kwa sasa inakabiliwa na upungufu wa wauguzi mahitaji ni wauguzi 200.

HUU NDIO USAFIRI WA MJAMZITO BUTIAMA

Dereva Bajaji Malegesi Malegesi  akiwa kazini katika kijiji cha Rwamkoma akitokea Butiama Mjini, usafiri huo kwa abiria analipa nauli ya sh. 15,00 lakini kwa mjamzito akikodi analipa sh. 15,000 kutoka Rwamkoma mpaka katika hospitali ya wilaya ya Butiama mkoa wa Mara.

Usafiri huo sio salama kwa wajawazito katika kijiji hicho chenye wakazi zaidi ya 5000 na kila mwezi wanapokea wajawazito kuanzi 10 hadi 15 ambao wanamatatizo ya uzazi na wanahitaji usafiri wa kwenda hospitali.

Wednesday, February 27, 2013

MATATIZO YA HUDUMA ZA AFYA NCHINI TANZANIA

Baadhi ya wajawazito wakisubili huduma katika kituo cha afya cha Manyamanya wilaya ya Bunda, lakini mtoto wa miezi saba akipimwa uzito katika mzani wa kichanga katika zahanati ya Rwamkoma wilaya ya Butiama mkoa Mara.

Monday, February 25, 2013

UTAPIAMLO BADO UPO TANZANIA?

Wakati jamii mbalimbali wakifikiri kwamba ugonjwa wa Utapiamlo umeisha lakini katika Jimbo la Mwibara wilaya Bunda mkoa wa Mara katika kata ya Kibara na Kisori ugonjwa huo bado upo.
Sababu kubwa ya kuwa na ugonjwa huo ni ukame kwa kukosa mvua za kutosha pamoja na kupungua kwa samaki na dagaa katika ziwa Victoria na wanaovuliwa wanaishia kwenye viwanda vya samaki kwa kutengeneza minofu na kusafirishwa nchi mbalimbali.

Watoto hao wangekula samaki na dagaa kwa wingi wangeweza kupata madini ya chuma na protini kwa wingi na ingeweza kupunguza ugonjwa huo.
Kati ya watoto 17,570 watoto 294 wanaumwa ugonjwa wa utapiamlo ambayo ni sawa na asilimia 1.5.

Sunday, February 24, 2013

HUYU NDIO WANAMKE SHUJAA?

Boke Makori ni wifi yake na Nyangeta Maiga Makori wakazi wa kijiji cha Nyambono wilaya ya Musoma vijijini, Boke ndiye 'WANAMKE SHUJAA' aliyemshawishi kaka yake Mwita Makori kuuza ng'ombe ili wapate nauli ya kumpeleka wifi yake kituo cha afya Manyamanyama Bunda ili ajifungue katika uwangalizi wa wataalamu.

"Wifi akiwa na ujauzito wa miezi nane nilianza kumshawishi kaka kuuza japo ng'ombe mmoja ili tupate nauli ya kumpeleka wifi kituo cha afya alikataa kwa mara ya kwanza, lakini sikuchoka kumwambia kila ninapokwenda kumuona wifi maendeleo yake, niliendelea kumwambia zaidi ya mara tano ndio alikubali kipindi hicho Nyangeta alikuwa na ujauzito wa miezi tisa,"alisema Boke

Kwa upande wake mume wake Nyangeta Bwana Mwita Makori alisema ni kweli dada alikuwa akinihiza kuuza ng'ombe mmoja ili apate nauli ya kumpeleka mke wangu kujifungua katika kituo cha afya, nilikubali kwa shingo upande kwa sababu dada amening'ang'aniza kuuza ng'ombe, nilichaguoa kang'ombe kadogo nikauza kwa Tshs. 15,0000.


"Sasa nimeona umuhimu wa kuuza kang'ombe kangu kadogo ili mke wangu apate nauli ya kwenda kituo cha afya, amejifungua vema watoto mapacha ndio nimefika kumchukua kumrudisha nyumbani Musoma vijijini, nawashauri wanaume wa mkoa wa Mara kuwatunza wajawazito na kuwapeleka katika kituo cha afya kujifungua sio kung'ang'ania wakezao kujifungua kwa wakunga wa jadi,"alisema Mwita

Dereva wa Bodaboda Chacha alisema kuwa nasikia fahari kubwa sana kumbeba mama mwenye watoto mapacha kumrudisha kijijini, nitaendesha pikipiki pole pole na kukwepa mashimo ili mama na watoto wafike salama.

Ghalama za kukodi pikipiki kutoka kijijini Nyambono mpaka Bunda ni Tshs. 60,000 kwenda na kurudi kijijini, ni wanawake wangapi wanaowashawishi kaka zao vijijini kuuza ng'ombe, mbuzi,kuku pamoja na mazao ya kilimo ili ipatikane nauli ya kumpeleka mjamzito pindi anapoumwa uchungu kituo cha afya au hospitali?

Ni wanaume wangapi wanaokubali kuuza rasilimali ili mkewe ajifungulie katika kituo cha afya kwa uwangalizi wa wataalamu? kumbe inawezeka kupunguza vifo vya akinamama kwa jamii kubadilika kwa kutoa msaada kwa mjamzito akikalibia kujifungua?

Safari ya kuelekea kijijini ndio hiyooo imeanza kwa familia ya Makori? nadhani atawatunza vema watoto hao mapacha aliowapata ili wawe viongozi  wa baadae katika nchi yetu ya Tanzania.

HII NDIO MATVILLA BEACH NDANI YA MUSOMA

Hii ndio Matvilla Beach iliyoko Musoma Mjini pembeni mwa Ziwa Victoria Mkoa wa Mara.

Friday, February 22, 2013

AJIRA KWA MTOTO BADO KITENDAWILI KISICHOPATIWA JIBU?

Saa 4:00 asubuhi muda wa shule mtoto anachunga ng'ombe na mbuzi katika kijiji cha Mugundu wilaya Iramba mkoa wa Singida, nani atalimaliza hili?

MIUNDOMBINU,USAFIRI BADO NI KITENDAWILI KWA WAJAWAZITO MARA?

Ni saa 8:30 mchana Nyangeta Makori ambaye ni mjamzito anatoka kijiji cha Nyambono wilaya ya Musoma vijijini,usafiri unaofaa kwa mjamzito haupo hali iliyomlazimu kuchukua pikipiki na kupita katika barabara mbovu kwa saa nne, huku akisikilizia uchungu kutoka Msoma vijijini mpaka Kituo cha afya cha Manyamanyama wilaya ya Bunda mkoa wa Mara.

Alifika saa 11:30 jioni alipokelewa katika kituo cha afya cha Manyamanyama, bila ya kufahamu kama anamapacha katika tumbo lake,  kwa bahati nzuri baada ya muda saa moja alijifungua watoto wakiume wazuri, Doto akiwa na kilo 3.1 na Kulwa naye ana kilo 3.5 ndani ya mfuko mmoja wa uzazi.

Nyangeta huu ni uzazi wake wa tano ana watoto sita wote wakiume, watoto wa nne amejifungulia nyumbani akisaidiwa na wifi yake kwa kumshika sehemu ya mgongo wakati wa kujifungua na yeye kusukuma na kutoa mtoto, kitu kinachosababisha Nyangeta kuzaa nyumbani watoto wanne ni kijiji anachokaa hakuna zahanati na hospitali iko mbali ni mwendo wa saa 6 kwa pikipiki.

Wifi yake Nyangeta ni 'SHUJAA' amemuokoa Nyangeta asipoteze maisha kwa kumshawishi kwenda katika kituo cha afya kujifungua pamoja na kumsindikiza kutoka musoma vijijini mpaka Bunda, lakini pia ndiye mwanamke aliyemsaidia kujifungua nyumbani watoto wanne.

Ni wajawazito Tanzania wanaokumbana na shida wakati wa kutafuta huduma za kujifungua ikiwa pamoja na umbali, usafiri usio wa uhakika na barabara mbovu, kwa mujibu wa utafiti wa masuala ya afya ya uzazi ya Kitaifa wa serikali mwaka 2010(TDHS) unaeleza kuwa kila siku wajawazito 23 wanapoteza maisha kwa matatizo mbalimbali ya uzazi wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.

Thursday, February 21, 2013

LUSIANA MJAMZITO ANAYEPOTEZA DAMU KILA MWEZI

Lusiana Danda (26) alipokuwa na mimba ya miezi nane (Oktoba 2012), alikuwa anatokwa na damu ya mwezi. Hali hii ambayo ni hatarishi kwa mjamzito na mimba yake ilianza wakati ana mimba ya miezi minne, baada ya yeye kuugua malaria.

Lusiana, ambaye ni mkulima na mkazi wa kijiji cha Ifinga, Songea, alipata matibabu katika zahanati ya Ifinga. Alivyokutwa na malaria, alipewa dozi ya dawa ya mseto ambayo hakumaliza.

“Niliamua kuacha kumeza dawa baada ya kusikia naendelea vema. Pia, nilipokuwa nameza dawa hizo nilikuwa nasikia maumivu chini ya kitovu; nikahofia mimba yangu isije kutoka,” alisema Lusiana.

Lusiana hajaolewa na hana mahusiano na mwanaume aliyempa mimba aliyokuwa nayo wakati huu. Kwa kuwa tayari ana watoto wawili na pasipokuwa na mtu mwingine wa kumtegemea, Lusiana aliendelea na kazi za kulima kama kibarua bila ya kupumzika, japokuwa alikuwa mjamzito na japokuwa alikuwa anaumwa.

Siku moja, Lusiana akiwa shambani na baada ya kulima kwa saa mbili, ghafla aliaanza kusikia maumivu makali chini ya kitovu. Maumivu hayo yalikuwa yakizidi kadiri muda ulivyokwenda na alikuwa akijisikia hali ya kutaka kujisaidia haja ndogo. Alipoenda msalani kujisaidia, ndipo akashtukia kuwa haukuwa mkojo bali ilikuwa ni damu.

Damu hii iliendelea kutoka kidogokidogo kwa siku tatu bila kukatika, ndipo Lusiana aliamua kwenda zahanati ya Ifinga kupima kama ujauzito wake bado ulikuwa salama.

“Nilipofika zahanati niliambiwa nitoe Tsh. 2,000 ili nipimwe kujua kama mimba bado ipo. Nilikuwa sina pesa kwa hiyo nilirudi nyumbani nikiwa sina raha,” alisema Lusiana.

Japokuwa damu ilikoma kutoka siku hiyo hiyo ya tatu, baada ya wiki mbili, Lusiana alifanikiwa kupata Sh10, 000 na kurudi tena kwenye zahanati kufanya kipimo cha ujauzito. Kipimo kilionesha kwamba bado alikuwa mjamzito lakini, mwezi uliofuata damu iliendelea kutoka tena na Lusiana aliporudi kwenye zahanati ya Ifinga kwaajili ya kujua kwa nini, hakufanikiwa.

“Niliambiwa hakuna vifaa vya kuchunguza kujua kama damu inayotoka inasababishwa na nini; na mhudumu wa afya aliniambia kuwa hajasomea kujua damu inayotoka kwa mjamzito inasababishwa na nini,” alisema Lusiana.

Kwa mujibu wa Dk. Ahmed Makuani, mtaalam wa magonjwa ya wanawake na uzazi salama kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kutokwa na damu kwa mjamzito ni kiashirio cha hatari sana. Mjamzito akiona damu inatoka anatakiwa kuwahi haraka hospitali.

Dk. Makuani alisema wanawake walio na umri wa zaidi ya miaka 35 wakishika mimba wako katika hatari ya kupoteza damu kwa sababu ya kondo la nyuma kuning’inia katika shingo ya kizazi upande wa ndani. Tatizo hili linajulikana kama placenta previa. Kitendo cha kondo la nyuma kuvumba kinaweza kusababisha kuachia sehemu iliyojishika na kutoa damu sehemu ile iliyoachia, pamoja na kuziba njia ya uzazi kuwa ndogo na mtoto kushindwa kutoka vizuri, kuzaliwa mtoto mfuu kwa kukandamizwa na kondo hilo, kuzaliwa mtoto njiti pamoja na kuzaliwa mtoto mwenye uzito mdogo
 
Naye Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Seif Rashid anasema kuwa tatizo la mjamzito kupoteza damu ni tatizo sugu na kubwa sana  hapa nchini Tanzania na ndio chanzo kikubwa cha wajawazito kufariki. Dk. Rashid alisema kuwa, wataalam wa kulitatua tatizo hilo wapo wachache sana katika zahanati mbalimbali za vijijini ambako asilimia 75 ya watanzania ndio wanaishi huko.

“Kwa sasa tupo katika mkakati wa kuboresha zahanati mbalimbali kwa kuwapeleka watumishi wa sekta ya afya kusoma, masuala ya uuguzi kwa miaka miwili ili muuguzi anapokutana na tatizo hilo awe na ujuzi wa kumsaidia  mjamzito,”alisema Dk. Rashid.

Wakati Sera ya Afya ya 2007 inasistiza utoaji wa huduma bora na bure kwa mjamzito, hili bado ni changamoto kwa maeneo kama Ifinga, Songea. Zahanati ya Ifinga ina nesi mmoja na muhudumu wa afya aliyefika darasa la saba mmoja. Pia, katika zahanati hiyo, kuna mganga moja na mpimaji magonjwa maabara mmoja.

Hakuna mtaalam wa magonjwa ya mjamzito na wala hakuna vifaa tiba kama mashine ya kumsaidia mtoto kupumua akizaliwa. Kwa wakati huu, ambapo Lusiana alikuwa ni mjamzito na kuhitaji huduma hizi, kulikuwa hakuna dawa za kumchoma sindano mama ili mfuko wa uzazi usinyae baada ya kujifungua na mzani wa kupimia mtoto akizaliwa mbovu.

Japokuwa ameshindwa kupata ufumbuzi wa tatizo lake, Lusiana anatarajia kujifungua katika zahanati ya Ifinga. Hana uwezo wa kwenda katika hospitali ya Peramiho inayomilikiwa na Kanisa Katoriki Jimbo la Ruvuma, ambapo ni kilometa 243 kutoka katika kijiji cha ifinga. Nauli ya kwenda ni Tsh.38,000 na gharama za kujifungua ni Tsh. 11,000; hapo bado gharama za kuishi.

Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Songea Dk. Daniel Masawe alisema kuwa katika wilaya hiyo, wajawazito 95 kati ya 100,000 kila mwaka wanapoteza maisha kwa sababu ya upungufu wa damu. Alithibitisha kwamba vifo hivi vinachangiwa na ukosefu wa vifaa tiba pamoja na wataalam wa kumsaidia mjamzito kujifungua salama katika zahanati mbalimbali kwenye wilaya hiyo.

"Kwa sasa watalaam wa kumsaidia mjamzito kujifungua salama ambao wamebobea katika ukunga hapa Songea ni wanne tu, ukilinganisha na zahanati 35 tulizonazo," alisema Dk. Masawe.

Mtaalam wa magonjwa ya akinamama katika hospitali ya Peramiho Dk. Marieta Mtumbuka alisema kuwa mwezi Septemba mwaka 2012, wajawazito wawili walifika katika hospitali hiyo wakiwa na tatizo la kupoteza damu. Kati ya hao ni mmoja alikuwa na miaka 37.

Mjamzito akiumwa malaria na kucheleweshwa au kutokumaliza matibabu, anakuwa hatarini kupatwa na tatizo la kutokwa na damu. Ndiyo maana, kwa mujibu wa Dk. Rashid kuna umuhimu wa mjamzito kutumia dawa ya mseto kwa sababu ndio dawa pekee iliyofanyiwa utafiti na kugundulika inaweza kutibu na kumkinga mjamzito na mtoto aliye tumboni na malaria akitumia kipindi ambacho haumwi malaria.

“Wizara imeamua kupitisha dawa ya mseto baada ya tafiti mbalimbali kubaini dawa ya chloroquin inausugu wa kuzoeleka na wadudu wa malaria. Tulipotoka katika dawa ya chloroquin tukaanza matumizi ya dawa ya  fansider lakini nayo ikaonesha uwezo mdogo wa kukabiliana na wadudu wa malaria. Baada ya utafiti ndio tumegundua dawa mbadala ya kumkinga mjamzito na malaria ni dawa mseto,” alisema Dk. Rashid

Mjamzito anapewa dawa ya mseto akiwa na mimba ya wiki 20 na wiki ya 28.

Katika kitabu cha hotuba ya makadilio ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha 2012/2013, kinafafanua kuwa jumla ya dozi 9,196,080 za dawa mseto pamoja na kusambaza vyandarua vya hati punguzo vyenye viuatilifu 5,412579 kwa wanawake wajawazito lakini Lusiana hana chandarua.

"Nilipoanza kwenda zahanati kupima ujauzito wangu, sikupewa chandarua. Niliambiwa vimekwisha na sina uwezo wa kununua chandarua hivyo nalala bila ya kutumia hicho chandarua,"alisema Lusiana.
Aidha kwa mujibu wa bajeti ya afya ya mwaka 2012/2013, kumekuwa na ongezeko la vituo vya afya na zahanati za serikali na binafsi, kuanzia mwaka 2005 kutoka zahanati 4,322 hadi zahanati zahanati 4,679 mwaka 2012.

wa upande wa vituo vya afya, kumekuwa na ongezeko kutoka 481 mwaka 2006 hadi kufikia 742 mwaka 2012 na kwa upande wa hospitali kutoka 219 hadi kufikia 241. Hata bado kuna wanawake kama Lusiana wanaoshindwa kupata huduma za afya zenye ubora na kwa gharama wanazoweza kuzimudu.